loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mambo ya kuzingatia diplomasia ya uchumi ilete mafanikio

Japokuwa diplomasia ya uchumi siyo dhana ngeni katika masuala ya kimataifa, kwa miaka ya hivi karibuni ndipo imepata umaarufu mkubwa na kuifanya itambulike na kukubalika duniani kote.

Kwa sasa, siasa haiongozi uchumi, bali uchumi ndiyo unaongoza siasa. Kwa mfano, uhusiano wa miaka ya hivi karibuni kati ya China na Marekani, umedhihirisha jinsi matakwa ya kibiashara (kiuchumi) yalivyo na ushawishi mkubwa katika siasa licha ya kuwa na tofauti kubwa za kiitikadi kati ya mataifa hayo.

Aidha, China imekuwa ikitumia dhana ya “Haijalishi paka ni mweupe au mweusi, ili mradi anashika panya” kupanua uhusiano na nchi nyingi bila kujali itikadi zao ili kujinufaisha kiuchumi. Kwa maana hiyo, mahitaji ya kiuchumi ndiyo yamekuwa kipaumbele cha kwanza katika juhudi za nchi kutimiza malengo ya sera ya kigeni.

Nchi zilizoshindwa kutambua umuhimu wa diplomasia ya uchumi, zimeshindwa na zimebaki nyuma katika kutimiza malengo yake ya sera za kigeni.

Kwa kutambua hilo, nchi nyingi duniani zilibadilisha mwelekeo wao kutoka diplomasia ya kizamani/jadi iliyolenga zaidi kutekeleza masuala ya kisiasa kama ukombozi, kulinda uhuru, mamlaka na amani ya nchi; na kuelekea kwenye utekelezaji wa diplomasia ya uchumi inayosisitiza kuendeleza maslahi ya kiuchumi.

Ni kwa kiasi gani nchi hizo zimetilia mkazo na zimenufaika na diplomasia ya uchumi, ni suala litakalojadiliwa kwenye makala zinazokuja. Katika toleo lililopita, tulichapisha makala kuhusu utekelezaji wa diplomasia ya uchumo Serikali ya Awamu ya Tano.

Tuliona kwamba diplomasia ya uchumi ni mkakati wa nchi kushirikisha mataifa ya kigeni kujinufaisha kiuchumi. Nchi inanufaika kiuchumi kwa kushirikiana na mataifa ya nje kupitia biashara, uwekezaji, misaada na mikopo, utalii, mazungumzo na kupokea teknolojia ya kisasa.

Swali la msingi ni hili: Ni mambo gani ya kuzingatia ili nchi inufaike na diplomasia ya uchumi? Hili ni swali la msingi linalohitajia majibu. Makala hii ambayo ni matokeo ya tafiti zilizofanywa kutoka nchi mbalimbali zilizonufaika na utekelezaji wa diplomasia ya uchumi, itajibu swali hilo.

Kwa maana hiyo, kama Tanzania inataka kunufaika na diplomasia ya uchumi ni vema ikazingatia masuala hayo.

KUWA NA MIPANGO MIZURI YA KIUCHUMI NDANI YA NCHI

Ni vema tukafahamu mapema kwamba, diplomasia ya uchumi haiwezi kutatua matatizo au changamoto za ndani ya nchi. Kwa kuwa diplomasia ya uchumi ni mwendelezo (advancement) wa utekelezaji wa maslahi ya kiuchumi ya nchi kwenye nchi za kigeni, mipango mizuri ya kiuchumi ndani ya nchi husika ndiyo msingi wa diplomasia yenye mafanikio.

Ni kweli kama alivyosema mmoja wa wanadiplomasia maarufu kwamba, “Japokuwa kwenye uwanja wa kimataifa, kuna vita vya kila nchi kutaka kuendeleza maslahi yake, ni nyumbani kwa kila nchi ndipo vita halisi ya maendeleo inapopiganwa na ushindi unapopatikana.”

Kwa mantiki hiyo, ni wajibu wa kila nchi inayotaka kunufaika na diplomasia ya uchumi kuhakikisha kwamba, inakuwa na mipango mizuri ya kukuza uchumi na yenye lengo la kuwanufaisha wananchi wake.

Mipango ambayo ndiyo nchi inashirikisha mataifa ya kigeni kuitekeleza. Kama huna mipango mizuri unashirikisha mataifa ya kigeni kufanya nini na kwa manufaa ya nani? Wanazuoni wengi wa kimataifa wanaamini kwamba, “nchi ambayo haina mipango mizuri ya kiuchumi ya ndani imepanga kushindwa mapema kwenye uwanja wa kimataifa”.

Faida linganifu Nchi zilizofanikiwa kwenye diplomasia ya uchumi ni zile zilizotambua na kujikita kwenye uzalishaji wa bidhaa na huduma kwenye sekta/ maeneo ambayo zina faida linganifu.

Aidha, baada ya uzalishaji, nchi inahakikisha inaziongezea thamani bidhaa zake ili inufaike na biashara ya kimataifa. Hii inafanyika kwa kuanzisha viwanda vya kuongeza thamani bidhaa na huduma ambazo nchi ina faida linganifu badala ya kuziuza zikiwa ghafi.

Nchi nyingi zimeshindwa kunufaika na biashara ya kimataifa kwa sababu zimekuwa zikiuza bidhaa nyingi ghafi ambazo zina thamani ndogo. Kwa mfano, kilo moja ya kahawa ghafi inauzwa kati ya Dola za Marekani 2.5 na 5, wakati kilo moja ya kahawa iliyoongezewa thamani inauzwa Dola za Marekani 10 na 15 (angalia pia bei ya korosho).

Aidha, utashangaa kusikia kwamba nchi za India na Kenya zimekuwa zikiuza madini ya tanzanite yenye thamani kubwa zaidi ya Tanzania nchi pekee inayozalisha madini hayo duniani.

 

Moja ya sababu ni kutokuwa na viwanda vya kuongeza thamani madini hayo. Ni kwa msingi huo mpango wa ujenzi wa viwanda vya kuongezea thamani bidhaa haukwepeki! Faida za kiushindani Japokuwa nchi inaweza kuwa na faida linganifu za uzalishaji kwenye maeneo mengi, ni vema nchi ikachagua maeneo machache ambayo ina uwezekano mkubwa wa kufanya vizuri zaidi.

Pamoja na umuhimu wa faida linganifu, kichocheo kikubwa cha kukuza biashara, uwekezaji na utalii, ni uwepo wa faida za kiushindani. Faida za kiushindani za nchi zinajumuisha kitu chochote kinachoipa au kinachoifanya nchi kuwa na faida au ubora zaidi kuliko washindani wengine.

Kwa mfano, nchi ya Moroko ilifanikiwa kukuza uchumi wake kwa zaidi ya mara 2.5 kwa kuchagua sekta nne tu zenye faida za kiushindani, ambazo ni: utalii, kilimo, vifaa vya magari na viwanda vya nguo.

Shirika la Uchumi Duniani (World Economic Forum - WEF) ambalo huchapisha ripoti ya ushindani ya kila nchi duniani kila mwaka, linataja misingi 12 inayochochea ushindani katika kila nchi. Misingi hiyo ni: utendaji wa taasisi; miundombinu; teknolojia ya mawasiliano na habari (ICT); uimara wa uchumi mkubwa; afya; ujuzi; ufanisi wa soko la bidhaa; ufanisi wa soko la ajira; mfumo wa fedha; ukubwa wa soko; mwenendo wa biashara; na uwezo wa ubunifu.

Kwa mfano, katika ripoti ya mwaka 2019, Tanzania ilikuwa nchi ya 117 duniani kwa ushindani. Aidha, kwenye Jumuia ya Afrika Mashariki Tanzania ilikuwa ya nne, nyuma ya Kenya (95), Rwanda (100) na Uganda (115).

Burundi ilikuwa ya mwisho (135). Maana yake ni kwamba, bidhaa zinazozalishwa Tanzania hazina ushindani kwenye soko la dunia. Kwa hiyo, hatuwezi kunafaika sana na biashara ya kimataifa.

Kama tunataka kunufaika na biashara ya kimataif,a lazima tuifanyie kazi hiyo hiyo 12. Nchi ya Singapore ndiyo inaongoza kwa kuwa na ushindani mkubwa duniani.

Kama Singapore imeweza kwa nini sisi tushindwe? Jambo la kutia moyo ni kwamba, kwa miaka ya hivi karibuni, Tanzania imefanikiwa kuboresha mazingira ya kiushindani. Kwa mfano, mwaka 2016 Tanzania ilikuwa nchi ya 120 kwa ushindani duniani na mwaka 2019 ikafanya vizuri kidogo ikawa ya 117.

foto
Mwandishi: Prof. Kitojo Wetengere

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi