loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Wachimbaji wapinga mgawanyo tozo

WACHIMBAJI wadogo wa madini ya almasi, wanaounda vikundi vinavyotarajia kupokea marudio ya mchanga wa madini kutoka Mgodi wa Williamson Diamond Ltd (WDL), wametofautiana na serikali kupitia Tume ya Madini kuhusu mgawanyo wa asilimia za tozo za madini hayo, wakidai zimelenga kunufaisha baadhi ya watu na sio wao.

Walisema hayo kwenye kikao cha kuvitambua vikundi hivyo, vitavyopewa marudio hayo ya mchanga, kilichoketi Kata ya Songwa chini ya uenyekiti wake Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Nyabanga Taraba.

Wachimbaji hao walisema wamegomea baadhi ya tozo, wakidai zimelenga kumnufaisha mtu mmoja ama kikundi cha watu fulani. Baadhi ya wachimbaji hao, Onesmo Jidawa na Gulusan Hassani, walilalamika kutoshirikishwa katika mchakato mzima wa mgawanyo wa asilimia.

Walidai kuwa asilimia 70 iliyotengwa kwa ajili ya mkandarasi, anayetengeneza miundombinu ya barabara na eneo la kuhifadhia makinikia chini ya Mbunge wa Jimbo la Kishapu, Suleiman Nchambi, ni kubwa na itamnufaisha mwenyewe na sio wachimbaji wadogo kama ilivyokusudiwa.

“Sisi hatutaki hiyo asilimia ni kubwa, kwani wakati wanaipanga hawakutushirikisha, hivyo tunaomba serikali ikae upya itushirikishe tupange kwa pamoja kila kundi liweze kunufaika kuliko hivi sasa linanufaisha kampuni moja ambayo inamilikiwa na mbunge wa jimbo hili,” alisema Soela Ndalu.

Ofisa Madini Mkoa wa Shinyanga, Joseph Kumburu alisema asilimia 70 inayokwenda kwa mkandarasi huyo, imetokana na kukosa mtu wa kujitolea kufanya kazi hiyo na baadaye alipwe kutokana na upatikanaji wa almasi.

Kumburu alisema kupitia Sheria ya Madini na makubaliano na Chama cha Wachimbaji Wadogo Mkoa wa Shinyanga (SHIREMA), asilimia 15 itaenda kwa mchimbaji mdogo, asilimia 0.3 halmashauri, asilimia 7 Ofisi ya Madini, 15 ya mwenye shamba na nyinginezo ambazo baadhi wachimbaji wadogo wamepinga, wakidai hawakushirikishwa.

Kilicholalamikiwa kingine ni tozo ya Sh 200,000 inayotozwa na Shirema kwamba imelenga kuwanyong’onyeza, wakati serikali iliona busara wapewe marudio hayo ili kujikwamua na hali ngumu ya maisha waliyonayo.

Hata hivyo, ofisa madini huyo aliitaka Shirema kusitisha kuchaji tozo hiyo kwa sasa na kwamba itakatwa wakati mauzo ya almasi yatakapoanza Mkuu wa wilaya aliwataka wachimbaji hao kuheshimu sheria, taratibu na miongozo ya serikali ili kufikia lengo lao na kwamba ambaye hayupo tayari anaweza kufanya vitu vingine ikiwemo kilimo.

Katibu Mkuu wa Shirema, Gregory Kibusi alisema tozo hiyo ya Sh 200,000 ipo kwa mujibu wa Katiba ya Shirema inayotaka ili kutambuliwa na chama hicho ambacho ndio kimeingia mkataba na Mgodi wa WDL, ni lazima awe mwanachama hai.

KATIBU Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Leonard Akwilapo, ...

foto
Mwandishi: Kareny Masasy, Kishapu

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi