loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Waliomua kinyama mtoto wasakwa

Mkuu wa Bunda mkoani Mara, Lydia Bupilipili ameliagiza jeshi la polisi wilayani humo, kuwasaka wahusika wote wa tukio la mauaji ya kinyama ya mtoto Rahma Waryoba (6).

Rahma ambaye ni mkazi wa mtaa wa Bunda Stoo katika Halmashauri ya Mji wa Bunda, aliuawa kinyama kwa kunyongwa na watu wasiojulikana na kisha mwili wake kutelekezwa katika eneo la Maisha Plus hivi karibuni.

Bupilipili ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya, alisema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake. Alisema kuwa katika kipindi hiki, yametokea mauaji ya kikatili, yakiwemo ya mtoto huyo mdogo.

“Kwa siku za hivi karibuni yametokea matukio ya mauaji hapa wilayani Bunda, tena mengine ya kikatili kama hilo la mtoto mdogo aliyeuawa katika eneo la Maisha Puls mtaa wa Bunda stoo, tukio hilo linasikitisha sana. Sasa ninamuagiza OCD kufanya uchunguzi wa kina kuhusu tukio hilo na mengine yote ili waliohusika wakamatwe na kufikishwa mahakamani,” alisema.

Bupilipili alisema mtoto huyo mdogo alifanyiwa kitendo cha kikatili, maana inadaiwa alibakwa kisha kuuawa, kitendo hicho kamwe hakiwezi kuvumiliwa. Mkuu huyo wa wilaya alitaja matukio mengine kuwa ni mwanaume mmoja asiyejulikana jina wala makazi yake, aliyeuawa na watu wasiojulikana na mwili wake kutupwa katika eneo la Butakare. Tukio lingine ni la mwendesha bodaboda aliyekutwa ameuawa eneo la Mzani mjini Bunda.

Aliuawa na watu wasiojulikana, ambao walimpora pikipiki yake na kutokomea nayo. Pia kuna mwananchi mmoja aliyekuwa mlinzi katika eneo la Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola alikutwa amekufa gesti katika eneo la Nyasura mjini hapa.

Alisema kutokana na matukio hayo ya mauaji, polisi wilayani Bunda wafanye upelelezi wa haraka ili waliohusika na mauaji hayo wakamatwe na kufikishwa mahakamani. Wakati huo huo, Mkuu huyo wa Wilaya alimtaja mwanaume mmoja, Mchaina Mkama (33) mkazi wa Namarama wilayani hapa, kuwa amemuua mke wake Jeska (25) kisha na yeye akajinyonga kwa kutumia kamba juu ya mti wa mwembe.

Tukio lingine ni mwanamke mmoja aitwaye Chausiku, mkazi wa Kijiji cha Mwisenyi, amekamatwa na kuliwa na mamba wakati akioga katika Ziwa Victoria. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Daniel Shilla, alifafanua kuwa mtoto aliyeuawa ni mwanafunzi wa chekechea. Alisema kwamba jeshi hilo linaendelea na upelelezi wa matukio hayo na linafanya msako ili kuwatia mbaroni wahusika.

BARAZA la Mitihani la Tanzania (NECTA) limesisitiza ...

foto
Mwandishi: Ahmed Makongo, Bunda

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi