loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Ujue Msitu wa Magoroto wilayani Muheza

MKOA wa Tanga una maeneo ya kitalii yanayoweza kuwavutia watalii wengi ndani na nje ya Tanzania, hasa kutokana na hali ya hewa na ukarimu wa watu wake.

Watu wa Tanga wanasifika kuwa na haiba ya ukarimu kama walivyo Watanzania wengi, jambo linaloweza kuwa kivutio kwa watalii wengi kutembelea mkoa huo. Kwa kawaida ukarimu huwavuta watalii wengi, kuwajengea hali ya usalama na kujifunza mengi kutoka kwa wenyeji wao.

Nimetembelea Mkoa wa Tanga mara kadhaa, na miongoni mwa maeneo niliyotembelea ni pamoja na mandhari ya kuvutia ya Milima ya Usambara, Mbuga ya Mkomazi, makumbusho ya kihistoria, Msitu wa Magoroto n.k.

Ukiachana na ukaribu wa Mkoa wa Tanga na Jiji la Dar es Salaam, kuna utajiri wa utamaduni wa Waswahili wanaopatikana katika pwani ya Bahari ya Hindi, shughuli za uchumi na kibiashara, pamoja na wanasiasa na wasanii mbalimbali wanaolipeperusha vyema jina la Mkoa wa Tanga.

Mkoa huu pia una historia nzuri katika burudani. Yapo machapisho mengi yanayoelezea kuwa, Tanga ndiyo kitovu cha burudani katika nchi hii, ukiwa na historia nzuri kuanzia soka, muziki, sinema na kadhalika.

Kwa upande wa vivutio vya utalii, Mkoa wa Tanga una vivutio ambavyo haviwezi kupatikana sehemu nyingine. Hivi ni kama Mbuga za Saadani ambayo ni matokeo ya Pori la Akiba la Saadani, Ranchi ya Mkwaja na sehemu ya Kaskazini ya Mkwaja sambamba na akiba ya msitu wa asili wa Zaraninge. Hifadhi hii inapatikana baina ya Mkoa wa Tanga na Pwani. Pia kuna Mbuga ya Mkomazi.

Mmkoani Tanga kuna maeneo kama vile Mapango ya Amboni, Mto Pangani na makumbusho ya kale yanayojulikana kama Urithi Tanga Museum, ambayo yamebeba historia na urithi wa mkoa huo tangu enzi za wakoloni.

Kwa kawaida, kila binadamu mwenye uhai anayefanya kazi kikamilifu kuna muda huwa anahitaji mapumziko. Mapumziko haya siyo ya usingizi wa siku moja, lakini muda mrefu ambao atautumia katika mazingira tulivu kurejesha mawazo, akili na mwili katika hali ya kawaida.

Hapa sizungumzii mapumziko ya kuacha shughuli za kiofisi au biashara na kutulia na familia nyumbani wakati wa likizo, au ya kuwatembelea ndugu na wazazi kijijini, bali kwenda kutembelea maeneo mbalimbali ya utalii ikiwa ni sehemu ya kubadilisha mazingira uliyoyazoea na kujifunza vitu vipya.

Kama wewe ni miongoni mwa watu wanaopenda utalii, sehemu sahihi ya kwenda kutembelea mwaka huu, ukiachana na maeneo hayo niliyoyaeleza, ni katika Msitu wa Magoroto uliopo wilayani Muheza, kilomita 37 kutoka jijini Tanga.

Msitu huo wenye ukubwa wa ekari 591 umelizunguka ziwa la maji masafi, ulifunguliwa mwaka 1896 na watawala wa Kijerumani kama shamba la kwanza la kibiashara katika Afrika Mashariki na baadaye ukahifadhiwa kama sehemu muhimu yenye uoto wa asili. Kwa mujibu wa Meneja wa Msitu wa Magoroto, Jeremiah Mchechu, mara ya kwanza shamba hilo lililima zao la mpira baada ya kushindwa kulima kahawa na chai na baadaye kulimwa michikichi mwaka 1921.

Eneo hilo lilichukuliwa na wazawa “Amboni Group” mwaka 1940 na kilimo cha michikichi kilisitishwa baada ya kuwepo ushindani kati yetu na nchi za Malaysia na Indonesia. Baada ya hapo, Msitu wa Magoroto ulihifadhiwa mpaka leo kwa kuzingatia upekee na uzuri wake.

Upekee wake ni kuwepo kwa Ziwa Magoroto lililotengenezwa na binadamu lenye viumbe mbalimbali wakiwemo samaki. Msitu wa Magoroto unatumika kama sehemu ya utunzaji wa mazingira kutokana na uwezo wake wa kuhifadhi uoto wa asili ambao haupatikani katika maeneo mengine mengi nchini. Pamoja na kupakana na msitu wa Mlinga, Magoroto inatengeneza vipande vya Milima ya Usambaraambayo inayofahamika kwa uzuri na upekee wa uoto wa asili.

Unafahamika zaidi kwa uwepo wa ndege wa kipekee ambapo Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco) na Chama cha Uhifadhi Wanyamapori wanahusika katika uhifadhi wa misitu hiyo nchini.

Mogoroto ni kivutio cha utalii siyo wilayani Muheza pekee, bali kwa mtu yeyote mwenye nia ya kutembelea eneo hilo kutokana na hali yake ya hewa kuwa nzuri huku ikiambatana na mandhari nzuri ya chini ya milima.

Eneo hili humpatia mtu mwonekano mzuri kutoka bonde la Muheza hadi Bahari ya Hindi na pia, litakuwezesha kuona mimea adimu na ndege au kutembelea katika mashamba ya zamani ya michikichi. Pia utapata nafasi ya kujifunza juu ya viungo asilia kama pilipili, karafuu, mdalasini, chai, vanila pamoja na vingine vingi vyenye umuhimu au kuogelea katika ziwa zuri la Magoroto.

Hili ni eneo adimu ambalo baadhi ya wasanii wa muziki wa kizazi kipya wamewahi kwenda kupiga picha za video kwa ajili ya nyimbo zao. Kwa mfano, video ya wimbo wa Amen ulioimbwa na Maua Sama akimshirikisha Ben Pol ilichukuliwa Magoroto, video ya wimbo wa The One wa Diamond Platnumz pia ilichukuliwa hapo.

Ki ukweli hili ni eneo zuri sana kutembelea na baadhi ya watu ambao wamewahi kufika eneo hilo wanaweza kukubaliana nami kuwa ni sehemu sahihi ya kutuliza akili.

Jeremiah Mchechu, wakati akizungumza na baadhi ya vyombo vya habari vya mtandaoni, alisema kuwa mtalii atakayefika eneo hilo ataweza kupanda milima, kutembea, kuendesha baiskeli, kuogelea kwenye Ziwa Magoroto, kuvua samaki, kuwaona ndege, kutembea msituni, kutembelea kavazi na eneo la viungo.

Pia ukifika hapo utapata fursa ya kucheza michezo mbalimbali na muziki nyakati za usiku. Magoroto ni sehemu ya kipekee kwa utalii na linaweza kuhudumia watu 30 hadi 40 kwa siku ili kuhakikisha mazingira ya asili ya eneo hilo hayaharibiwi.

Hata hivyo, Mchechu anasema kuwa changamoto iliyopo ni kwamba, wageni kutoka nje ya nchi bado hawafahamu sana kuhusu msitu huu na kuongeza kuwa, wanaendelea na juhudi za kutangaza ili kuongeza shughuli za utalii na kuwa sehemu ya kuchangia pato la taifa. 0685 666964 au bjhiluka@yahoo.com

foto
Mwandishi: Bishop Hiluka

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi