loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mimba za utotoni, upigaji wanawake vyatawala unyanyasaji kijinsia Kilwa

MIMBA za utotoni, upigaji wanawake, kurithiwa bila hiari, kunyimwa mali za mume ni sehemu ya unyanyasaji wa kijinsia unaofanyika katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Kilwa mkoani Lindi.

Aidha imeelezwa kuwa wanajamii wamekuwa wakitoa visingizio vingi, ikiwamo mila na desturi katika kukwaza maisha ya wanawake ili wasiweze kuinuka na kujipatia furaha na uhuru wa kiuchumi. Hayo yalisemwa na wadau mbalimbali waliokuwa wakizungumza katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Kupinga Ukatili wa Kijinsia wilayani Kilwa, hafla iliyofanyika Kilwa Masoko.

Wamesema pamoja na kukosa kazi za staha, wanawake kushikwashikwa hovyo miili yao wanapofanya biashara, talaka zinazotolewa kama njugu zimenawaumiza na kuwafanya wawe watumwa wa maisha.

Walitaka mikakati kumaliza ukatili unaonyima wanawake na watoto uhuru wa kijamii na kiuchumi. Mohamed Kitotiko kutoka asasi ya Kingonet alisema wanawake na watoto wamekosa misingi ya maisha yenye staha kwa kukosa elimu ya uraia na pia kutambua misingi ya usawa na haki kwa kila mwananchi.

Alisema jamii inatoa visingizio kuhalalisha ukatili huo, hivyo wakati umefika jamii kujitambua na kuacha visingizio ikiwamo mimba za utotoni kwamba zimepelekwa na wafugaji wakati ndio wanaficha wahalifu.

Zaida Ndemu wa kijiji cha Namayoni alisema ukatili wa kijinsia upo mwanamke kuitwa kibiritingoma.

“Unafanya kazi zako za mama lishe, mtu anakuja anakushikashika maungo yako bila ridhaa. Inaudhi sana na wakati mwingine unapofanya biashara pale watu wanakuona kama kahaba, hii inakera,”alisema.

Mwenyekiti wa kitongoji cha Magofuni, Kilwa Kivinje alisema unyanyasaji wa kijinsia upo hasa ndoa inapoharibika kwani watoto na mama yao huachwa bila msaada, hivyo kuwaingiza katika mazingira hatarishi.

Akipokea maandamano, Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Christopher Ngubiagai alisema yapo mambo ambayo halmashauri ya wilaya itayafanyia kazi hasa mitaji na masoko ya bidhaa za wanawake na makundi yao.

Aidha aliiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kushughulikia unyanyasaji hasa kwa kuwakamata waliosababisha mimba za utotoni, wanaodai rushwa za ngono na kukiuka sera ya ajira.

“Takukuru itusaidie, hili la watoto wadogo kuwa na mimba si sawasawa. Tangu Januari hadi Oktoba kuna mimba 53 na kuna kesi za ulawiti na ubakaji 28. Huu ni ukatili uliopitiliza,” alisema Mkuu huyo.

Pia alizungumzia mkakati mkubwa wa kuigeuza Kilwa kuwa na kazi za staha hasa kutokana na kilimo na utalii na kusema kuna mambo makubwa wilaya imepanga ili kuongeza kipato cha wananchi wake Kilwa. Katibu wa Jukwaa la wanawake katika Wilaya ya Kilwa, Pili Kuliwa aliwataka wananchi wa Kilwa kukabiliana na ukatili wa kijinsia kwa kuwa wazi na kutumia vyombo vilivyopo katika kudai haki zao.

Mratibu wa Shirika la ActionAid Kilwa, Stevie Bernad ambaye shirika lake limekuwa mstari wa mbele kukabiliana na ukatili wa kijinsia amesema kwamba shirika lake limefanya tafiti katika wiki nzima na kubaini kwamba wanawake wanahitaji msaada mkubwa wa kisheria ili kukabili ukatili huo.

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu, Kilwa

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi