loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Tanapa inavyopania Hifadhi ya Nyerere kuongeza watalii nchini

TANZANIA ni moja ya nchi chache duniani zilizobarikiwa kuwa na maliasili nyingi wakiwemo wanyamapori ambao wana umuhimu mkubwa kimazingira na kiuchumi.

hawa ni urithi wa asili na ni rasilimali yenye umuhimu mkubwa kitaifa na kimataifa na umuhimu wake umejikita katika thamani ya kibiolojia ya spishi husika na mazingira ya asili yaliyopo.

Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere katika hotuba yake ya mwaka 1961 baada ya kupata uhuru, alisema “Uhai wa wanyamapori ni jambo linalotuhusu sote katika Afrika.”

Mwaka huo wa 1961 wakati Tanzania inapata uhuru, kulikuwa na hifadhi za taifa tatu pekee; Serengeti, Ziwa Manyara na Arusha, zikiwa na jumla ya eneo lenye ukubwa wa kilomita za mraba 17,000.

Hadi kufikia mwaka 2015, kipindi ambacho Serikali ya awamu ya tano iliingia madarakani, Tanzania ilikuwa na hifadhi za Taifa 16 zenye ukubwa wa jumla ya kilomita za mraba 57,000. Katika kipindi cha miaka minne (2015-2019) tangu Serikali ya Awamu ya Tano ilipoingia madarakani, zimeongezeka hifadhi za taifa sita.

Hatua hii imeifanya Tanzania kupitia Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa), kuwa na jumla ya hifadhi za Taifa 22 zenye eneo la kilomita za mraba 104,000. Hifadhi mpya za Taifa zilizoanzishwa ni Burigi- Chato, Ibanda-Kyerwa na Rumanyika-Karagwe, Kigosi, Mto Ugalla na hifadhi ya Taifa ya Nyerere inayomegwa kutoka katika Pori la akiba la Selous.

Kutokana na kupandishwa hadhi kwa hifadhi ya Nyerere ambayo makala haya yanaimulika zaidi, mwezi uliopita Tanapa ilifanya vikao kazi kadhaa na wadau wa hifadhi hiyo, kimoja kikishirikisha wakuu wa mikoa ambayo hifadhi hiyo inapitia ya Pwani, Lindi, Ruvuma na Morogoro. Kupitia vikao hivyo vya kujengeana uelewa, Kamishna wa Uhifadhi wa Tanapa, Dk Allan Kijazi, anasema Hifadhi mpya Nyerere ni moja ya hifadhi kubwa duniani yenye vivutio vingi vya asili na wanyamapori.

Anasema hifadhi hiyo na nyingine mpya zilizoanzishwa zitachangia sana katika kuongeza idadi ya watalii, upatikanaji wa ajira na mapato kutokana na shughuli za utalii. Anasema moja ya mambo yanayotakiwa kufanywa ni kuondokana na usimamizi wa utalii wa picha na uwindaji kama ilivyokuwa awali kwenda kwenye usimamizi wa utalii wa picha pekee.

Anasema hifadhi hiyo yenye ukubwa wa kilometa za mraba 30,893 moja ya vivutio vyake visipopatikana kwingineko ni miti iliyogeuka kuwa mawe katika Kanda ya Kalulu, kusini mwa hifadhi, umbali wa kilometa 96 kutoka mjini Tunduru, mkoani Ruvuma Hifadhi ya taifa ya Nyerere pia imabarikiwa kuwa na wanyama watano wakubwa wa porini; tembo, faru, nyati, simba na chui.

Anafafanua kwamba wanyama hawa hawakuchanguliwa kwa kuangalia ukubwa wa miili yao ila ni kutokana ugumu wa kuwindwa na pia ndio wanyama hatari na wenye hasira kali kuliko wote. Dk Kijazi anafafanua kwamba Pori la Akiba la Selous lilikuwa na kanda nane na kwamba kwa sasa kanda sita miongoni mwa hizo ndizo zinaunda Hifadhi ya Taifa ya Nyerere na hivyo kanda mbili zilizobaki zinaendelea kuwa pori la akiba la Selous chini ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori nchini (Tawa).

Dk Kijazi anazitaja kanda hizo sita kuwa ni Matambwe ambayo ni maalumu kwa utalii wa picha, Msolwa, Ilonga, Kululu, Likuyu seka na Liwale. Dk Kijazi amewahakikishia Watanzania na Jumuiya ya Kimataifa ya kwamba watarajie kuona mabadiliko ya dhati ya uboreshaji na utendaji katika Hifadhi ya Taifa ya Nyerere ambayo anasema yatakidhi hadhi ya utalii wa picha unaoendana na viwango vya kimataifa.

Pia anawaondolea hofu wawekezaji wote wanaofanya shughuli za utalii wa picha na uwindaji kuwa, umewekwa utaratibu mzuri kipindi hiki cha mpito katika kuendelea na utaratibu uliokuwa unatumika chini Tawa.

Dk Kijazi anasema kufuatia mabadiliko hayo zipo shughuli zitasitishwa na nyingine zitakazoendelea ni zile tu zinazokubalika kwa mujibu wa sheria ya Tanapa. Katika kikao na wakuu wa mikoa, Dk Kijazi alitaka maoni ya wadau kuhusu namna bora ya kusimamia aneo la hifadhi katika kipindi hiki cha mpito ili kusitokee mtikisiko wa kibiashaera na pia kuboresha maeneo ya kiutenaji kwenye utalii wa picha.

Dk Kijazi anasema Tanapa ipo kwenye hatua za mwisho za kuachiana majukumu na wenzao wa Tawa na baada ya hapo watachukua jukumu rasmi la kuanza kusimamia hifadhi hiyo Januari hii.

“Katika hili niwaondoe hofu wawekezaji wote wanaofanya shughuli za utalii wa picha na uwindaji kwamba zimewekwa taratibu nzuri katika kipindi hiki cha mpito,” anasema Dk Kijazi.

Anaongeza: “Tutajitahidi kuendelea na utaratibu uliokuwa chini ya Tawa ili tusije kuleta mtikisiko wa kibiashara wakati huo huo tukiweka mifumo mizuri ya kuanza kusimamia eneo la Hifadhi ya Taifa ya Nyerere chini ya mfumo wa Tanapa.”

Anasema wawekezaji walio na mikataba ya uwandaji wa utalii hususani katika eneo la kusini mwa Selous wanabaki kuendelea na shughuli zao hadi mwaka 2021 mikataba yao itakapofikia ukomo. Anasema Tanapa inatarajia kununua helikopta mbili ili kuimarisha ulinzi na kuyafikia maeneo yasiyofika kirahisi kwa gari ili kukabiliana na vitendo vya ujangili kwenye hifadhi hiyo mpya ya Nyerere pamoja na eneo la bwawa la kufua umeme la Nyerere.

Anasema uimarishaji ulinzi kwenye hifadhi ya Taifa ya Nyerere ili kukomesha majangili utakuwa endelevu na kwamba Kitengo cha Intelijensia kitaimarishwa zaidi ili kuifayanya hifadhi hiyo kuwa salama muda wote.

Anasema Tanapa itashirikiana na maofisa wa wanyama pori wa halimashauri pamoja na wananchi wa vijiji jirani na hifadhi kwa kuwapa elimu na kuwaomba waendeleee kuwafichua majangili wanaojificha kwenye maeneo yao.

Dk Kijazi anasema uwepo wa maeneo ya hifadhi ni fursa kubwa ya kiuchumi kwa nchi kwani sekta hiyo imekuwa mojawapo ya sekta tatu kuu za kiuchumi ikichangia asilimia 17.5 ya pato la Taifa na asilimia 25 ya fedha za kigeni.

“Zaidi ya nusu ya wageni wanaokuja nchini hutembelea hifadhi za Taifa,” anasema na kuongeza kwamba jitihahada nyingi zimefanywa na serikali ya awamu ya nne katika kuongeza mapato kupitia utalii.

Naye Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Kitengo cha Uhifadhi, Godwell Meing’ataki, anasema Tanapa itaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu namna ya kutumia njia rafiki za kiasili za kuzuia wanyamapori waharibifu wa mazao wanaoingia kwenye mashamba yao.

Meing’ataki ametaja njia hizo kuwa ni pamoja kuweka mizinga ya nyuki kwenye njia ambazo wanyama wanapenda kupita, kupanda pilipili kwenye mipaka na kuweka kamba ambazo zinapiga kelele.

Naye mwakilishi Tawa, Zahoro Kimwaga, anasema mabadiliko katika kutoka pori la akiba la Salous hadi hifadhi ya Nyerere yanaenda katika utaratibu sawia na kwamba hayataleta matatizo kwa upande wa kibiashara.

Anasema Tawa itakuwa bega kwa bega kushirikiana na Tanapa kuhakikisha nia na madhumuni ya kubadilisha sehemu ya Pori la Akiba la Selous kuwa hifadhi ya Taifa ya Nyerere yanafanikiwa.

Kamishna mkuu wa TAWA, Dk James Wakibara, anasema kuwa Pori la Akiba la Selous kwa asilimia kubwa limekatwa kuwa Hifadhi ya Taifa ya Nyerere na kwamba Tawa itashirikiana na mamkala zingine katika kuimarisha ulinzi na usalama katika eneo lililobaki.

Mkuu wa mkoa wa Lindi, Gofrey Zambi, ameishauri Tanapa kuangalia namna bora ya kutatua changamoto mbalimbali zitakazojitokeza kwenye Hifadhi mpya ya Taifa ya Nyerere kutokana na uchanga wake ili kuendelea kuimarishwa uhusiano mwema na wananchi katika vijiji vinavyozunguka hifadhi hiyo.

Mkuu wa mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo anasema kikao hicho kimesaidia kamati za ulinzi na usalama za mikoa na wilaya zote zinazozunguka hifadhi ya Taifa Nyerere kuelewa shughuli mbalimbali zinazofanywa na Tanapa.

foto
Mwandishi: John Nditi

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi