loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Wizara yaanza kuhamasisha utalii wa ndani

WIZARA ya Maliasili na Utalii imeanza mkakati wa kuwatumia wakuu wa wilaya kuhamasisha utalii wa ndani.

Kutokana na hali hiyo, jana Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu aliongozana na wakuu wa wilaya saba kutoka wilaya mbalimbali nchini kwa ajili ya kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Burigi Chato iliyopo mkoani Kagera ili watambue fursa zinazopatikana ndani ya hifadhi hiyo mpya.

Kanyasu alisema sekta ya utalii ni sekta muhimu katika maendeleo ya nchi hivyo wakuu wa wilaya nchini wapatao 139 ni kundi muhimu katika kuwahamasisha wananchi wanaowangoza kuhusu umuhimu wa kutembelea hifadhi zilizopo nchini.

Akizungumzia sababu za kuwatumia wakuu wa wilaya hao, Naibu Waziri alisema mbali ya kuwatumia waandishi wa habari pamoja wasanii na watu maarufu, wakuu wa wilaya ni kundi muhimu kwa vile wao ni wenyeviti wa kamati wa ulinzi na usalama katika wilaya zao.

Kwa upande wake, Damiani Salu ambaye ni Mkuu wa hifadhi hiyo alisema ujio wa wakuu wa wilaya hao utasaidia kuchagiza utalii wa ndani kwa vile wao ni viongozi wanaowangoza watu hivyo watatumia ushawishi wao katika kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa kutembelea hifadhi nchini.

Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Festo Kiswaga aliipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kutumia makundi mbalimbali yenye ushawishi katika jamii kuhamasisha utalii wa ndani ambao umekuwa haufanyi vizuri.

Wakuu wa wilaya waliotembelea hifadhi hiyo ni Mkuu wa Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa, Asia Abdallah, Mkuu wa Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma, Mwanahamisi Munkunda, Mkuu wa Wilaya ya Momba mkoani Songwe, Jumaa Irando pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Temeke mkoani Dar es Salaam, Felix Lyaniva.

Wengine ni Mkuu wa Wilaya ya Gairo mkoani Morogoro, Siriel Mchembe, Mkuu wa Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma, Deogratias Ndejembi pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu, Festo Kiswaga.

Hifadhi ya Taifa ya Burigi Chato ni miongoni mwa hifadhi mpya iliyozinduliwa miezi michache iliyopita na Rais John Magufuli, na kufanya idadi ya hifadhi za taifa Tanzania kufikia 22.

WAZIRI wa Nchi Ofi si ya Rais, Tawala za Mikoa ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Maalumu, Chato

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi