loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Magufuli: Msifiche fedha nje ya nchi

RAIS John Magufuli amewataka Watanzania kutoficha fedha zao nje ya nchi; na badala yake wazitumie kuwekeza kwenye miradi mikubwa yenye tija kwa jamii za Tanzania na kukuza uchumi hapa nchini.

Sambamba na hilo, Rais Magufuli pia alisema serikali inawaunga mkono wafanyabiashara wazalendo wenye nia ya kuwekeza miradi mbalimbali ya maendeleo, itakayokuza pato la taifa.

Rais Magufuli alitoa mwito huo jana wakati wa uzinduzi wa Hoteli ya kisasa yenye hadhi ya nyota tano, Hotel Verde iliyopo eneo la Mtoni, nje ya mji wa Unguja inayomilikiwa na mfanyabiashara maarufu nchini, Saidi Salim Bakhresa.

Alimsifia mfanyabiashara huyo kwa uwekezaji huo wa hoteli, ulioiingizia Sh bilioni nne serikali ya Zanzibar kwa miaka miwili iliyoanza kufanya kazi kisiwani humo. Alisema mfanyabiashara Bakhressa ni wa kupigiwa mfano kwani ameamua kutumia fedha zake kwa ajili ya kuwanufaisha wananchi wazalendo kwa kuwekeza.

Rais Magufuli alisema kuwa wapo watanzania waliowekeza nje ya nchi na kushindwa kuwekeza hapa nchini mahali, ambapo kama wakiwekeza faida itazinufaisha vizazi vyao vijavyo, huku akibainisha kuwa na taarifa za watanzania waliohifadhi fedha nje ya nchi.

Aliwataka kuiga mfano wa Bakhresa mfanyabiashara ambaye ameweka kupaumbele zaidi katika uwekezaji wa ndani ya nchi, huku akijikita zaidi katika biashara za usafirishaji, kilimo, habari na kuwekeza kwenye hoteli hiyo, ambayo inasaidia kukuza utalii.

“Watanzania wekezeni nyumbani acheni kuficha fedha nje ya nchi na kuwekeza zaidi huko, huyu Bakhresa mbali na kuwekeza Malawi, Kenya, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na kwingineko lakini Tanzania ndio amefanya mambo makubwa zaidi,” alisema.

Alikemea tabia ya baadhi ya watendaji serikalini, kuwakatisha tamaa wafanyabiashara wazalendo walioonesha moyo wa kuwekeza. “Nawataka watendaji wetu kuacha tabia ya kuwakatisha tamaa wafanyabiashara wazalendo... wekezeni nchini na muache tabia ya kuficha fedha nje ya nchi ukifa zitaliwa na watu wengine,” alisema.

Aliwataka wafanyabiashara wengine kuiga mfano wa Bahressa wa kuwekeza kwanza nchini na baadaye kuwekeza nchi jirani. Mapema, Magufuli alitoa wito kwa taasisi zinazofanya kazi ya kutangaza utalii Zanzibar na Tanzania Bara, kushirikiana ili kuitangaza sekta hiyo.

Kwa mfano alisema Tanzania Bara kwa mwaka imepokea watalii milioni 1.5 wakati Zanzibar imepokea watalii 520,809 katika mwaka 2018. Hata hivyo, alisema idadi ya watalii wanaotembelea katika nchi mbili za Misri na Morocco wanafikia milioni 10 kwa mwaka.

“Tunahitaji kushirikiana zaidi kutangaza utalii, kipo kisiwa kidogo cha Maldive kinapokea watalii milioni 1.5 kwa mwaka,” alisema.

Awali kabla ya kutoa hotuba yake, Ofisa Mtendaji Mkuu wa hoteli hiyo ya Verde, Salim Aziz Salim alibainisha kuwa hoteli hiyo imeajiri wafanyakazi 250 huku 15 kati yao wakiwa ni walemavu na wengine ni watu wanaosambaza bidhaa mbalimbali hotelini hapo.

Alisema gharama za ujenzi wa hoteli hiyo ni Sh bilioni 65 za Tanzania na ina vyumba 106 mabwawa ya kuogelea na kumbi kadhaa za mikutano zenye uwezo wa kuchukua watu 10 hadi 500 pamoja na maeneo mbalimbali yanayovutia watalii. Salim alisema kuna michezo mbalimbali ya kwenye maji inayoweza kutumiwa na watu 1,000 kwa pamoja huku pia kukiwa na eneo la kuegesha boti 48 zenye urefu wa mita 100. Hoteli hiyo ina mfumo wa kubadilisha maji machafu na kuyasafisha kisha kuyatumia kwa shughuli za umwagiliaji wa bustani au vyooni.

Alisema hotel Verde ina mfumo mzuri wa matumizi ya umeme, ambapo imewekeza kwenye umeme wa jua unaotumia nguvu kidogo ya nishati huku alimhakikishia Rais Magufuli kuwa licha ya hoteli hiyo kuwa karibu na bahari, hakuna uchafu unaoingia baharini kutokea hotelini hapo.

Akiwa kwenye eneo la bustani ya hoteli hiyo, Rais Magufuli pia aliendesha harambee ya kuchangia kundi la vijana wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kisiwani humo ambapo alitoa Sh milioni tatu, Bakhresa alichangia milioni tano, Makamu wa Rais alichangia Sh milioni moja huku viongozi wengine wa CCM, wafanyabiashara na viongozi wa serikali wakichangia pia. Katika harambee hiyo Sh milioni 50 zilipatikana huku taslima zikiwa Sh milioni 12 na ahadi Sh milioni 38.

MGOMBEA urais wa ...

foto
Mwandishi: Waandishi Wetu

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi

Magufuli: Nataka kumalizia kazi

masaa 14 yaliyopita Magnus Mahenge, Dodoma

MGOMBEA urais wa ...

Wanawake waihakikishia CCM ushindi

masaa 14 yaliyopita Magnus Mahenge, Dodoma

 

Waziri aagiza mifumo ya fedha ipunguze rushwa

masaa 16 yaliyopita Mwandishi Maalumu, Simiyu

WAZIRI ...