loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

RITUNGU Ngoma ya Wakurya inayopandisha mori vijana

“KAMA mtu ni mwizi, mvivu au malaya; awe wa kike au wa kiume, ni wakati wa ngoma ya Ritungu vijana wanapojigamba ndipo mtu huyo husemwa na kusimangwa. Hufi kia hatua wengine wakalia, labda kutokana na ulemavu wao, umaskini au basi pengine hata wakidhani labda uyatima wao ndio umekuwa chanzo cha masimango. Mara nyingi huamua kupigana kufuatia mwelekeo wa hisia za masimango.”

Anasema Samweli Keraryo mzaliwa wa Itiryo wilayani Tarime anapozungumzia ngoma maarufu ya Wakurya iitwayo Ritungu. Wao huiita, “Iritungu.”

Wakurya ni miongoni mwa makabila yanayopatikana katika Mkoa wa Mara hasa katika wilaya za Tarime, Musoma na Serengeti. Huu ni kati ya mikoa inayopatikana Tanzania. Upo Kaskazini Mashariki mwa Tanzania na unapakana na nchi za Kenya na Uganda ukiwa na wilaya sita za Musoma, Bunda, Butiama, Serengeti, Tarime na Rorya. Makabila makuu ya Mkoa wa Mara ni Wakurya, Wajaluo na Wajita. Wakurya ni kabila kuu la wilaya za Tarime na Serengeti.

Wajita ni kabila kuu la Wilaya za Musoma na Bunda. Wajaluo ni kabila kuu la Wilaya ya Rorya. Makabila mengine yaliyopo mkoani humo ni Wazanaki, Wangoreme, Wasuba, Waikizu, Waisenye, Waikoma, Wakwaya, Waruri, Washashi, Wanata na Wasweta. Wakurya wana mila na desturi zao, ikiwemo sherehe za tohara. Utamaduni wao ni hai katika hali zote.

Vyanzo mbalimbali vinasema, wanayo matambiko kadhaa ya kila mwaka na kuwapa watu nyadhifa mbalimbali, mila ya kuoa na kuolewa, jando na unyago kupitia ngoma za Ritungu. Turudi na kujikita katika ngoma ya Ritungu ambayo imekuwa sehemu muhimu ya utamaduni wa jamii hiyo. Samwel Keraryo maarufu Munge akiwa mjini Tarime anasema ngoma hii inachochea ari ya mapambano kwa vijana.

Anasema: “Kwa mfano, kama mwanangoma amejitapa hata akamsimanga mwingine kwamba ni mvivu, au ni maskini au uchokozi wowote, aliyesimangwa au kufanyiwa kejeli anaweza kuamua ama kuondoka, au ‘kuliwasha’ hapo hapo yaani kuanzisha ugomvi.”

Hata hivyo, Munge anasema kuondoka kwa mtu huyo, mara nyingi hakumaanishi kuwa ameepusha shari, bali kwenda kutafakari kwa nini amedhalilishwa huku akitafakari kwa kujiuliza, ‘ighanke ansere igho’ yaani kwa nini amenidharau namna hiyo.”

Kwa mujibu wa uchunguzi, kwa jamii hiyo ambayo sasa imeanza kubadilika, mara nyingi hali hiyo huhitimishwa kwa ugomvi unaoweza kuwa wa mtu na mtu, au familia/ ukoo na nyingine. Bibi mmoja aliyekataa jina lake lisitajwe mkazi wa kijiji cha Nyambiri wilayani Butiama, alisema inapotokea wakati wa kucheza Ritungu, mchezaji akijigamba kwa kuzungumza maneno.

Kisha akamkejeli, kumsimanga au kukashifu mwingine hata pengine akafichua uvumi uliokuwapo kuwa fulani ana uhusiano mbaya na mkewe; wao husema ‘alamolya ebhelenge’ yaani anamhujumu,’ na hapo ndipo mwenye mali hupandwa jazba na mori inayohitimishwa kwa ugomvi dhidi ya mbaya wake.

Bibi huyo anasema: “Ngoma hii inayochezwa huku jamii wa rika mbalimbali wakiwemo vijana na wazee wakiishuhudia, huchochea moyo wa ushujaa wa kupambana na adui hususan wezi wa ng’ombe, ushirikiano katika kufanya kazi mbalimbali kama kilimo, ujenzi na ulinzi”.

Mugheko Sanchawa wa kijiji cha Sirorisimba wilayani Butiama anasema, wakati wa kucheza ngoma hii, vijana hupata fursa ya kujitangaza kuwa wako tayari kuoa au kuolewa na hata kila mmoja wao hutaka aoneshe ujasiri wake kwamba haogopi kitu na yuko tayari kupambana na adui yeyote anayepinga maendeleo yake.

“Iritungu hutumika katika kipindi cha jando; hasa baada ya vijana kutoka jandoni na sherehe mbalimbali zinazokwenda sambamba na shughuli za jando, harusi, mavuno na hata viongozi mbalimbali wa serikali ngazi ya taifa hupendelea kuitazama na kushiriki wanapoiona uwanjani ‘ikifanya vitu vyake.’

“Ma-Dj” wa ngoma hii ya Wakurya hutumia gitaa la kamba nane (ritungu), vibuyu viwili vinavyowekwa aina fulani ya mbegu au changarawe ili kutoa sauti vinapotikiswa, filimbi ndefu za matundu na hizi za kawaida, pamoja na makopo yanayofungwa miguuni mwa mpiga filimbi (amaghoroo).

Mpiga ritungu pia huwa na fimbo yenye aina fulani ya vikopo maalumu vyenye vyuma ndani yake vinavyofungwa kwenye fimbo hiyo anayoitikisa kwa kutumia dole gumba la mguu, hutoa sauti nzuri inayomithilishwa na sauti za kengele ndogo za kanisani.

Uchunguzi wa makala haya umebaini kuwa, kwa kawaida ngoma hii inayoimbwa kwa lugha asilia ya Kikurya ikiwa na maudhui mbalimbali kutegemea wakati na tukio husika, huchezwa huku wasichana wakiwa vifua wazi, lakini wakihifadhi maeneo nyeti kwa staha za Kibantu na hali wamejifunga vazi rasmi la kanga kwa mtindo maalumu.

Wavulana hujipanga katika mstari kila baada ya idadi kadhaa ya nyimbo na ndipo kila msichana huenda kumchagua mvulana anayemtaka ili acheze naye. Kwa baadhi ya koo za Wakurya, mtindo huo huitwa kwa Kikurya “cholo.”

Vyanzo hivyo kwa nyakati tofauti vinabainisha kuwa, wavulana huwa na kawaida ya kuwa na silaha kama rungu au fimbo ambazo hucheza huku wamezishikilia mikononi; wakiruka na kuzirusha shingo zao nyuma na mbele.

Kwa watazamaji wageni, mchezo huu huogopesha na hata kuonekana kuwa huwachosha wanangoma. Kwa wenyeji, ni ngoma inayofurahisha, inayovutia na isiyochosha kabisa. Inapotokea mara kwa mara msichana akamchagua mvulana mmoja tu kucheza naye, hisia nyingi tofauti huanza kujengeka miongoni mwa wanajamii na hata wenyewe kwa wenyewe yaani mvulana na msichana huanza kutazamana kwa “aibu za kishujaa” na hapo mara nyingi huwa mwanzo na kichocheo kikubwa cha ndoa za kutoroshana kwa vijana hao.

Hii haina maana kwamba ndio makusudio ya ngoma hiyo, bali hali hii hukemewa na kulaaniwa na jamii husika kwani ndoa hizo huwa ni kinyume cha maadili ya ndoa za Kikurya.

Mara nyingi hutokea kwamba kijana wa kiume ambaye hachaguliwi katika cholo, hujisikia chuki na moyo wa wivu kumtawala dhidi ya yule anayechaguliwa mara kwa mara na wakati mwingine, kuchaguliwa na wasichana wengi huku wengine wakikosa. Hivyo, anayeachwa mara nyingine huamua ‘kuzua vagi’ dhidi ya yule mwenye bahati ‘inayomtilia usiku’, hapo pia ugomvi mkubwa mara nyingi huweza kutokea.

Ugomvi unaweza kuanza baina ya mtu na mtu, ukawa baina ya kikundi na kikundi na pengine hata kuwa ugomvi wa ukoo na ukoo. Mara nyingi watu wa kabila la Wakurya hawapendi kumaliza ugomvi kwa mapatano yanayoonesha kuwa fulani kashinda. Kwao, kukubali kushindwa au kumaliza mambo kwa maridhiano, ni kama kuonesha udhaifu. Hata hivyo, mambo sasa yanazidi kubadilika.

“Kijana mmoja anaitwa Osama (si jina halisi) wa Kijiji cha Kitaramanka wilayani Butiama aliwahi kupigwa kwa kiboko kwa kuwa eti wasichana wengi walikuwa wanamchagua katika cholo kwa wakati mmoja na hali vijana wengine wakiwa hawapati msichana hata mmoja,” anasema Mgaya Wambura anapozungumzia ngoma hiyo.

Ingawa ni vema kudumisha ngoma hiyo inayochochea ujasiri, ushujaa, ushirikiano na mengine mengi mazuri, ni vema jamii husika ya Wakurya ikakaa chini na kuchambua kuyatoa mabaya yote yaliyomo na yale yalipitwa na wakati kama ugomvi na kwenda kucheza ukiwa na silaha, hali inayoweza kuhatarisha amani na usalama wa watazamaji na wachezaji wenyewe.

Mazuri yaliyo katika uchezaji wa ngoma ya Ritungu kama kuchochea ujasiri na ushirikiano katika kupambana na adui wa jamii wakiwamo wezi wa mifugo kijijini na vijiji jirani, ni jambo muhimu kwa kuwa linaendeleza dhana ya ulinzi shirikishi na kuimarisha umoja katika jamii.

Miongoni mwa mambo mazuri kwa Wakurya ni kuwa, hata kama mlikuwa maadui mchana, jioni mtu akipata tatizo kama la kuvamiwa na majambazi au kuibiwa mifugo, tofauti zile za mchana huzikwa na wote kuwa nguvu moja kupambana na adui.

foto
Mwandishi: Joseph Sabinus

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi