loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

BoT yaagizwa kudhibiti vitendo vya utapeli

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango ameiagiza Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kusimamia kikamilifu Sheria ya Huduma za Fedha ya 2018, inayodhibiti vitendo vya utapeli, vilivyokuwa vikifanywa na watoa huduma na wapokea huduma hizo.

Mpango alisema hayo wakati wa kuzindua Mpango wa Elimu wa Umma kuhusu Sera, Sheria na Kanuni za Huduma ndogo za Fedha jijini hapa jana. Alisema tatizo la vitendo vya utapeli ni kubwa, hivyo BoT wanatakiwa kusimamia sheria hiyo 2018, ambayo inadhibiti vitendo hivyo.

“Benki Kuu ya Tanzania wasimamie sekta hii kikamilifu ili michezo michafu inayochezwa na watoa huduma ndogo za fedha kwa upande mmoja na wapokea huduma kwa upande mwingine ikome!” alisema.

Alisema serikali imechoka kusikia vilio vya wananchi, wanaotumia wa huduma ndogo za fedha kutokana na kunyanyaswa na wakati mwingine kuchukuliwa vitu vyao ili kulipia madeni waliyokopa. Mpango aliwataka BoT pia wasimamie kikamilifu utoaji huduma za fedha kupitia mitandao ya kidigitali ili kuhakikisha zinafanyika kikamilifu kwa kufuata sheria, sera na kanuni za huduma hiyo.

“Benki Kuu ya Tanzania ifuatilie kwa makini sana mwenendo wa utoaji huduma ndogo za fedha kupitia mita” alisema.

Alitaka Wizara ya Fedha kuifanya elimu kwa umma kuwa endelevu isambae nchi nzima ili wananchi watumiaji wa huduma za fedha, wajue sheria, sera na kanuni ambazo zinalenga kuwainua watu masikini wa kipato cha chini.

Alisema takribani wananchi milioni 15.4 sawa na asilimia 55.3 ya nguvu kazi ya taifa, wanatumia huduma ndogo za fedha na kuwa zimekuwepo sheria za kusaidia kutambua na kulinda haki zao.

Mpango alisema Sheria hiyo ya 2018, Sera ya 2017 na Kanuni za Huduma ndogo za Fedha za 2019 ambazo zimeanza kutumika tangu Novemba 1, mwaka huu, zitasaidia watoa huduma na wapokeaji huduma hiyo kuzifuata na kuepuka adhabu kutokana na kuzivunja sheria hizo.

Alisema kabla ya sheria ya kusimamia sekta ya huduma ndogo za fedha kutungwa, kulikuwa na changamoto nyingi kadhaa zikiwemo za wananchi kutozwa riba kubwa, kukosekana kwa uwazi wa masharti ya mikataba ya mikopo na kutopatikana kwa takwimu sahihi za uendeshaji taasisi za fedha.

“Kutokuwepo kwa taratibu za kisheria na kutokuwa na matakwa ya sheria ya udhibiti wa utakatishaji wa fedha haramu, kulitumika kama mwanya ya utakatishaji wa fedha haramu kwa taasisi zinatozotoa huduma hiyo,”alisema.

Mpango alisema kutokana na kukosekana kwa sheria, wananchi walitozwa viwango vikubwa vya riba na tozo kuanzia asilimia tatu hadi 20 kwa mwezi, sawa na asilimia 36 hadi 240 kwa mwaka, jambo ambali lilileta madhara makubwa kwa watumiaji wa huduma hiyo.

“Pia mikopo ilitolewa kiholela na kusababisha malimbikizo ya madeni kwa wateja, utaratibu usiofaa wa kukusanya madeni uliosababisha wananchi kupoteza mali zao na wasio waaminifu kutoa huduma kiholela,” alisema.

Mwakilishi wa Gavana wa BoT, Profesa Florens Luoga, Meneja wa Kanda ya Kati ya mikoa ya Tabora, Singida, Morogoro na Dodoma, Robert Wambari alisema benki hiyo imejipanga kusimamia sheria na kanuni zake tano kwa ajili ya watoa huduma na wapokeaji kuzifuata.

MASHIRIKA mbalimbali ya kimataifa ya usafiri ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu, Dodoma

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi