loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

MINAMINO Nimekuja Liverpool kupiga kazi

JUMATANO iliyopita mabingwa watetezi wa Ligi ya mabingwa Ulaya na vinara wa Ligi Kuu England, Liverpool, walikamilisha dili la kuinasa saini ya Takumi Minamino.

Liverpool wameipata saini ya mchezaji huyo raia wa Japan baada ya kuilipa Red Bull Salzburg ya Austria pauni milioni 7.25 na inaaminika amesaini mkataba wa miaka minne na nusu.

Haikuwa rahisi kwa Liverpool kumpata mchezaji huyo anayeimudu vema nafasi ya ushambuliaji kwani kulikuwa na klabu kadhaa Ulaya ambazo nazo zilikuwa zikimuhitaji ikiwemo Manchester United. Liverpool ndio waliokuwa na hamasa kubwa ya kuhakikisha wanafanya juu chini ili kumpata mchezaji huyo ambaye ana umri wa miaka 24 baada ya kuonesha kiwango kizuri katika michezo yao miwili ya Ligi ya Mabingwa Ulaya katika hatua ya makundi. Liverpool walikuwa kundi E mbali na Red Bull Sulzburg ambao walimaliza nafasi ya tatu pia ilikuwepo Napoli na Genk.

Minamino amepewa jezi namba 18 na atajiunga rasmi Anfield Januari mosi ambapo dirisha la usajili litakua limefunguliwa. Baada ya kujiunga na timu hiyo kuna uwezekano mkubwa akawepo katika kikosi kitakachocheza dhidi ya Everton kwenye Kombe la FA Januari 5. Akizungumzia usajili wake huo Minamino anafunguka kuwa ilikuwa ni ndoto yake siku moja kucheza Liverpool na amefurahi ndoto yake imetimia.

Anaongeza kuwa baada ya kutimiza ndoto yake hiyo hakuna cha kufanya zaidi ya kupiga kazi ya maana ambayo itainufaisha Liverpool kwa kipindi chote atakachokuwa klabuni hapo. “Hii ilikuwa ndoto yangu ya muda mrefu, nilikuwa natamani mno kuwa mchezaji wa Liverpool, nimefarijika sana kuona ndoto yangu imetimia hii leo. Minamino ambaye ni mmoja kati ya wachezaji wa timu ya taifa ya Japan ambapo mpaka sasa amecheza mechi 22 alianzia katika Klabu ya Cerezo Osaka kati ya mwaka 2012 na 2014 kisha akajiunga na Red Bull Salzburg (2015).

Katika msimu huu ameisaidia klabu yake kuongoza ligi huku akipachika mabao saba na kutengeneza matano. Minamino anaongeza; “Licha ya kuiwazia Liverpool lakini pia nilikuwa ninamalengo ya kucheza Nimekuja Liverpool kupiga kazi MINAMINO Ligi Kuu England, hakuna asiyefahamu kama ligi hii ni moja kati ya ligi bora duniani, nilikuwa naumiza kichwa maisha yangu ya soka yatamalizika bila kucheza katika ligi hii.?”

“Kuna muda ulifika nikawa siamini kama nitacheza Liverpool lakini baada ya kila kitu kutimia kiukweli nimefurahi, sina cha kufanya zaidi ya kukomaa kufanya kazi ya maana... “Nimebahatika kucheza dhidi ya timu hii katika mechi mbili na nimegundua kuwa timu hii inacheza kwa kutumia mbinu za kiufundi mno pamoja na nguvu sana… “Asikwambie mtu ukicheza na Liverpool kwa sasa unahisi kabisa ni timu bora na ubingwa wa Uefa waliouchukua walistahili hasa… “Malengo yangu ni kubeba kombe la EPL pamoja na Ligi ya Mabingwa Ulaya, sio kubeba tu bali hata mchango wangu uonekane.”

Katika kuonesha kuwa mchezaji huyo amekuja kuwa msaada mkubwa kwa Liverpool kuzidi kupata mafanikio kocha wa miamba hiyo, Jurgen Klopp, hakusita kumwagia sifa na kumuhakikishia kumpa ushirikiano mkubwa.

“Huu ni moja kati ya usajili bora kwetu kiukweli tuna furaha mno kukamilisha dili hili. “Mashabiki wetu tayari wameshaona kiwango chake hivi karibuni hivyo sina sababu ya kuzungumzia sana kiwango chake.

“Takumi ni mchezaji mwenye kasi, akili, anajua kutafuta nafasi ya kufunga hatari akiwa na mpira lakini pia hata akiwa hana mpira ni hatari pia, akishika mpira huwa na faida kwake pamoja na faida kwa wenzake maana anaweza kufunga yeye au akamtengenezea mwenzake. “Kucheza Ligi ya Mabingwa ni tiketi yake ya kuingia moja kwa moja katika kikosi naamini atatupa kitu ndani ya muda mfupi.

Minamino anaweza kumudu kucheza katika nafasi ya ushambuliaji kwenye mfumo wa 4-3-3 pia anaweza kubeba jukumu la namba 10 hivyo Klopp ataamua nani amuweke benchi kati ya Roberto Firmino, Mohamed Salah na Sadio Mane.

“Sio jambo la ajabu kuona klabu kama Salzburg kuwa na mchezaji kama huyu hatari na mwenye kiu ya mafanikio. “Kwa kile tulichokiona katika mechi mbili tulizocheza nao naweza kusema Salzburg inaonesha wazi kuwa ni moja ya timu ambayo italiteka soka la Ulaya hivi karibuni.

“Nina uhakika mkubwa mashabiki wote wa Liverpool watamfanya Takumi ajihisi kama yupo nyumbani. “Pia na mimi nafurahi kuongeza wanafamilia wapya wa Liverpool kutoka Japan, najua kuna raia wengi wan chi hiyo wataanza kutufuatilia kwasababu tuna mchezaji wao,” anafafanua Klopp.

foto
Mwandishi: LIVERPOOL, England

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi