loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Sultan Qaboos wa Oman afariki dunia

MTAWALA wa muda mrefu katika nchi za Kiarabu, Sultan Qaboos bin Said Al Said (pichani) wa Oman, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 79. Baraza la Familia ya Kifalme limethibitisha kifo hicho na kueleza kuwa Sultan alifariki dunia juzi, Ijumaa jioni.

“Kwa masikitiko Sultan wa Oman amefariki. Sultan wetu Qaboos bin Said Al Said, Mwenyezi Mungu alimwita kwake Ijumaa jioni,” ilieleza taarifa ya familia jana asubuhi.

Hata hivyo, sababu za kifo chake bado hazijaelezwa bayana, lakini mwezi uliopita Sultan Qaboos ambaye hakuwa na mrithi ama mtu aliyekuwa ameteuliwa kuchukua nafasi yake, alikuwa nchini Ubelgiji kwa wiki nzima akipata matibabu na kulikuwa na taarifa kwamba anaugua saratani.

Baraza la Familia ya Kifalme limemteua na kumuapisha binamu wa Sultan Qaboos, Haitham bin Tariq Al Said (65) aliyewahi kuwa Waziri wa Utamaduni wa Oman, kurithi nafasi hiyo. Sultan ndio mwenye mamlaka ya mwisho nchini Oman. Pia anashikilia wadhifa wa waziri mkuu, amiri jeshi mkuu, waziri wa ulinzi, waziri wa fedha na waziri wa mambo ya nje.

Kumetangazwa siku tatu za maombolezo na bendera zitapepea nusu mlingoti kwa siku 40. Shughuli za mazishi zinaendelea katika mji mkuu wa Muscat na nje Msikiti wa Sultan Qaboos, ambako mwili umepelekwa jana mchana kwa dua maalum ya maziko.

Sultan Qaboos kwa kushirikiana na Uingereza, mwaka 1970 akiwa na umri wa miaka 29, alimng’oa madarakani baba yake, Said bin Taimur, katika mapinduzi ya amani na kuiweka Oman katika mwanzo mpya wa maendeleo kwa kutumia utajiri wake wa mafuta.

Alimpindua baba yake kutokana na misimamo mikali, ikiwamo kupiga marufuku watu kusikiliza redio, kuvaa miwani ya jua na kuamua nani atakayeoa, kupata elimu au kufukuzwa nchini humo. Kwa kipindi cha miaka 50, Sultan Qaboos ametawala siasa za Oman, nchi yenye idadi ya watu milioni 4.6 huku takriban asilimia 43 wakiwa ni kutoka nchi nyingine.

NAHODHA wa timu ya Taifa ya Tanzania rasmi ametolewa kwa mkopo ...

foto
Mwandishi: MUSCAT, Oman

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi