loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Kili Stars yafufua matumaini Chalenji

TIMU ya Soka ya Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’ jana ilionja ushindi wa kwanza kwenye Michuano ya Kombe la Chalenji baada ya kuifunga Zanzibar Heroes bao 1-0 katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa KCCA , Kampala, Uganda jana.

Kilimanjaro Stars ambayo ilikuwa inahitaji ushindi kwa namna yoyote ili kufufua matumaini ya kuendelea kusalia kwenye michuano hiyo baada ya kufungwa mchezo wa awali na Kenya ilifunga bao hilo pekee dakika ya 38 kupitia kwa Ditrim Nchimbi akimalizia mpira uliotemwa na kipa wa Zanzibar Heroes, Ahmed Ali Suleiman.

Mchezo huo ambao Bara waliutawala kwa kiasi kikubwa ulijaa ushindani kutokana na wachezaji kufahamiana huku mchezaji wa Zanzibar Heroes, Mudathir Yahya akiumia na kushindwa kuendelea. Baada ya mchezo kumalizika kocha wa Kilimanjaro Stars, Juma Mgunda alisema mchezo ulikuwa na ushindani na hawamdharau yeyote hivyo watahakikisha wanapata ushindi kila mechi.

“Mechi ilikuwa ngumu ila tunashukuru tumeshinda. Sisi hatumdharau yeyote hivyo tutajipanga kuhakikisha tunapata ushindi ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kufuzu nusu fainali,” alisema Mgunda.

Naye kocha wa Zanzibar Heroes, Hemed Morocco alisema kukosekana kwa Ibrahim Hilika ambaye alioneshwa kadi nyekundu katika mchezo dhidi ya Sudan hakujawaadhiri kwa sababu ana kikosi kipana.

“Timu imecheza vizuri hatukuwa na bahati hivyo kukosekana kwa Ibrahim Hilika sijaona pengo lake kwa sababu nina wachezaji wengi ambao wanaweza kucheza nafasi yoyote ile,” alisema Morocco.

Katika michezo ya mwisho kwenye kundi B, Bara yenye pointi tatu itacheza na Sudan ambayo haina pointi na Zanzibar yenye pointi moja itaivaa Kenya yenye pointi sita Katika mchezo mwingine Uganda iliifunga Sudan kwa mabao 2-1 mabao yake yakifungwa na Hassan Abdallah na Oscar Wamalwa na lile Sudan likifungwa na Muhammad Namir. Maichuano hiyo inatarajiwa kuendelea leo kwa michezo ya Kundi A ambapo Eritrea itacheza na Uganda na Burundi itaivaa Djibouti.

LEO ndio fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) ...

foto
Mwandishi: Rahel Pallangyo

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi