loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mihuri serikali za mitaa yazua zogo, wananchi wahoji

MATUMIZI yasiyo sahihi ya mihuri ya wenyeviti wa vijiji na mitaa yameendelea kuwaumiza wananchi kutokana na kutozwa fedha pale wanapohitaji huduma hiyo kwenye ofi si hizo.

Hali ni mbaya zaidi kwa wananchi wenye hali duni za maisha ambao baadhi wameshindwa kupata huduma za mihuri kwenye barua au fomu za maombi na kuuza mali za familia kugharamia. Wakazi wa Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya waliohudhuria Maadhimisho ya Kilele cha Siku ya Maadili kwa Watumishi wa Umma kata ya Kyimo wamedai hayo wilayani hapa karibuni.

Maonesho hayo yaliandaliwa na Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Utumishi wa Umma Kanda ya Nyanda za Juu Kusini. Diwani wa Viti maalumu kata ya Kyimo, Emmy Masseta alisema bado wananchi wengi vijijini hawatendewi haki na wenyeviti wa vijiji wanaowataka walipie huduma ya kugongewa mihuri na kuhoji msimamo wa serikali katika jambo hilo ni upi.

Mkazi wa Kijiji na Kata ya Kyimo, Marley Mwabulambo alisema mwenyekiti wa kijiji chao amekuwa akiwatoza Sh 3,000 na zaidi akigonga mhuri kulingana na kipato cha mtu. “Kuna haja ya kuwatazama kwa jicho la tatu wenyeviti wetu kwani wapo baadhi hata wanaposhughulikia suala la mauziano ya ardhi, asilimia 10 ya fedha inayotakiwa kupelekwa kwenye halmashauri ya kijiji haionekani na pia waliohusika kulipa asilimia hiyo hawapewi stakabadhi.

Kwanza mwananchi kutozwa huduma ya muhuri ni sheria?” Alihoji Mwabulambo. Akijibu hoja hizo, Mkuu wa Sekretarieti ya Maadili ya Utumishi wa Umma Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Paul Kanon alisema msimamo wa serikali ni mihuri yote kuwa chini ya watendaji wa mitaa, vijiji na kata na si wenyeviti wa vitongoji akisisitiza kuwa huduma ya kugongewa mihuri inapaswa kuwa bure si malipo.

Aliwataka wananchi kutambua ofisi za mitaa na vijiji zinaendeshwa kwa kasma ya serikali na si fedha zitokanazo na kuchangishwa, hivyo huduma zinapaswa kutolewa bure huko.

“Serikali ilitangaza mihuri iwe chini ya maofisa watendaji na si wenyeviti. Mwenyekiti wa mtaa au kijiji na Ofisa Mtendaji wakitoza fedha za muhuri ni ukiukaji maadili ya utumishi wa umma hivyo msilipe pesa kupewa huduma,” alisisitiza Kanon.

Akitoa mada ya Maadili ya Utumishi wa Umma kwenye maadhimisho, Ofisa Maadili Ofisi ya Sekretarieti ya maadili ya utumishi wa umma Kanda, Gideon Mwafili aliwataka wananchi kutofumbia macho maovu yanayofanywa na viongozi wao.

Alisema maeneo ya vijijini kwenye mizizi ya serikali kuna malalamiko ya uwajibikaji wa watumishi wa umma na viongozi, jambo ambalo likipuuzwa lina mchango mkubwa kuporomoka maadili ya viongozi na watumishi wa serikali ngazi za juu.

Akimwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Chalya Julius kwenye maadhimisho hayo, Ofisa Tawala wilayani hapa, Amimu Mwandelile aliwataka wananchi wanapowataja viongozi wasio na maadili wawe na uzalendo na kutaka wanaoifuata wapewe haki stahiki na kuwaongezea moyo wa kujituma kazini.

foto
Mwandishi: Joachim Nyambo, Rungwe

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi