loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Tanesco kununua magari 106 kuwafuata wateja

SHIRIKA la Umeme Tanzania (Tanesco) linapanga kununua magari 106 kwa ajili ya uboreshaji wa utoaji wa huduma kwa wateja ikiwamo kitengo cha dharura kwa ajili ya kuwahudumia wateja baada ya kupata kibali cha ununuzi.

Aidha, shirika hilo limesema uboreshaji wa mfumo wa umeme katika kituo cha kupoza umeme cha Ubungo, Dar es Salaam unatarajia kukamilika Desemba 19, mwaka huu na hivyo kuboresha upatikanaji wa umeme nchini.

Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Dk Tito Mwinuka, alisema hayo juzi mjini Morogoro kwenye hotuba yake kabla ya kumkaribisha Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Mohamed Utaly, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Loata Sanare, kufungua mkutano wa Baraza la 49 la Wafanyakazi wa Tanesco.

Dk Mwinuka alisema shirika linatambua kuwapo kwa changamoto ya uhaba wa magari ya kufanyia kazi, hivyo ili kukabiliana na hali hiyo litanunua magari 106 ambayo yatawezesha kuboresha huduma kwa wateja na tayari kibali cha ununuzi kimeshatolewa na shirika lipo kwenye taratibu za manunuzi.

Akizungumzia makusanyo ya fedha, alisema yamepanda hasa kwa wateja wakubwa, akitolea mfano wa makusanyo ya Oktoba, mwaka huu yalikuwa ni Sh bilioni 160.4 ikilinganisha na makusanyo ya Sh bilioni 155.9 Oktoba mwaka 2018. Hata hivyo, alisema licha ya kuimarika kwa makusanyo hayo, deni ambalo shirika linadaiwa ni Sh bilioni 952 na upande wa hasara imezidi kupungua. Alisema kipindi cha mwaka wa fedha 2015/16 hasara ilikuwa ni Sh bilioni 349.56, wakati mwaka wa fedha 2018/19 hasara imepungua hadi kufikia Sh bilioni 44.63.

“Hali hii inaonesha kuwa, mwelekeo wa shirika ni mzuri hivyo nawasihi wafanyakazi wenzangu tuendelee kuchapa kazi kwa bidii ili tufikie azma ya shirika kupata faida,” alisema Dk Mwinuka.

Kuhusu uboreshaji mfumo wa umeme katika kituo cha kupoza umeme cha Ubungo, alisema transfoma mpya ya megawati 240 itakayokuwa na uwezo wa kupokea umeme wa msongo wa kilovoti 220 kutoka kwenye Gridi ya Taifa uko katika hatua za mwisho za ujenzi na kazi hiyo inatarajiwa kukamilika Desemba 19, mwaka huu.

“Kama mnavyofahamu kwa muda mrefu shirika limekuwa na uhitaji wa transfoma ya kuboresha mfumo wa umeme katika Kituo cha Kupoza Umeme cha Ubungo, transfoma hii inahitajika ili kuboresha upatikanaji wa umeme katika jiji la Dar es Salaam na Zanzibar,” alisema Dk Mwinuka.

Kuhusu wafanyakazi wasio waaminifu, Dk Mwinuka alionya hawatamvumilia yeyote atakayebainika kujihusisha na vitendo viovu, bali atafikishwa kwenye vyombo vya dola na shirika halitakuwa tayari kuendelea naye na kazi.

MGOMBEA ubunge kwa tiketi ...

foto
Mwandishi: John Nditi, Morogoro

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi