loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Dk Nchimbi na mkakati imara wa korosho kufufua uchumi Singida

Hivi karibuni Rais John Magufuli alifanya ziara kisiwani Zanzibar na kuzindua hoteli ya kimataifa ya nyota tano ya Verde Zanzibar-Azam Luxury Resort and Spa.

Pamoja na mambo mengine, Rais alielekeza na kusisitiza kuwa, juhudi za pamoja baina ya Tanzania Bara (Tanganyika) na visiwani (Zanzibar) zinahitajika katika kutangaza utalii wa nchi ili kuinua uchumi kwa kuwa ni miongoni mwa sekta inayoongoza kwa kuliiingizia taifa mapato yakiwamo ya fedha za kigeni.

Kwa mujibu wa Rais Magufuli, kwa sasa watalii wanaotembelea Tanzania Bara ni wachache ukilinganisha na ukubwa wa nchi. Mwaka 2018 Tanzania Bara ilitembelewa na wageni milioni 1.5 huku Zanzibar ikitembelewa na wageni 520,809.

Alisema ni muhimu kukumbuka kuwa, kisiwa kama Maldives chenye takribani kilometa za mraba 298, kinapata wageni milioni 1.5 kwa mwaka. Akawataka watendaji wa serikali kufanya kazi kwa mkakati na kufikia au kuzizidi nchi za Afrika kama Moroco na Misri zinazopata takribani watalii milioni 10 kwa mwaka.

Kwa mujibu wa ripoti ya Benki Kuu, nchini Tanzania sekta ya utalii ndiyo inayoongoza kwa kwa kuliingizia taifa mapato. Kwa mwaka unaoishia Novemba 2019, sekta hiyo ililiingizia taifa takriban Dola za Marekani bilioni 2.5.

Kauli ya mkuu wa nchi imeanza kutekelezwa kwa vitendo na baadhi ya watendaji wa serikali yake huku kukiwa na mafanikio makubwa katika kipindi hiki kifupi cha utawala wake katika mikoa ambayo awali ilikuwa inaonekana kama masikini na yenye kudharaulika.

Januari Mosi mwaka huu katika Mkoa wa Singida, kumezinduliwa Kituo Kikuu cha Hija katika eneo la Sulamahela eneo ambalo ni katikati ya Tanzania. Kituo hicho cha hija kitakuwa miongoni mwa vituo vikubwa duniani.

Kinatarajiwa kuwavuta wageni wengi kuja nchini na hivyo, kubadili uchumi wa wananchi wa Tanzania kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk Rehema Nchimbi. Dk Nchimbi anasema, katika kuunga mkono kazi kubwa inayofanywa na Rais Magufuli, Mkoa wa Singida upo kwenye mapinduzi makubwa ya kijani ya kilimo cha pamoja (block farming) cha zao la korosho.

Hadi sasa, mkoa umeweza kuwaunganisha wananchi kulima ekari 12000 kwa pamoja katika Wilaya ya Manyoni na kwamba, mikorosho hiyo imeshaanza kuzaa na kuvunwa.

Amesema programu hiyo inalenga kufanya kilimo hicho kuwa ni miongoni mwa utalii wa kilimo kwa kuwa hadi sasa watu wengi kutoka sehemu mbalimbali duniani, wanavutika kuja kujifunza namna kilimo hicho kinavyoleta mabadiliko makubwa ya fikra na kijamii kwa wananchi wa Mkoa wa Singida na Tanzania kwa jumla.

Hivi karibuni, kundi la wanachuo na wakufunzi kutoka Chuo cha Ulinzi cha Taifa walitembelea mradi wa kilimo cha pamoja cha korosho Masigati wilayani Manyoni.

Wakiwa huko, walijifunza mambo mbalimbali na kusifu juhudi zinazofanywa na mkoa katika kuwaletea mageuzi ya kiuchumi wananchi. Kiongozi wa Msafara wa Chuo cha Ulinzi cha Taifa, Balozi Peter Kallaghe alipongeza juhudi na mapinduzi makubwa yanayofanywa na Mkuu wa Mkoa wa Singida.

Katika ziara hiyo Kallaghe anasema mageuzi haya yanapaswa kuigwa na mikoa yote nchini ili kuunga mkono jitihada za kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda ifikapo 2025.

Dk Nchimbi anasema Mkoa wa Singida unaendelea kufanya mageuzi makubwa ya kiuchumi na kijamii kupitia mkakati wa kuwainua wananchi wote kwa kubuni kilimo cha pamoja ili kila mwananchi apate ekari kuanzia tano.

“Katika kipindi hiki cha takribani miaka miwili, tunamshukuru Mungu kuwa tumeleta mabadiliko makubwa ya kitabia na kifikra kwa wananchi wetu kupitia mradi huu ambao wengi wao wameendelea kujiunga siku hadi siku,” alisitiza Dk Nchimbi.

Anasema licha ya kupata ekari 1200 katika Wilaya ya Manyoni, pia wamepata ekari 500 katika eneo la Itigi na ekari 500 katika eneo la Ikungi. Zote zinaendelezwa kwa mtindo wa kilimo cha pamoja.

Dk Nchimbi anaongeza kuwa, mpango wa baadaye katika mradi huo ni kuongeza eneo kubwa la kulima korosho na kuanzisha ushirika wa pamoja wa wakulima wa korosho wa eneo hilo.

Aidha, wametenga maeneo makubwa kwa ajili ya kujenga viwanda na maghala kwa ajili ya kuchakata na kuhifadhia korosho. “Ni mpango wetu kwamba, katika eneo hili tuweze kuboresha miundombinu ya kisasa na kuweka viwanda vikubwa hapahapa ambapo minada yote itafanyika hapa,” anasisitiza Mkuu wa Mkoa.

Anasema baada ya kukamilika kwa miundombinu na kuimarika kwa kilimo hicho katika eneo hilo, litakuwa eneo utalii mkubwa wa kilio nchini utakaoliingizia taifa mapato.

Aidha, anatoa rai kwa wananchi kote nchini, kwenda kulima katika eneo hilo huku akionya kuwa serikali itamtoa mtu yeyote ambaye hatalitumia eneo hilo kwa lengo lililokusudiwa.

“Tunaelewa wapo watu wanadhani kuwa, kwa kuwa tunaligawa eneo hili, basi wanakuja ili kupata hati ya eneo hili, naomba kuwatangazia kuwa wasijidanganye kwa kuwa hati inayotolewa hapa ni maalum kwa ajili ya kulima zao la korosho na siyo vinginevyo hivyo tupo makini sana katika hilo,” anasema.

Kwa mujibu wa Dk Nchimbi, kutokana na tafiti zilizofanywa na Taasisi ya Kilimo ya Naliandele, eneo hilo ni bora ukilinganisha na maeneo mengi hapa nchini na kwamba, korosho za eneo hilo zinawahi zaidi kukua na pia zinazaa mara mbili kwa mwaka.

Hali hii inatokana na eneo hilo kuwa na misimu miwili ya kiangazi hivyo, kutoa maua mara mbili kwa mwaka mmoja. Aidha anasema, kutokana na eneo hili kuwa na umuhimu wa pekee katika kilimo cha korosho, tayari taasisi mbalimbali za kilimo za serikali zimeanzisha ofisi za kudumu ili kuwasaidia wananchi katika ukulima wa zao hili.

Anazitaja baadhi ya taasisi hizo kuwa ni pamoja taasisi ya utafiti wa kilimo Naliandele na Bodi ya Korosho nchini.

Nchimbi anampongeza na kumshukuru Rais Magufuli kwa kutoa pikipiki nne kwa ajili ya kusaidia kazi hiyo na kwamba, aliahidi jumla ya pikipiki kumi. “Kipekee kabisa nachukua nafasi hii kumpongeza Rais wetu; kwa kweli yupo pamoja na sisi katika mpango huu; ametutia nguvu sana, tunamwombea kwa Mwenyezi Mungu aishi miaka mingi,” anasema Dk Nchimbi.

Anasema mapindunzi ya kijani ya kilimo cha korosho yameifanya Singida, sasa kuwa tofauti na Singida ya zamani ambapo ilisadikiwa kuwa ni Singida ya njaa, Singida masikini, Singida kame na Singida isiyokuwa na fursa hali iliyowafanya hata baadhi ya watumishi wa umma kukwepa kuhamia katika mkoa huo.

Anasema baada ya kufanikiwa katika mradi huu, mkoa unatarajia kuanzisha mradi mwingine kama huo kwa mazao ya kudumu baada ya kufanya tafiti za kutosha ili kuinua uchumi wa wananchi wa kawaida wa mkoa huo.

Mkuu wa mkoa huyo anasema, mkakati wa mkoa huo ni kuufanya kuwa mkoa wenye uchumi mkubwa kwa kuwa mbali ya kuwa na rutuba na hali ya hewa nzuri, pia una utajiri wa rasilimali za kutosha ikiwa ni pamoja na vivutio mbalimbali vya kihistoria kama vijiji vya Kilimatinde.

Kijiji hicho kina historia ya kuwa kituo cha njia kuu ya watumwa katika miaka ya 1885 na ngome ya utawala wa Mjerumani na Mwingireza. Kadhalika, yapo mabwawa makubwa ya samaki na Kituo Kikubwa cha Hija kilichopo Sukamahela.

MIAKA michache iliyopita kulikuwa ...

foto
Mwandishi: Na John Mapepele

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi