loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Askari shujaa alivyojitosa kuzima moto mkubwa Tipper

ASKARI aliyefunga valvu ya mafuta katika tangi la mafuta lililolipuka Kigamboni mkoani Dar es Salaam juzi, Wilson Mwageni (40) amesema kabla ya kuchukua hatua ya kuingia kwenye moto, alimuomba Mkuu wa Kikosi cha Zimamoto, Temeke, Elia Kakwembe, amuagie familia yake.

Mwageni ambaye jana Kamishna Mkuu wa Jeshi la Zimamoto nchini, Thobias Andengenye alimpandisha cheo kutoka Sajini na kuwa Stesheni Sajini (Staff Sergeant), alisimulia namna alivyoamua kwa uzalendo mkubwa, kujitoa kufa kwa ajili ya Tanzania.

Moto huo katika matangi ya mafuta, yanayomilikiwa na kampuni ya Lake Oil, ulilipuka juzi saa 3:00 usiku katika maeneo ya Kigamboni na kusababisha taharuki kubwa kwa wakazi wa eneo hilo na Jiji la Dar es Salaam. Jeshi la Zimamoto kwa kushirikiana na vikosi vingine vya zimamoto Bandari na binafsi, walifanikiwa kuuzima saa 5:00 usiku, baada ya Mwageni kujitosa kuingia ndani na kufunga valvu iliyokuwa ikivujisha mafuta yaliyochochea zaidi moto.

“Haikuwa rahisi lakini nilijiuliza nisipofanya mimi nani atafanya? Ukiwa askari wakati wote ni kufa au kupona kwa ajili ya wengine, viapo vyetu vinasema hivyo.

“Kabla sijaingia kufunga valvu iliyokuwa inavujisha mafuta, niliongea na Afande wa Mkoa (Kakwembe) kama nikifa, awaambie watoto na mke wangu kwamba nawapenda ila nchi ilinihitaji pia,” alieleza Mwageni mwenye watoto wawili na mke mmoja, Agatha, anayetarajia kujifungua wakati wote kuanzia sasa.

Alisema aliingia ndani kuzima moto na askari watatu, yeye na wenzake wawili; mmoja wa Bandari na mwingine wa kampuni binafsi, lakini joto lilikuwa kali na wenzake walishindwa kuhimili na kukimbilia nje lakini yeye aliendelea kufunga valvu hadi kufanikiwa na kutoka.

Anasema alipata majeraha na kupoteza fahamu baada ya kutoka, lakini anamshukuru Mungu alifanikiwa. Aliyempandisha cheo jana katika Ofisi za Jeshi la Zimamoto, Temeke, kwa niaba ya Kamishna Mkuu Andengenye ni Naibu Kamishna, Fikiri Salla, ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Ukaguzi wa Kinga na Uchunguzi Majanga ya Moto katika jeshi hilo.

Akizungumza baada ya kupandishwa cheo, Mwageni alimshukuru Mkuu wa Jeshi hilo, viongozi wake na askari wenzake kwa kutambua mchango wake na kuahidi kuendelea kufanya kazi kwa uzalendo mkubwa.

“Niliajiriwa kufanya kazi, sikuajiriwa ili kupata zawadi wala vyeo. Hivyo napenda sana kauli mbiu ya Rais Dk John Magufuli ya ‘Hapa Kazi Tu’, nami niseme kwamba nitaendelea kufanya kazi, ‘Hapa Kazi Tu,” alisema Mwageni huku akishangiliwa na askari wenzake waliomnyanyua juu kwa furaha.

Akizungumza na waandishi baada ya kumpandisha cheo Mwageni, Naibu Kamishna Salla alisema moto ulianza katika eneo la kusukuma mafuta katika matangi ya kuhifadhi mafuta na kwamba chanzo hakijafahamika bado.

Alisema Kamishna Mkuu, Andengenye ameunda kamati ya uchunguzi wa tukio hilo (salla ni Mwenyekiti) na wakikamilisha, wataueleza umma nini sababu ya moto huo. Awali, Mkuu wa Utawala na Fedha wa Jeshi hilo, Mbaraka Semwanza aliliambia gazeti hili kuwa moto ulianza saa 3:00 usiku juzi.

Alisema kwa juhudi kubwa za Zimamoto na vikosi vingine, pamoja na ujasiri wa Mwageni aliyekubali kujitoa kufa kwa ajili ya Watanzania kufunga valvu, walifanikiwa kuuzima moto huo juzi saa 5:00 usiku.

“Kutokana na kitendo hicho alichokifanya Wilson (Mwageni) cha kizalendo Kamishna Mkuu amempandisha cheo kuanzia leo (jana) kutoka Sajini na kuwa Staff Sajini,” alisema Semwanza.

Alisema pamoja na kwamba hakuna aliyejeruhiwa, lakini nchi ingepata hasara pamoja na nchi jirani zaidi ya sita, ambazo husafirisha mafuta kupitia Tanzania.

foto
Mwandishi: Gloria Tesha

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi