loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Sheria inavyoruhusu pingamizi la jina katika daftari la wapigakura

KABLA ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa Rais na Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Madiwani wa Tanzania Bara, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) inalo jukumu la kisheria la kuboresha daftari la kudumu la wapigakura.

Lengo la uboreshaji huo ni kutoa fursa kwa Watanzania wenye sifa za kupigakura kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapigakura ili waweze kutumia haki yao ya kikatiba ya kupigakura katika uchaguzi mkuu unaofanyika nchini.

Umuhimu wa Tume kuboresha Daftari la Kudumu la Wapigakura unatokana na ukweli kuwa, idadi ya watu wenye sifa za kuwa wapigakura inaongezeka kila mwaka. Kwa mantiki hiyo, Tume inapaswa kuhakikisha ongezeko hilo la watu wenye sifa za kuandikishwa kuwa wapigakura nalo linapewa fursa hiyo ya kujiandikisha.

Kifungu cha 15(5) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 na Kifungu cha 21(5) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa Sura ya 292, vinaitaka Tume kuboresha Daftari la Kudumu la Wapigakura mara mbili katika Uchaguzi Mkuu mmoja uliomalizika na Uchaguzi Mkuu mwingine unaofuatia.

Msisitizo huu wa kisheria ndio umekuwa dira na mwongozo wa Tume katika utekelezaji wa jukumu lake la kufanya maboresho ya daftari la kudumu la wapigakura. Katika kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020, NEC ilianza rasmi kazi ya uboreshaji wa daftari la kudumu la wapigakura kwa awamu ya kwanza Julai 18, 2019 ambapo lilizinduliwa kitaifa mkoani Kilimanjaro.

Kazi hiyo hadi sasa imekamilika katika mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara ambayo ni pamoja na Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Simiyu, Mara, Mwanza, Kigoma, Tabora, Songwe, Kagera, Geita, Shinyanga, Katavi, Rukwa, Singida, Dodoma, Iringa na Mbeya Pamoja na lengo kuu la uboreshaji wa dafatari la kudumu la wapigakura kuwa ni kuingiza wapigakura wapya waliofikisha umri wa kupiga kura (miaka 18) au watakaofikisha umri huo ifikapo tarehe ya uchaguzi mkuu ujao, kazi hiyo pia inayo malengo mengine.

Kwa mujibu wa NEC, malengo mengine ni pamoja na kuondoa wapigakura waliokosa sifa kama vile waliofariki, kurekebisha taarifa za wapigakura zilizokosewa na kuhamisha taarifa za wapigakura waliohama kutoka eneo moja la uchaguzi kwenda eneo lingine la uchaguzi.

Sambamba na hili, Tume baada ya kukamilisha uboreshaji wa daftari la kudumu la wapigakura, huweka wazi daftari la awali la wapigakura. Miongoni mwa sababu za Tume kuweka wazi daftari hilo ni kutoa fursa kwa wapigakura walioandikishwa kuhakiki taarifa zao, kurekebisha taarifa zao zilizokosewa kama vile majina n.k pamoja na kuweka pingamizi dhidi ya jina lisilokuwa na sifa lililomo katika daftari la kudumu la wapigakura.

Hata hivyo, si kila mwananchi anaruhusiwa kuweka pingamizi dhidi ya jina lililomo katika daftari la kudumu la wapigakura, bali ni wale tu wanaoruhusiwa kwa mujibu wa sheria ni mkurugenzi wa uchaguzi, ofisa mwandikishaji na mtu yeyote aliyeandikishwa katika eneo la uchaguzi. Hivyo, mtu yeyote aliyeandikishwa katika daftari la kudumu la wapigakura katika eneo husika la uchaguzi anayo haki ya kuweka pingamizi dhidi ya jina lake mwenyewe au majina ya watu wengine yaliyoandikishwa katika daftari hilo.

Ikumbukwe kuwa, ili mtu aweke pingamizi ni lazima jina lake liwemo katika daftari la awali la wapigakura kwenye eneo husika la uchaguzi. Kifungu cha 24 cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 kinaeleza kuwa, mtu yeyote ambaye jina lake lipo katika daftari la awali la wapigakura la eneo la uchaguzi, anaweza kupinga kuendelea kuwemo katika daftari la awali la wapigakura, jina lake mwenyewe au jina la mtu mwingine yeyote kwa sababu kuwa mtu huyo au mtu mwingine yeyote hana sifa au hana sifa tena za kuandikishwa au mtu mwingine huyo amefariki.

Kifungu hiki cha sheria kinamuwezesha mtu yeyote ambaye jina lake lipo katika daftari la awali la wapigakura la eneo la uchaguzi, kushiriki katika uandikishaji wa daftari la kudumu la wapigakura kwa kuhakikisha kuwa walioandikishwa ni wale tu wenye sifa hitajika.

Aidha, sheria hii inaimarisha ushirikiano wa Tume na wapigakura na hivyo, ni moja ya kiashiria kuwa Tume hutekeleza majukumu yake kwa uwazi na kwa ushirikiano kati ya Tume na wapigakura ambao ni miongoni mwa wadau muhimu wa Tume.

Mtu anaweza kujiuliza ni kwanini Tume inaruhusu wapiga kura kuweka pingamizi? Jibu ni rahisi tu kwamba, ni kwa sababu huenda kuna wananchi wasio kuwa na sifa walifanya udanganyifu na kuandikishwa katika daftari la kudumu la wapigakura na watendaji wa Tume hawakuweza kubaini udanganyifu huo mapema wakati wa zoezi la uandikishaji.

Pia, huenda kuna wapigakura waliokuwa na sifa, lakini wamefariki hivyo wanapaswa kuondolewa katika daftari la kudumu la wapigakura. Kifungu Namba 25 (2) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi Sura ya 343 kinaeleza kuwa, kila pingamizi mbali na pingamizi iliyowekwa na mkurugenzi wa uchaguzi au ofisa mwandikishaji, itawasilishwa ikiwa imeambatana na dhamana ya kiasi cha fedha kama ambavyo Tume inaweza kwa Tangazo litakalochapishwa katika gazeti la Serikali, kuelekeza.

Aidha, pingamizi litatakiwa kuwasilishwa ndani ya siku saba kuanzia siku ya mwisho ya uwekaji wazi daftari la awali. Pingamizi hilo litawasilishwa kwa kujaza fomu namba 3B na kuambatanisha kiasi cha fedha kama ambavyo Tume ya Taifa ya Uchaguzi itakavyoelekeza.

Ofisa mwandikishaji baada ya kupokea pingamizi hilo, atamtaarifu aliyewekewa pingamizi sababu ya pingamizi ndani ya siku 7 na kumtaka atoe maelezo ya utetezi kwa maandishi. Isipokuwa, ofisa mwandikishaji hatapaswa kupeleka taarifa endapo pingamizi imewekwa kwa sababu ya kuwa mtu ambaye jina lake liko katika daftari la awali la wapigakura amefariki.

Kisha, ofisa mwandikishaji atatoa taarifa ndani ya siku 7 kuhusu tarehe, mahali na muda ambapo atasikiliza shauri hilo, na kufanya uamuzi wa kukubali au kukataa pingamizi hilo. Ofisa mwandikishaji atapaswa kufanya uchunguzi juu ya pingamizi hilo na kisha kutoa maamuzi. Ofisa mwandikishaji atatoa uamuzi kuhusu pingamizi iliyowekwa chini ya sehemu hii ndani ya siku saba tangu siku ya mwisho ya kutolewa kwa taarifa ya uchunguzi.

Pamoja na kifungu hiki cha sheria kumpa nafasi muweka pingamizi kuweka pingamizi na ofisa mwandikishaji kutoa uamuzi, bado kuna nafasi ya rufaa ikiwa uamuzi uliotolewa na ofisa mwandikishaji haukumridhisha mmoja kati yao (aliyeweka au aliyewekewa pingamizi).

Kifungu cha 27 (1) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi Sura ya 353 kinaeleza kuwa, endapo mweka pingamizi au mtu yeyote aliyewekewa pingamizi hakuridhishwa na uamuzi wa ofisa mwandikishaji chini ya Kifungu cha 26 mweka pingamizi au mtu huyo anaweza ndani ya siku saba kuanzia tarehe ya uamuzi kutolewa, kukata rufaa katika mahakama ya wilaya.

Mahakama itapaswa kutoa hukumu ya shauri hilo ndani ya siku 14 tangu tarehe ya rufaa hiyo kuwasilishwa mahakamani. Uamuzi wa mahakama ya wilaya ndio utakuwa uamuzi wa mwisho na mtu huyo hataruhusiwa kukata rufaa katika mahakama nyingine yoyote.

Hvyo, ili mtu yeyote aliyeandikishwa katika daftari la kudumu la wapigakura aweke pingamizi dhidi ya jina lolote lililopo katika daftari hilo na sheria tajwa ziweze kutumika, ni muhimu wananchi wote waliojiandikisha katika eneo la uchaguzi kufanya uhakiki wa majina mara tu daftari la awali la wapigakura linapowekwa wazi katika maeneo yao.

Subira Kaswaga ni Ofisa Habari wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

foto
Mwandishi: Subira Kaswaga

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi