loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Utamaduni unavyojenga taasisi kimaadili

KATIKA toleo hili, tunaangalia namna utamaduni uliopo katika utumishi wa umma, unavyoweza kusaidia katika ujenzi wa taasisi zinazozingatia maadili kutekeleza majukumu yake, ili kuweka mazingira mazuri ya kutoa huduma bora kwa wananchi, kwa mujibu wa sheria.

Utamaduni wa taasisi unaweza kuhusisha uhusiano baina ya watumishi, namna wanavyowasiliana, namna wanavyoandaa malengo yao, namna wanavyotekeleza majukumu yao ili kufikia malengo hayo na namna wanavyoweza kupima utendaji wao wa kazi na matokeo ya shughuli zao.

Kwa ujumla, utamaduni wa taasisi yoyote una uhusiano mkubwa na maadili, kwa vile utamaduni mzuri unaweza kuwasaidia watumishi kuteleza majukumu yao vizuri, huku wakizingatia maadili na hivyo kuleta manufaa makubwa kwa umma wa kupitia huduma wanazopata.

Kwa mfano, taasisi ikifanikiwa kujenga utamaduni wa watumishi kupenda malipo halali yanayotokana na kazi walizozifanya, watumishi wa umma hawatakuwa na nafasi kudai malipo bila kazi au malipo kwa kazi ambazo kimsingi ni sehemu ya majukumu yao ya kila siku yanayowafanya watumishi hao walipwe mshahara wao.

Vilevile taasisi ikifanikiwa kuwajengea watumishi utamaduni wa kutanguliza maslahi ya taasisi mbele badala ya watumishi kutaka kujinufaisha wao binafsi kwa kila jambo wanalolifanya, watumishi hao watakuwa wanaopenda kutoa huduma bora kwa wateja wote bila kuwapendelea wateja wenye uwezekano mkubwa wa kuwanufaisha watumishi hao binafsi.

Aidha, ukijengwa utamaduni wa kujisomea katika taasisi, kuna uwezekano mkubwa wa watumishi umma kusoma miongozo mbalimbali inayowazunguka na kuizingatia katika utekelezaji wa majukumu yao, badala ya kufanya kazi zao kwa mazoea, kufanyia kazi hata kwa urahisi masuala yanayohitaji kusoma nyaraka mbalimbali zilizoandikwa kwa kirefu na kujipatia maarifa zaidi ya jumla kwa ajili ya ufanisi wa kazi za taasisi.

Vilevile iwapo taasisi itawajengea watumishi wake utamaduni wa kupenda kujifunza kutoka kwa watumishi wengine kupitia michango ya hoja zao, watumishi waliopo katika uongozi watakuwa na uwezo wa kutoa nafasi ya kusikiliza walioko ngazi za chini na watumishi wa ngazi za chini hawataogopa kutoa mawazo yao ya kitaalamu pale wanapotakiwa kufanya hivyo kwa manufaa ya taasisi husika.

Utamaduni wa kujenga uhusiano mzuri na watumishi wengine wakiwamo watumishi wa juu na wa chini, uutaondoa uwezekano wa baadhi ya watumishi kuwachukulia wenzao wenye uhusiano mzuri na watumishi wengine na wenye kupenda kujituma, kama watu wanaopenda kujipendekeza na wenye viherehere na kuwafanya watumishi wafanye kazi zao kwa bidii na kwa ushirikiano.

Vilevile, taasisi ikifanikiwa kuwajengea watumishi utamaduni wa kutumia muda wao wa kazi kwa shughuli za kikazi tu, watumishi wataondokana na mambo yanayoweza kuwapotezea muda katika utekelezaji wa majukumu yao, ikiwa ni pamoja na matumizi ya simu binafsi za mikononi kwa mambo binafsi nyakati za kazi na kutumia ofisi kwa ajili ya kuwapokea wageni binafsi na kufanya mazungumzo binafsi.

Aidha, taasisi inaweza kutekeleza majukumu yake vizuri kwa kuzingatia maadili, endapo itafanikiwa kuwajengea watumishi utamaduni wa kuthamini mali za umma na hivyo kuondokana na upotevu au uaharibifu wa mali hizo, ili kuwa na rasilimali muhimu kwa ajili ya kutekelezea majukumu mbalimbali. Kuna mambo mengi yanyoweza kufanywa na taasisi kujenga utamaduni mzuri utakaosaidia kuhakikisha inatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia maadili.

Kwa mfano, taasisi husika inatakiwa kuhakikisha kuwa tabia ya uadilifu inayoanzia kutoka kwenye mawazo yenye uadilifu, inaweza kuwa sehemu ya utamaduni wa taasisi kwa watumishi kuelimishana wenyewe kwa wenyewe kuhusu mambo muhimu, maadili ya utumishi wa umma na yale ya kitaaluma.

Aidha, ni vizuri taasisi za umma zikatengeneza tamko la dhati, linaloonesha hamu ya kila mtumishi ya kutekeleza majukumu yake vizuri na kwa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma na maadili ya kitaaluma.

Pia ni vizuri watumishi walio madarakani wakajiweka kama mfano wa kuigwa na watumishi wengine, katika kufanya kazi zao vizuri wakizingatia maadili ya utumishi wa umma na maadili ya kitaaluma.

Aidha, kanuni za maadili ya utumishi wa umma na maadili ya kitaaluma lazima ziwe ni sehemu ya utamaduni wa taasisi, kwa kuziingiza ipasavyo katika mfumo mzima wa mapitio na tathmini ya utendaji kazi wa watumishi wa taasisi.

Vilevile ni vizuri jamii ikaanza kutumia vizuri aina mbalimbali za kauli, ikiwa ni pamoja na tamathali za semi, nahau na methali zinazohamasisha watu kupenda uadilifu badala ya kuwa na matumizi mabaya ya kauli kama vile ‘mbuzi hula kwa urefu wa kamba yake’, ‘kizuri kula na nduguyo’ au hata ile inayotokana na lugha ya Kiingereza kama vile ‘nikune mgongoni kwangu na mimi nikukune mgongoni kwako.’

Zaidi ya hayo, utamaduni wa watumishi wa umma kuzingatia maadili katika utekelezaji wa majukumu yao, unaweza kujengwa kwa kuhakikisha Watanzania wanajengewa misingi ya maadili, ili wanaotoka katika jamii kuingia katika taasisi za umma, waingie wakiwa na ari ya kazi kwa uadilifu na vilevile jamii inakuwa mstari wa mbele katika kushabikia vitendo vya uadilifu.

Mfano mzuri katika kuhakikisha Watanzania wnajengewa misingi ya maadili, unaoneshwa na Rais John Magufuli katika hotuba zake mbalimbali anapoeleza madhara ya ukiukwaji wa maadili kwa taifa na namna jamii inavyopaswa kupambana na ukiukwaji huo.

Kifo cha Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamini Mkapa ...

foto
Mwandishi: Dk Alfred Nchimbi

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi