loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

U17 wanawake yajiweka pazuri kombe la Dunia

TIMU ya Taifa ya soka ya wanawake chini ya umri wa miaka 17, imeifunga timu ya Burundi kwa mabao 5-1 katika mchezo wa kufuzu Kombe la Dunia 2020 nchini India uliochezwa Uwanja wa Taifa Dar es Salaam jana.

Katika mchezo huo wa hatua za awali kufuzu Kombe la Dunia Tanzania ilianza kupata bao dakika ya tisa likifungwa na Aisha Masaka na lingine alifunga dakika ya 12,Joyce Meshack alifunga bao la tatu dakika ya 35 na Protasia Mbunda akafunga bao la nne na kuifanya kwenda mapumziko wakiwa mbele kwa mabao 4-0.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku Tanzania ikizidisha mashambulizi na dakika ya 59 Aisha Masaka akafunga bao la tano ambalo lilikuwa la tatu kwake kwa mchezo huo lakini ikiwa ni ya ‘hat trick’ ya sita kwake tangu aanze kucheza mpira.

Dakika ya 72 Burundi walipata bao la kufuta machozi lililofungwa na Lydia Karenzo kutokana na mabeki kuzembea kuondoa mpira eneo la hatari na kumpiga tobo kipa wa Tanzania na kuingia wavuni.

Baada ya mchezo kumalizika makocha wa timu zote walizungumzia mchezo huo ambapo Kocha wa Tanzania, Bakari Shime aliwashukuru wachezaji kwa kufanya kile alichowatuma na kuwapongeza Watanzania kwa kuwaunga mkono.

“Nimefurahi kupata ushindi leo ila kazi ndio imeanza kwani tunakwenda kuruadiana Januari 25 Bujumbura na lolote linaweza kutokea hatuwezi kusema tumewatoa,” alisema Shime.

Naye kocha wa Burundi Daniella Niyibimenya alilalamikia uwanja pamoja na joto lakini alikiri timu yake kufanya makosa kadhaa ambayo yalisababisha kufungwa.

“Uwanja haukuwa rafiki kwetu kwani tumezoea nyasi bandia, pia joto lilikuwa kali lakini tulifanya makosa ambayo yalitugharimu na nitakwenda kuyafanyia kazi ili mchezo ujao tushinde,” alisema Daniella.

Daniella ni kama vile hakutarajia kipigo hicho ukizingatia mara ya mwisho walipocheza na Tanzania katika mashindano ya Cecafa yaliyofanyika nchini Uganda walitoka sare ya mabao 3-3.

BAADA ya Namungo FC ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi