loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Gesi asilia; mbinu sahihi kubana  matumizi ya fedha kwa wenye magari 

RIPOTI ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2015/16, ilifichua udhaifu katika mradi wa bomba la usafirishaji gesi asilia kati ya Mtwara na Dar es Salaam, ilipobainisha kiwango kidogo cha matumizi ya gesi hiyo nchini.

Katika ripoti yake hiyo, CAG alieleza kuwa bomba hilo lililojengwa na Kampuni ya Maendeleo ya Petroli na Teknolojia China (CPTDC)kwa gharama ya Dola za Marekani bilioni 1.283 (Dola bilioni 1.225 zikiwa ni mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Exim ya China), ujenzi wake ulifanyika kabla ya kutafuta wateja wa gesi hiyo. 

CAG alibainisha kuwa hali hiyo inasababisha ukakasi katika marejesho ya mkopo yaliyotegemea kupatikana kwenye mauzo ya gesi asilia baada ya kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa bomba na kuanza kutumika kibiashara.

Wakati makadirio ya mauzo halisi ya gesi asilia ni futi za ujazo milioni 138.8 kwa siku, CAG alibaini Shirika la Umeme (Tanesco) ndiyo mteja pekee wa gesi hiyo na anatumia wastani wa futi za ujazo milioni 46.61 kwa siku, hivyo matumizi ya bomba hilo ni ya asilimia sita tu ilhali malengo yalikuwa kusafirisha gesi kwa ajili ya matumizi ya kuzalisha umeme, viwandani, kupikia majumbani na matumizi ya magari.

Kampuni ya Pan African Energy kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) wanakiona kikwazo hicho katika matumizi ya gesi asilia na kuanzisha mradi wa kujaza gesi kwenye magari katika kituo chao cha Ubungo Maziwa jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi Mtendaji wa Pan African Energy Tanzania, Andy Hanna, anasema wamekuwa wakitoa huduma za kujaza gesi magari kwenye kituo hicho cha gesi wakiwa wabia wa TPDC kwa kuhakikisha huduma za gesi na wameendelea kuhakikisha huduma zinawavutia wengi ili kubadili mfumo.

“Tunatoa huduma kwa zaidi ya magari 100 kwa siku na huduma zetu ni za saa 24. Na hii imezidi kuwa njia mojawapo ya kuwavutia watu wengi kupitia wale tunaowahudumia, lakini tatizo lipo kwani kituo ni kimoja tu na hakipo kwenye eneo rafiki kibiashara.

“Mifumo hii iliyopo kwenye kituo hiki tuliifunga miaka tisa iliyopita, na hadi sasa idadi ya magari yanayopata huduma ni zaidi ya 300. Kwa sasa, ni watanzania wachache wanafurahia kutumia gharama ndogo kwenye uendeshaji wa magari.

"Kama wangefahamu wengi zaidi manufaa ya kutumia gesi badala ya mafuta kwenye magari na vituo vikaongezeka, basi wanufaika wangekuwa wengi, lakini pia utunzaji wa mazingira ungeongezeka kwani asilimia 72 ya kinachotoka kwenye mafuta ya petroli na dizeli huchafua mazingira,” anaeleza.

Katika kituo hicho cha kujaza gesi kwenye magari, HabariLeo inakutana na dereva teksi, anayejitambulisha kwa jina moja la Ezekiel, anayesema ana miezi saba tangu aanze kutumia gesi kwenye gari lake aina ya Toyota IST analolitumia kwa biashara hiyo.

Ezekiel anasema: “Mimi ni dereva wa gari hili la biashara, kwa kweli sasa nafurahia kutumia gesi badala ya mafuta kwenye gari, matumizi ya fedha ni kidogo. Nikiweka kilo 10 za gesi kwenye gari langu, naliendesha kwa kilometa 170 bila ya kupata adhaa yoyote, tena kwa gharama nafuu kwani kilo moja kwa sasa tunauziwa shilingi 1,550.

“Zamani nilikuwa nikitumia zaidi ya lita 30 kwa kilometa 170, tena hiyo ni pale unapokuta hakuna msongamano wa magari, na kama unavyojua kwa kipindi cha miaka ya hivi karibuni, petroli imekuwa ikiuza kati ya shilingi 2,150 na 2,350,” anasema.

Dereva teksi mwingine, James Osward, naye anasifu matumizi ya gesi kwenye magari, akieleza kuwa gharama za nishati kwa ajili ya magari yake sasa zimepungua baadala ya kuanza kutumia gesi.

“Nina magari mawili ya biashara, yote ni Toyota IST. Hadi sasa, nina miezi sita tangu nilipobadilishia mfumo wa hili moja na ndilo ninalolitumia ninapokuwa kwenye shughuli zangu za kubeba abiria.

"Kwa kweli sasa ninafurahia kupata unafuu mkubwa linapokuja suala la matumizi nya fedha kwa ajili ya nishati kwenye gari. Nilipokuwa ninatumia petroli, nilikuwa nikitumia fedha nyingi ukilinganisha na sasa. 

"Lakini jambo hili wengi wamekuwa hawalielewi mpaka pale mtu atakapopata fursa la kutumia gari linalotumia gesi. Mtazamo wangu ni kuwa miaka ijayo watu wengi watahamia huku maana unapofunga mfumo huu, matumizi yanapungua marudufu,” anasifu.

Ramadhani Yasin, dereva wa basi dogo la abiria, maarufu daladala, linalofanya safari zake kutoka Gongo la Mboto na Stesheni, anasema amekuwa na maisha mazuri tangu mwajiri wake alipoamua kuunganisha mfumo wa gesi kwenye gari hilo aina ya Toyota Coaster.

“Aisee, siku hizi ninaona fedha imenikubali, kuunganishwa kwa mfumo wa gesi kwenye gari kunanipa faida, na bosi wangu naye anapata.

"Zamani nilikuwa nikimpelekea hesabu shilingi 80,000 kwa siku, lakini kwa sasa napeleka 'laki moja' (Sh. 100,000) wakati huohuo mimi nabaki na shilingi 50,000 tofauti na zamani ambapo nilikuwa nikipata shilingi 20,000 kwa siku.

“Kwenye matumizi, kwa siku ninaweka gesi kilogramu 25 asubuhi na 25 jioni, lakini zamani nilikuwa nikinunua dizeli ya mpaka shilingi 160, 000 kwa siku, faida ilikuwa kidogo,” anaeleza dereva huyo ambaye anasisitiza itakuwa ngumu kukubali kuajiriwa na mmiliki wa gari lisilokuwa na mfumo huo wa gesi.

TRILIONI 30 ZAOKOLEWA

Kwa mujibu wa TPDC, kwa kipindi cha miaka 15, tangu Tanzania ilipoanza kuzalisha na kusambaza gesi, imeokoa kiasi cha Sh. trilioni 30, ambazo zingetumika kuagiza mafuta nje kwa ajili ya kuzalisha umeme na uendeshaji wa viwanda.

Mkurugenzi wa TPDC, Dk James Mataragio anasema kiasi hicho cha fedha kingetumika kwenye ununuzi wa mafuta kwa ajili ya umeme wa mafuta, lakini kutokana na uwapo wa gesi asilia, takribani asilimia 54 ya umeme unaozalishwa nchini unatumia gesi asilia, huku nishati hiyo pia ikitumika viwandani na pia kwenye magari.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi inayojishughulisha na Utafiti wa Sera (Repoa), Dk. Donald Mmari, anasema utumiaji wa gesi unaweza kuwa chanzo cha mapato makubwa ya taifa.

“Nchi nyingine tunaweza kuona kama vile China, Malaysia na India, magari yote ya kijamii yakiwamo mabasi yanatumia gesi asilia na kufanya gharama ya uchukuzi kushuka chini. Ni wakati sasa kuitumia sekta hii,” Dk. Mmari anashauri.

VITUO KUONGEZWA

Kamishna Msaidizi wa Gesi wa Wizara ya Nishati, Sebastian Shana, anasema kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya gesi asilia kwenye magari huku huduma hiyo ikiwa inatolewa kwenye kituo kimoja, serikali inakusudia kutengeneza vituo vingine viwili vikubwa kwa ajili ya kusambaza gesi kwenye vituo vingine vidogo vilivyoko jijini. 

Shana anasema takribani magari 300 nchini yanatumia gesi kama mbadala wa mafuta, huku mengi zaidi yakiendelea kubadilishwa mifumo ili yatumie nishati ya gesi.

Agosti 21 mwaka huu, Mkurugenzi wa TPDC, Dk. Mataragio, katika wasilisho lake kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, alisema kutokana na ongezeko la magari yanayotumia gesi, kituo cha majaribio kilichoko Ubungo, kinashindwa kuhimili matakwa ya matumizi, hivyo shirika limejipanga kujenga kituo kikubwa eneo la Sam Nujoma jijini humo.

“Kituo hicho kinachotarajiwa kukamilika Oktoba 2020, kitatumika kujazia gesi katika magari pamoja na kupeleka gesi maeneo ambayo miundombinu ya mabomba ya gesi bado haijafika,” aliahidi.

MWENDOKASI KUNEEMEKA

Dk Mataragio pia alisema TPDC inalenga kuupatia gesi asilia mradi wa mabasi ya mwendokasi (DART), akieleza kuwa kwa kuanzia, kituo cha kujazia gesi kwenye magari kitajengwa eneo la DART, depoti ya Ubungo Oktoba mwakani.

Alisema shirika lilikubaliana na DART kuwezesha kuweka vituo maalum vya gesi katika depoti ya Gongo la Mboto na Mbagala ili kupunguza gharama za uendeshaji wa mabasi hayo, lakini pia kupunguza nauli kwa wananchi.

Mratibu wa Mradi wa Matumizi ya Gesi Asilia kwenye Magari (CNG Vehicle Project) kutoka Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), Dk Esebi Nyari anasema wanaendelea kuunganisha magari kwenye mfumo wa matumizi ya gesi asilia badala ya petroli na kwamba hadi sasa, magari zaidi ya 100 yameunganishwa kwenye karakana yao.

Dk. Nyari anasema mfumo huo wa kuunganisha gesi asilia unasaidia kupunguza gharama kwa wamiliki wa magari na kwamba kiasi kidogo cha gesi asilia kinatumika kwa umbali mrefu.

“Mfumo huu una faida nyingi, kilogramu moja ni shilingi 1,550 huku petroli lita moja ikiwa ni wastani wa shilingi 2,200, ukiweka gesi asilia kilogramu moja unaweza kwenda zaidi ya kilometa 20 huku petroli lita moja inakwenda kilometa zisizozidi 12. 

"Mtungi wa gesi asilia wa kilogramu 15 (shilingi 23,250) unaweza kutumika kutembea zaidi ya kilometa 200 tofauti na petroli,” anafafanua.

Kuhusu gharama za kubadili mfumo, mtaalamu huyo anasema kuwa mwenye gari lenye 'cylinder' nne, wanatoza Sh milioni 1.8 na kwa zaidi ya hapo bei inapanda kidogo.

"Cylinder 'nne ni shilingi milioni 1.8, ukiwa na gari lenye 'cylinder' zaidi ya hapo bei inapanda lakini hii ikitokea kutatokea kampuni au taasisi mbalimbali za ufundi zitafanya kazi ya kuunganisha magari, basi bei ya uunganishaji itashuka...

"...Serikali pia ikiangalia namna fulani ya kutoa msamaha wa kodi kwa baadhi ya vifaa vya kuunganishia vinavyotoka nje ya nchi, huenda watu wanaotumia gesi wanaongezeka kutoka 300 waliopo sasa kwani bei ya kuunganisha itakuwa chini," anasema Dk Nyari.

Kwenye kuunganisha mfumo, DIT ndiyo pekee inafanya kazi hiyo kwa sasa nchini kwa inashirikiana na kampuni ya wazawa ya Energo Tanzania Limited ambayo inashughulikia teknolojia na DIT hao wanahusika zaidi kwenye ufundi wa mfumo huo.

Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja, anasema ni wakati sasa nchi kuongeza kasi kwenye uvunaji wa gesi asilia. Anasema ili uchumi wa nchi upige hatua, ni vyema rasilimali zake zikatumika kwa usahihi.

Ngeleja ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini, anasema: “Wenye maamuzi (serikali) waangalie jinsi gani watafanyia kazi utafiti uliofanywa na wadau mbalimbali wakiwamo Repoa kuhusu gesi. 

"Kuna juhudi kubwa zinazofanywa na Rais John Magufuli pamoja na wasaidizi wake, lakini tunahitaji kuongeza kasi kwenye uvunaji wa gesi ili iweze kunufaisha taifa. Dunia haitusubiri, tuvune tulichonacho kwa ajili ya vizazi. Kama vitatumika vizuri, tutafika mbali.

KATIBU Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Leonard Akwilapo, ...

foto
Mwandishi: Alfred Lasteck

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi