loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

DC: Asikitishwa kufungwa kwa viwanda vya kuchakata miti

MKUU wa Wilaya ya Mufindi, Jamhuri William amepokea kwa masikitiko taarifa ya uwepo wa baadhi ya viwanda vya kuchakata miti vinavyofungwa wilayani mwake na kuziagiza mamlaka zinazohusika kuchunguza sababu zake ili kuweka mipango itakayosaidia kuvinusuru.

Taarifa hiyo ilitolewa juzi katika kikao cha wadau wa sekta ya misitu wa wilaya hiyo kilicholenga kujadili mafanikio na changamoto mbalimbali zinazowakabili wawekezaji katika sekta hiyo wakati wakiuaga mwaka 2019 na kujiandaa kuukaribisha 2020.

“Taarifa ya baadhi ya viwanda kufungwa zinakwenda kinyume na matarajio ya Rais anayetaka kujenga Taifa la Viwanda; Tukikaa kimya bila kuchukua hatua, sisi tutakuwa tatizo,” alisema William na kuziagiza mamlaka za chini yake kumpelekea taarifa ya viwanda vilivyofungwa na sababu zake.

Taarifa ya viwanda hivyo kufungwa iliibuliwa na mkurugenzi wa moja ya kampuni kubwa za uzalishaji wa mbao wilayani humo, Komas Sawmill Ltd, Audax Mshumbusi aliyesema wapo baadhi ya wafanyabiashara anaowafahamu walioanzisha viwanda vya kuchakata magogo na baada ya muda mfupi walisitisha uzalishaji na kuvifunga.

Mshumbushi alitoa taarifa hiyo baada ya Kaimu Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wa wilaya hiyo, Ernest Kagali kusema Wilaya ya Mufindi yenye wakazi zaidi ya 300,000 ina walipakodi wasiozidi 4,500.

Meneja huyo wa TRA alisema idadi hiyo ya walipa kodi ni ndogo kwa sababu baadhi ya wafanyabiashara wanakwepa kusajili biashara zao kama moja ya njia wanayotumia kukwepa kulipa kodi mbalimbali za serikali.

“Viwanda vingi vya kuchakata magogo, vilianzishwa wilayani Mufindi lakini baadhi yake vimekufa. Hii inatupata mtihani, kwanini vinafungwa,” alisema Mshumbushi na kuiomba serikali tathmini ya viwanda vilivyoko Mufindi ili kujua vinavyofanya kazi na visivyofanya kazi.

Naye Katibu wa Umoja wa Wavunaji wa Miti katika shamba la Taifa la Sao Hill (UWASA), Dk Basil Tweve alisema mbali na baadhi ya viwanda kufungwa, baadhi ya wavunaji wa miti katika shamba hilo ambao ni wanachama wao, wamehama Mufindi na maeneo mengine katika harakati zao za kutafuta mazingira rafiki ya biashara.

foto
Mwandishi: Frank Leonard, Mafinga

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi