loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

WILSON MWAGENI Askari aliyejitosa kufa kwa ajili ya Tanzania kuzima moto Kigamboni

UKIMUONA ana kwa ana, kwa umbo lake la kawaida, huwezi kuamini kama anaweza kuhusika katika matukio makubwa yaliyoweka historia nchini, likiwamo la kujitosa kufunga valvu iliyokuwa ikivujisha mafuta na kusaidia kuzima moto katika matangi ya mafuta yaliolipuka Kigamboni wiki iliyopita.

Moto huo katika matangi ya mafuta yanayomilikiwa na kampuni ya Lake Oil, ulilipuka Januri 8, mwaka huu saa tatu usiku katika maeneo ya Vijibweni, Kigamboni na kusababisha taharuki kubwa kwa wakazi wa eneo hilo na Jiji zima la Dar es Salaam. Pamoja na vikosi vya zimamoto na uokoaji kufanikiwa kuzima moto saa tano usiku, saa mbili baada ya moto kuwaka, kazi kubwa ilifanywa na Mwageni aliyejitosa kuingia ndani na kufunga valvu iliyokuwa ikivujisha mafuta katika eneo la kusukuma mafuta.

Nimekuwa mmoja wa waandishi wa habari waliopata nafasi ya kuzungumza na askari huyo wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kupata habari kuhusu alichokifanya kama kinaishia kuwa ni ujasiri aliyoupata katika mafunzo ya kijeshi au kuna msukumo wa ziada. Lengo awali lilikuwa ni kuzungumza naye namna alivyojitosa kufunga valvu iliyokuwa ikivujisha mafuta katika mlipuko wa moto wa matangi hayo ya mafuta lakini nikagundua ana mengi ya kijasiri aliyoyafanya, jamii inapaswa kuyajua na kuiga uzalendo wa askari huyu.

Akisimulia hatua hiyo aliyoichukua, Wilson Mwageni, kijana wa miaka 40, anasema kabla ya kuingia kufunga valvu, alimuomba Mkuu wa Kikosi cha Zimamoto, Temeke, Elia Kakwembe, amuagie familia yake.

Mwageni ambaye siku moja baada ya tukio la moto Kamishna Mkuu wa Jeshi la Zimamoto nchini, Thobias Andengenye alimpandisha cheo kutoka Sajini na kuwa Stesheni Sajini (Staff Sergeant), anasema aliamua kwa uzalendo tu kujitoa kufa kwa ajili ya Tanzania. “Haikuwa rahisi lakini nilijiuliza nisipofanya mimi nani atafanya? Ukiwa askari wakati wote ni kufa au kupona kwa ajili ya wengine, viapo vyetu vinasema hivyo. Majukumu ya kazi zetu ni kulinda maisha na mali za watu.

“Kabla sijaingia kufunga valvu iliyokuwa inavujisha mafuta, nilizungumza na Afande wa Mkoa (Kakwembe) nikamwambia kama nikifa, awaambie watoto na mke wangu kwamba nawapenda ila nchi ilinihitaji pia,” anaeleza.

Mwageni ana watoto watatu, Alison (13), Elison (10) na Edson (3) na mke mmoja aliyemtambulisha kwa jina la Agatha Shitundo, ambaye ni mjamzito anayetarajia kumleta mgeni katika familia hiyo wakati wowote kuanzia sasa.

Anasema alipowaga viongozi waliokuwapo eneo la tukio akiwamo pia Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Sarah Msafiri na Katibu Tawala wa Wilaya, Rahel Mhando, Sarah alimtania kwamba mtoto atayezaliwa kama akifa watamuita jina Lake Oil.

“Tukacheka pale kisha nikajitosa ndani kufunga valvu,” anaeleza Mwageni aliyejiunga na Jeshi la Zimamoto mwaka 2006 akitokea kampuni binafsi ya ulinzi ya Night Support.

Aliwahi kufanyakazi pia Security Group na katika kampuni hizo anawashukuru sana walimu wake kama Richard Becca (raia wa Uingereza), Laurence Kabigi, Hamis Mtengo na mzee Kunambi kwa kuchangia mafanikio yake. Anasema waliingia ndani kuzima moto askari watatu, yeye na wenzake wawili; mmoja wa Bandari na mwingine wa kampuni binafsi, lakini joto lilikuwa kali na wenzake walishindwa kuhimili na kukimbilia nje lakini yeye aliendelea kufunga valvu.

“Joto lilikuwa kali sana ndani, lakini mafunzo ya kijeshi na Mungu ndivyo vilitusaidia, baada ya muda wenzangu waliona wanaishiwa nguvu wakatoka nje, moyoni mwangu nikasema Mungu nisaidie Watanzania wananitegemea mimi tu hapa, nikaendelea kufunga valvu mpaka nilipomaliza.

“Wakati nilipomaliza nilikuwa najisikia kama kufa hivi, nikajitahidi kutoka nje lakini baadaye sikujitambua, kumbe nilizimia lakini namshukuru Mungu nipo salama na madhara pamoja na kwamba yametokea, ila si makubwa kama valvu ingeendelea kuvujisha mafuta, moto ungekuwa mkubwa na madhara yangekuwa makubwa zaidi,” anaeleza shujaa huyo.

Mwageni anasema ameshiriki katika matukio mengi ya uokoaji yaliotikisa jamii ya Watanzania. Bila shaka mpendwa msomaji unakumbuka tukio la kijana aliyekutwa na kichwa cha mtoto Salome akikifyonza damu maeneo ya Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) maarufu kwa jina la Rama ‘mla watu’ na kufunguliwa kesi namba 26 ya mwaka 2010. Stesheni Sajini Mwageni anasema tukio hilo alilifuatilia kuanzia nyumbani kwa akina Rama, Segerea kwa Bibi na baada ya kupata taarifa ameonekana Muhimbili, walikwenda na kushughulikia tukio hilo.

Anasema wakati wanaelekea Muhimbili, walishuhudia ajali ya Land Cruser na Hiace Magomeni na watu wawili walipoteza maisha papo hapo. “Waliopoteza maisha, ubongo ulitapaa barabarani. Ni mimi niliyeenda kuukusanya na kuhifadhi miili vizuri. Watu wali-kuwa wakisema yule kijana ni jasiri sana, walikuwa wakinishangaa lakini mimi nilikuwa kazini,” anaeleza Mwageni mwenye Shahada ya Sheria.

Anasema aliwahi kuingia katika karo la choo eneo la Ilala, Bungoni, Dar es Salaam likiwa na kinyesi kuopoa mwili wa fundi aliyetumbukia katika shimo hilo baada ya kuteleza na ukuta ukamfunika.

“Nilipaswa kumtoa, ndio kazi yetu kuokoa na kuopoa pia. Wenzangu walinishikia kamba ili likitokea la kutokea wanivute,”anasema kijana huyu shujaa.

Mwageni anasema alishawahi kudondokewa na ukuta katika matukio ya uokoaji na pia aliwahi kuzingirwa na moto wakati hoteli ya Sea Cliff ilipoungua lakini akatoka salama kutokana na mafunzo wanayopewa na viongozi wao na kwa msaada wa Mungu.

Nilivutiwa na namna Mwageni alivyotambua uweza wa Mungu katika kazi zake, nilipomuuliza kama ndio kitu cha ziada cha mafanikio yake alisema; “mimi ni RC (Roman Catholic), Mungu kwangu ni namba moja halafu ujuzi na taaluma inafuata. Maombi ni silaha kubwa sana ya mafanikio.”

Uzalendo wake anakiri unasukumwa na utendaji kazi wa Rais John Magufuli, anayemtaja kama mtu anayemfuatilia sana, anasema anatumia kauli mbiu ya Hapa Kazi Tu, kutekeleza majukumu yake ya kila siku.

“Kazini kuna mambo mengi, mwingine anaweza kuona unapanda akakushusha makusudi, lakini mimi niliajiriwa kufanya kazi, sikuajiriwa ili kupata zawadi wala vyeo. Hivyo napenda sana kauli mbiu ya Rais John Magufuli ya Hapa Kazi Tu, vijana tufanye kazi tuache kukaa kutwa nzima vijiweni,” anasema.

Anawahamasisha askari wenzake wapende kujituma, anamshukuru Kamishna Mkuu Andengenye, Mkuu wa Utawala na Fedha wa Jeshi hilo, Mbaraka Semwanza na viongozi wengine wote wa jeshi hilo kwa namna walivyomsaidia kufanyakazi kwa juhudi za uzalendo kwani wakati wote walimwongoza kwa vitendo na kumsaidia kufika alipofika.

Semwanza akizungumza na gazeti hili alisema Mwageni ameonesha ujasiri mkubwa kukubali kujitoa kufa kwa ajili ya Watanzania jambo lililosaidia kazi ya kuzima moto kwa muda mfupi na kupunguza madhara.

‘Kutokana na kitendo hicho alichokifanya Wilson (Mwageni) cha kizalendo Kamishna Mkuu amempandisha cheo kuanzia leo tarehe 9/1/2020 kutoka Sajini na kuwa Staff Sajini,” alisema Semwanza.

Aliongeza kuwa pamoja na kwamba hakuna aliyejeruhiwa sana, lakini nchi ingepata hasara kubwa na kutikisika kiuchumi pamoja na nchi jirani zaidi ya sita, zinazosafirisha mafuta kupitia Tanzania. Dada wa Mwageni, Happiness Mwageni, mwandishi wa Global TV, aliyekuwepo wakati kaka yake akipandishwa cheo, alimpongeza kwa hatua hiyo na kueleza kuwa amefurahi kuona juhudi za kaka yake zimethaminiwa na hatua hiyo inamuongezea naye juhudi katika kazi kama mwandishi wa habari.

Aliyempandisha cheo katika Ofisi za Jeshi la Zimamoto, Temeke, kwa niaba ya Kamishna Mkuu wa Jeshi hilo, Andengenye ni Naibu Kamishna, Fikiri Salla, ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Ukaguzi wa Kinga na Uchunguzi Majanga ya Moto katika jeshi hilo.

Baada ya kumpandisha cheo, Naibu Kamishna Salla aliwaambia waandishi wa habari kuwa chanzo cha moto huo hakijafahamika bado lakini Kamishna Mkuu, Andengenye ameunda kamati ya uchunguzi wa tukio hilo na yeye (Salla) ni Mwenyekiti na wakikamilisha, wataueleza umma nini sababu ya moto huo.

Salla aliwataka askari kuiga mfano wa Mwageni kwa kuweka uzalendo mbele lakini kwa tahadhari ya usalama ili wazidi kutumia ujuzi na nguvu zao kulitumikia Taifa na Watanzania.

foto
Mwandishi: Gloria Tesha

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi