loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

SUKAMAHELA: Kituo cha Hija kitakachochochea utalii Tanzania

TANGU aingie madaraka mwaka 2015, Rais John Magufuli amekuwa akiitambulisha Tanzania kama nchi yenye utajiri mwingi inayostahili kutoa misaada kwa mataifa mengine, badala ya kuwa ombaomba.

Amekuwa akinukuliwa na vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi akisisitiza kuwa Tanzania ina aina nyingi za madini yakiwemo madini ya tanzanite yanayopatikana Tanzania pekee.

Kwamba, eneo kubwa la Tanzania ni ardhi yenye rutuba inayofaa kwa mazao mbalimbali; mito maziwa na ukanda wa bahari na vivutio mbalimbali vya utalii visivyopatikana sehemu nyingine yoyote duniani. Tanzania ni ya pili duniani kwa kuwa na vivutio vya utalii. Inao pia utajiri wa hali ya hewa ya kuvutia; rasilimali watu ya kutosha, mifugo mingi ikishika nafasi ya pili kwa Afrika.

Tanzania, ni nchi yenye amani na usalama na kijiografia ipo kimkakati kama lango la kuingia nchi sita ambazo hazina bahari. Uwepo wa rasilimali zote hizi, unatoa fursa nyingi za uwekezaji.

Aidha, mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi; ukuaji wa uchumi endelevu, ujenzi wa viwanda; kurekebisha sheria na mikataba ili nchi inufaike na rasilimali zake; ujenzi wa mazingira mazuri ya biashara, utekelezaji wa diplomasia ya uchumi na utekelezaji wa miradi mikubwa kwa kutumia fedha za ndani, vimeipa nchi heshima kubwa na kujenga taswira nzuri kimataifa.

Katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Tano, chini ya uongozi wa Rais Magufuli, kumekuwa na uanzishwaji wa mbuga na hifadhi za wanyama sita za Nyerere, Burigi-Chato, Ibanda-Keyra, Rumanyika- Karagwe, Moyowosi na Ugala River.

Mara kadhaa wakati wa kupokea ndege zinazonunuliwa na serikali, Rais Magufuli amekuwa akisema serikali imejipanga vyema kuhakikisha kuwa nchi yetu inakuwa na ndege za uhakika.

Hizi ni ndege zitakazosaidia kuwaleta wageni moja kwa moja nchini kutembelea vivutio mbalimbali ambavyo nchi yetu imebarikiwa kuwa navyo, badala ya hali ilivyokuwa awali kutegemea mashirika ya ndege kutoka nchi nyingine. Kwa mujibu wa Waziri wa Maliasili na utalii Dk Hamis Kigwangala, usafiri wa anga ni kichocheo kikubwa cha ukuaji wa utalii nchini.

Anasema, mwaka 2018 takribani asilimia 62 ya watalii wote waliotembelea nchini kwa kutumia usafiri wa anga huku asilimia 37 wakitumia barabara na asilimia 0.1 walitumia reli na maji.

Aidha, katika kipindi hiki, Rais amekuwa akiwauteua mabalozi na kusisitiza kuwa kazi iliyo mbele yao ni kuiwakilisha vyema Tanzania na kutangaza fursa na vivutio mbalimbali vilivyopo ili kuliingizia taifa mapato, kwa maneno mengine ni kuwa Tanzania imekijikita katika diplomasia ya uchumi. Ni ukweli usiopingika kuwa, Tanzania sasa ni eneo linaloaminika zaidi kuwekeza kutokana na mazingira yaliyowekwa katika sekta nyingi. Takwimu zinaonesha kuwa, hata idadi ya watalii imekuwa ikipanda ikilinganishwa na miaka ya nyuma.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Profesa Adolf Mkenda, idadi ya watalii wanaoingia nchini imeongezeka hadi kufikia milioni 1.5 mwaka 2018 kutoka milioni 1.3 mwaka 2017 sawa na ongezeko la asilimia 13.5. Mkenda anasema, ongezeko hilo ni mara mbili ya ongezeko la utalii duniani Utalii huu uliongezeka kwa asilimia 6.1 kutoka watalii bilioni 1.3 mwaka 2017, hadi watalii 1.4 bilioni mwaka 2018.

Wakati tunaanza mwaka 2020 Tanzania imeingia katika historia mpya kwa kuzindua kivutio kingine kikubwa cha utalii wa kiroho katika Mkoa wa Singida. Kivutio hicho ni Kituo cha kikubwa cha Hija cha Bikira Maria kilichozinduliwa Januari Mosi, 2020 katika eneo la Sukamahela kutokana na ubunifu wa wazo kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk Rehema Nchimbi.

Dk Nchimbi anasema uzinduzi wa kituo hicho kikubwa cha kihistoria cha Hija na Maombezi cha Bikira Maria, kilijengwa eneo la Sukamahela ambalo ndiyo eneo linalodaiwa kuwa katikati ya nchi ya Tanzania kijiografia. Kipo wilayani Manyoni katika Mkoa wa Singida na kimsingi, licha ya huduma hasa za kiimani kwa waumini wa Kanisa Katoliki, kitabadilisha uchumi na kuchochea maendeleo ya Tanzania.

Dk Nchimbi anaamini uzinduzi wa kituo hicho unaifanya nchi yetu kuongeza idadi ya vivutio vya utalii wa imani nchini hivyo, kuvutia wageni kutoka sehemu mbalimbali duniani wanaokuja kutembelea maeneo mbalimbali ya mbuga na hifadhi za wanyama na bahari kujumuisha eneo hilo. Kwa mujibu wa mkuu wa mkoa huyo, eneo hili ni eneo la kihistoria na kimkakati kwa kuwa ndiyo eneo la katikati ya Tanzania ambalo pia lipo karibu kabisa na makao makuu ya nchi (Dodoma).

Kimsingi, kama eneo hilo litatangazwa, vizuri ni fursa kubwa hata kwa wageni mbalimbali wanaofika makao makuu kutembelea na kufanya hija. Anatoa rai kwa wananchi kufanya uwekezaji katika eneo hilo kwenye sekta za utoaji wa huduma ili kunufaika na wageni wanafika kuhiji kutoka sehemu mbalimbali duniani na kuunga mkono jitihada za Rais John Magufuli za kuwaletea maendeleo Watanzania.

“Uzinduzi wa Kituo cha Hija cha Bikira Maria siyo tu kwamba utaimarisha watu wetu (Wakristo -Wakatoliki) kiroho na kubadilisha kabisa uchumi wa watu wetu, bali utasaidia pia nchi yetu kukuza amani ambayo ni mhimili mkuu wa maendeleo ya taifa lolote duniani,” aliongeza Dk Nchimbi.

Anasisitiza kuwa, kiimani, uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka 2015 ulivyojaa misukosuko, hofu na mashaka, wasiwasi na hata wengine walitamani kuikimbia Tanzania, huku akikiri kwamba kilichotuvusha salama siyo kingine, bali ni hasa imani thabiti na sahihi za watu ikiwamo imani kwa Mama Bikira Maria (kwa Wakatoliki).

“Ndiyo maana mama huyu (Bikira Maria) hatimaye leo hii amesimama katikati ya nchi hii hapa Sukamahela ili kuendelea kutuvusha. Tusichoke kumkimbilia, tusichoke kumuomba amani ya taifa letu kupitia sala na maombezi yake,” anasema Dk Nchimbi.

Kanisa Katoliki nchini, limetoa pongezi na shukrani mahususi kwa Mkuu wa Mkoa wa Singida Dk Rehema Nchimbi kwa kuwa na maono ya kiroho ya kubuni wazo la kuwa na kituo hicho na kuliwasilisha kwa Kanisa Katoliki hatimaye kujengwa na kuzinduliwa kituo hicho katikati ya Tanzania. Akizungumza katika ibada maalumu iliyofanyika eneo la Sukamahela, Januari Mosi, mwaka huu, Askofu wa Jimbo Katoliki la Singida, Mhashamu Edward Mapunda kwa niaba ya Kanisa Katoliki nchini, alishukuru na kupongeza wazo la Mkuu wa Mkoa wa Singida Dk. Rehema Nchimbi.

Akahimiza Watanzania kutumia mwaka huu kwa sala na maombi wakati Taifa likielekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani, huku akiwasihi Wakristo nchini kote kumtumia Mama Bikira Maria ili aweke uchaguzi huo kwenye Moyo Mtakatifu kwa sababu yeye ni Malkia wa Amani.

Aidha, Askofu Mapunda kupitia Mkuu wa Mkoa, alimshukuru Rais John Magufuli kwa mchango wake katika kufanikisha ujenzi wa kituo hicho cha hija, alioutoa hivi karibuni akiwa safarini wakati alipopita mkoani hapa kuelekea Chato mkoani Geita kwa mapumziko.

Desemba 9, kila mwaka ndiyo imepangwa kuwa siku rasmi kukusanyika kitaifa. Kituo hiki kilichojengwa kwa ustadi mkubwa kinakuwa cha pili ndani ya mkoa wa Singida, kikitanguliwa na kile cha kwanza kilichopo eneo la Kimbwi nje kidogo ya mji, ambacho pia kwa lengo lile lile, hutoa fursa ya watu kukutana na Mungu kwa njia ya Bikira Maria. Kwa mujibu ya vitabu vitakatifu vya Kikristo, Bikra Maria alikuwa mwanamke Myahudi aliyeishi kati ya karne ya 1 KK na karne ya 1 BK.

Mke wa Yosefu, alimzaa Yesu Kristo. Kwa sababu hiyo na kwa utakatifu wake, anapewa heshima ya pekee katika madhehebu mengi ya Kikristo, lakini pia anafahamika katika Uislamu duniani kote. Mashehe wanasema katika Kurani Mariamu (Maria) ndiye mwanamke pekee aliyetajwa kwa jina katika kitabu hicho.

foto
Mwandishi: John Mapepele

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi