loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mtoto aliyefanya maajabu kidato cha 4 apata ufadhili masomo

MWANAFUNZI Yohana Lugedenga aliyefanya vizuri katika mitihani ya kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya Kata ya Igaganulwa mkoani Simiyu, amepatiwa fursa ya kusoma kidato cha tano na sita katika shule ya Sekondari ya Bondeni iliyopo Arusha.

Kijana huyo pamoja na kutoka kwenye familia yenye maisha ya umasikini, amepata daraja la kwanza, akiwa na ufaulu wa alama A kwenye masomo yote saba, aliyofanya yakiwemo ya Sayansi.

Fursa hiyo kwa mwanafunzi huyo ilitolewa jana na Taasisi ya Zaim Education Development Limited, inayomiliki Shule hiyo ya Sekondari ya Bondeni.

Akizungumza na gazeti hili, Mkuu wa Shule hiyo, Abbas Rahim alisema shule hiyo huwa inatoa bure ya malazi, elimu na chakula, ila mzazi hulamizika kununua sare za shule, madaftari na kugharamia mitihani.

“Hatutaki kumnyang’anya mzazi mtoto hivyo na yeye atalazimika kununua sare za shule kwa maana ya viatu, godoro, daftari, kalamu na kugharamia mitihani ili na yeye ajione ni sehemu ya mafanikio ya mtoto wake,” alisema.

Pia alisema katika shule yake, wana masomo ya sayansi kwa mchepuo wa Fizikia, Kemia na Hisabati (PCM), Fizikia, Kemia na Baiolojia(PCB) na Kemia, Baiolojia na Jiografia(CBG), hivyo ni chaguo la mwanafunzi kulingana na ufaulu wake.

Naye, Abdul Mohamed ambaye ni Mfanyakazi wa Taasisi ya Zaim Education Development Limited, alisema taasisi yao inasimamia shule za sekondari za Bondeni (Arusha), Kinondoni Muslim(Dar es Salaam) na Jamhuri ya Dodoma.

Alisema wanasaidia watoto wanaohitimu darasa la saba na kidato cha nne. Habari za ufaulu wa Yohana, ziliandikwa na gazeti hili toleo la Jumamosi, baada ya matokeo ya kidato cha nne kutoka.

Habari hiyo imeibua mjadala mkubwa katika mitandao ya kijamii. Wengine wanapongeza gazeti hili, kwa kumulika shule za kata na wengine wanaomba serikali ichukue jukumu la kumsaidia mwanafunzi huyo.

Yohana anaishi na mama yake pamoja na wadogo zake watatu, akiwa mtoto wa kwanza katika familia hiyo, ambayo baba yake aliondoka tangu mwaka 2013, kwa madai anakwenda kutafuta riziki Morogoro.

Lakini, hadi leo baba huyo hajarudi na familia yake haina mawasiliano naye.

Yohana alipata ufaulu huo kupitia Shule ya Sekondari ya Kata ya Igaganulwa iliyopo mkoani Simiyu. Katika shule hiyo wanafunzi 75 wamefaulu kwa kupata daraja la kwanza hadi la nne. Wengine 13 wamefeli.

MGOMBEA urais wa ...

foto
Mwandishi: Rachel Palangyo

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi

Magufuli: Nataka kumalizia kazi

masaa 13 yaliyopita Magnus Mahenge, Dodoma

MGOMBEA urais wa ...

Wanawake waihakikishia CCM ushindi

masaa 13 yaliyopita Magnus Mahenge, Dodoma

 

Waziri aagiza mifumo ya fedha ipunguze rushwa

masaa 16 yaliyopita Mwandishi Maalumu, Simiyu

WAZIRI ...