loader
Dstv Habarileo Mobile
Picha

Mwanafunzi fukara aliyefanya maajabu kidato cha 4

CHANGAMOTO ya mazingira na ufukara wa familia, haukumzuia kijana Yohana Lameck Lugedenga kufaulu vizuri kidato cha nne kutoka Shule ya Sekondari ya Kata ya Igaganulwa mkoani Simiyu.

Kijana huyo amepata daraja la kwanza, akiwa na ufaulu wa alama A kwenye masomo yote saba, aliyofanya yakiwemo ya Sayansi. Akizungumza na Habari- Leo jana kuhusu ufaulu huo, uliowafurahisha walimu wa shule hiyo pamoja na uongozi wa Mkoa wa Simiyu, Mkuu wa Shule hiyo, Emelius Emmanuel alisema walitarajia matokeo mazuri kwa Yohana, ingawa sio kwa kiwango hicho.

“Kwa kweli tuliona uwezo wake tangu akiwa kidato cha kwanza, tulitegemea angepata daraja la kwanza ila sio kwa alama zote hizo, lakini ametushangaza na sisi tumefurahi kupita maelezo, hasa ukizingatia ufukara wa familia yake”,alisema Mwalimu Emmanuel.

Alisema Shule ya Sekondari Igaganulwa ni ya Kata na kwenye matokeo ya kidato cha nne yaliyotoka juzi, wanafunzi waliofanya mtihani walikuwa 88, na waliofaulu ni 75 ambao wamepata kuanzia daraja la kwanza hadi la nne na wengine 13 wamefeli.

Shule hiyo ya Sekondari Igaganulwa, ipo umbali wa takribani kilometa 45 kutoka Bariadi mjini. Akizungumzia ufaulu wa Yohana, ambaye ndiye mwanafunzi pekee aliyepata daraja la kwanza tena kwa alama A za masomo yote saba, Mwalimu Emmanuel alisema siri ya ufaulu huo ni juhudi binafsi na makambi ya masomo, yanayofanywa mkoani humo.

“Yohana ni mtoto mtaratibu, alistahili ufaulu huo, ametoka mazingira magumu mno, anaishi na mama pekee, baba yao aliondoka nyumbani mwaka 2013 akidai anakwenda kutafuta maisha mkoani Morogoro, ila hadi leo hajarejea na hana mawasiliano na familia yake”,alisema Mwalimu Emmanuel.

Akisimulia aliyopitia Yohana, Mwalimu Emmanuel alisema baada ya kufaulu elimu ya msingi na kujiunga na Sekondari ya Igaganulwa, mtoto huyo alichelewa kuripoti shuleni hapo.

Walimu hawakujua tatizo lake hadi pale walimu wa shule ya msingi aliyosoma, walipowaambia kuwa anakabiliwa na matatizo ya kifamilia. Mwalimu Emmanuel alisema walimu hao wa msingi, ndio waliwaambia walimu wa Sekondari Igaganulwa kuwa hata sare za shule, walikuwa wakimnunulia na vifaa vingine. Waliomba asaidiwe sekondari, kwa kuwa ana uwezo kimasomo.

“Aliripoti shuleni kwa kuchelewa, kwa sababu mama yake alikuwa hana uwezo hata wa kumnunulia sare, tulimsaidia sare za shule, akaanza masomo na uwezo wake ukaanza kuonekana. Tuliona sio busara kumuacha, tukamsaidia. Na mimi ni mwalimu wa Hesabu, alikuwa kinara, na anajua kudadisi na ana nidhamu ya hali ya juu’’,alisema Mwalimu Emmanuel.

Mwalimu huyo aliongeza kuwa walipofanya mtihani wa kidato cha pili, aliibuka na matokeo mazuri. Pia mtihani wa majaribio wa kidato cha nne alifanya vizuri; na hiyo ikamfanya aende kambi mkoani, ambapo walimu walimsaidia gharama; na mama yake mzazi, alipeleka debe moja la mahindi.

“Huwa mkoa umeweka utaratibu wa kuinua kiwango cha elimu kwa kuanzisha makambi ya masomo na huyo kijana alichaguliwa kwenda kambi ya masomo mkoani ambako utaratibu wazazi huchangia gharama ndogo. Lakini, kwa Yohana mama yake alishindwa, ila akaleta debe la mahindi na sisi tukachanga na kupata fedha za kujikimu akaenda kuungana na wenzake ili wanolewe zaidi’’,alisema Mwalimu Emmanuel.

Akizungumzia matokeo hayo, Mwalimu Emmanuel alisema waliposikia ufaulu huo walishangilia, sio kwa sababu Yohana amepata daraja la kwanza pekee, bali kwa sababu amepata masomo yote saba alama A.

“Asubuhi ya leo (jana) Yohana alikuja shuleni hapa, kutoa shukrani kwa walimu kwa kumsaidia na kumtia moyo kusoma kwa bidii, na mwalimu wake wa somo la Kiswahili alikuwa na wasiwasi kwa sababu masomo mengine alikuwa akifaulu kwa alama A lakini Kiswahili akawa anapata B, alimsihi sana kukazania pia somo hilo na kweli leo matokeo yamedhihirisha kwani kapata alama A zote”,alisema.

Kwa mujibu wa Mwalimu Emmanuel, Yohana ndiye mtoto wa kwanza kwenye familia yao kusoma. Kwamba ana mdogo wake wa kike, ambaye ufukara wa familia na mazingira, vimechangia yeye kutokuwa na mwelekeo mzuri.

“Unajua nilienda nyumbani kwao, yaani mazingira yale sio ya kawaida, ni fukara na ninasikia pia hapo sio kwao, bali wamepewa wajihifadhi. Wakati mwingine hata mlo mmoja ni tatizo, ndio maana alipoingia kidato cha nne tulimchukua Yohana akaishi shuleni ili atulie asome” alisema. Yohana azungumza, apania kuwa daktari Akizungumzia furaha ya matokeo yake, Yohana alisema amefurahi sana kupata matokeo hayo.

Kwamba mama yake aliposikia habari hiyo njema, alimshukuru na kumwambia asante. “Kwa kweli nimefurahi kupata matokeo haya, mama aliposikia nimefaulu alinishukuru, alisema asante mwanangu, na mimi naahidi kufanya vizuri nikichaguliwa kidato cha tano, nataka kuendelea na masomo yangu ya Sayansi, ili baadaye nije kuwa daktari, niikomboe familia yangu”,alisema Yohana.

Alisema familia yake ina watoto wanne, mmoja ni marehemu na kwamba yeye pekee ndiye aliyebahatika kufika kidato cha nne, kwani mdogo wake aliishia kidato cha pili na hiyo ilichangiwa na mazingira magumu waliyonayo. Yohana aliiomba serikali impangie shule yenye mazingira mazuri na kumsaidia mahitaji, kwa sababu ufukara wa familia yake, unaweza kuwa kikwazo katika masomo yake, hivyo akipata shule nzuri yenye mazingira bora, atatulia na kusoma.

“Nawashukuru walimu na mama walinisaidia kunishauri na kuniongoza hadi nikafika na kupata matokeo haya. Naiomba serikali isiniache, inisaidie, kama kuna uwezekano nipate shule nzuri na mazingira mazuri nitulie nifanye vizuri zaidi”,aliomba Yohana.

DC azungumzia siri ya ufaulu Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya wa Bariadi, Festo Kiswaga aliliambia gazeti hili kuwa wamefurahishwa na matokeo ya kijana huyo na wengine mkoani humo, kwa sababu yanaendelea kuakisi matokeo ya mikakati, iliyowekwa na mkoa huo ya kuinua kiwango cha elimu na ufaulu.

Kiswaga alisema Mkuu wa Mkoa huo, Anthony Mtaka kwa kushirikiana na timu mzima ya mkoa, waliweka mkakati wa kuwa na makambi ya masomo, ili kuwasaidia wanafunzi kufanya vizuri zaidi na matokeo yake yameanza kuonekana.

“Mkoa una utaratibu wa kuwapeleka kambini wanafunzi, mfano tunakuwa na makambi aina tatu, moja ni kwa wanafunzi wenye uwezo wa juu wanakutanishwa pamoja na kupewa walimu wa kuwapiga msasa zaidi, pia tuna kambi ya wale wenye uweo wa kati nao tunawapa walimu bora zaidi wanawapiga msasa, hivyo hivyo kwa wale waliofanya vibaya nao tunawapa walimu na wanasaidiwa na wengi wamepiga hatua”,alisema Kiswaga.

Alisema matokeo ya makambi hayo ni kwamba ufaulu, umeongezeka mkoani Simiyu, ambapo mwa mwaja jana matokeo ya sekondari ufaulu uliongezeka kutoka nafasi ya 26 kwa mwaka uliopita hadi kuwa nafasi ya tisa kitaifa. Kadhalika kwa matokeo ya elimu ya msingi, ufaulu uliongezeka kutoka nafasi ya 22 mwaka 2018 hadi kufika nafasi ya nane mwaka jana kitaifa.

WAKALA wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) umeanza rasmi ...

foto
Mwandishi: Ikunda Erick

4 Comments

 • avatar
  Marius alphonce
  12/01/2020

  AWALI YA YOTE NAPENDA KUMSHUKURU MUNGU KWAN NINA HAKIKA KUWA MUNGU AMEWEKA KITU CHA ZIADA KWA KIJANA YOHANA LAMECK KWA AJILI YA KUIKOMBOA FAMILIA YAKE. PILI NINGEPENDA KUMPONGEZA KIJANA HUYO KWAKUWA AMEFAULU KWA DARAJA LA JUU SANA, NINGEPENDA KUISHAUR SELIKALI NA WADAU WA ELIMU KUWA WAPO VIJANA KAMA HAWA WENGI SANA JAPO WENGINE WANASHINDWA KUFANYA VIZUR KUTOKANA NA UGUM WA MAISHA YA FAMILIA ZAO HIVYO INGEKUWA NI VZURI KUWA ZIWEPO TAARIFA ZA WATU KAMA HAWA ILI IWE NIRAHISI KUWASAIDIA WAWEZE KUFIKIA NDOTO ZAO. NA MWISHO WA YOTE HONGERA KWA DR JOHN POMBE MAGUFULI KWA KAZI NZURI ANAYOIFANYA, ELIMU BURE IMEANZA KUONYESHA MATUNDA YAKE MUNGU AENDELEE KUMUONGOZA ILI AFANYE MAKUBWA ZAIDI MUNGU IBARIKI TANZANIA MUNGU IBARIK AFRIKA

 • avatar
  Dawia Matata
  12/01/2020

  Nimefurahishwa sana na nampongeza sana kijana Yohana kwa matokeo mazuri mno na changamoto ngumu anazopitia.Sambamba na hili Yohana asingekuwa kitu bila juhudi za hali ya juu za walimu wote waliogusa maisha yake , Watanzania inabidi tufike mahali tubadilike na kumdhani mwalimu kwani mabadiliko ya mtoto yoyote yule huanzia darasani ili kufikia ndoto zake , wote tunahusika moja kwa moja kufanikisha elimu ya mtoto lakini sehemu pekee inayowakutanisha watoto na kuwaweka katika usawa ni darasani .Walimu wa Tanzania tuna changamoto zisizopimika kwa maumivu lakini binafsi tufanye kazi hii ili tulipwe na Mungu tu , tuguswe na maisha ya watanzania wa kesho tusiwahukumu kwa kutokuwapenda na kuwaonesha njia isiyosahihi , tufanye kwa uwezo wetu wote na kuwasaidia kina Yohana kwani wapo wengi sana sana . Nimependa pia wazo lenu la makambi liimarisheni kwa kusimamia vyema nidhamu zao naimani mwaka huu simiyu itakuwa tatu bora kitaifa kila kitu kinawezekana wapendwa... Well done teachers and parents for support each other but also other stakeholders... Keep it up.

 • avatar
  Protas joseph
  14/01/2020

  Nimebaki nalia tu..nothing to say..hakika imenitoa machozi

 • avatar
  Michael jumanne
  14/01/2020

  Tatizo sijasikia serial ya mkoa itamsaidiaje Hugo kijana

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi