loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Daraja la Kigongo - Busisi kupaisha uchumi

MTANDAO wa miundombinu umekuwa ukifananishwa na mishipa ya damu katika mwili wa binadamu. Kama ambavyo mishipa ina kazi ya kupeleka damu katika kila kiungo cha mwili, miundombinu ina umuhimu mkubwa kuwezesha maeneo mbalimbali kufunguka kiuchumi.

Kwa hiyo kuna uhusiano mkubwa wa maendeleo ya eneo fulani la dunia na kuimarika kwa miundombinu yakle ambayo ndio huiwezesha sekta ua uchukuzi kuimarika pia.

Kwa mfano, wakulima wanategemea sana kuimarika kwa sekta ya uchukuzi kufikishiwa pembejeo katika maeneo yao ya kilimo halikadhalika kusafirisha mazao wanayozalisha hadi kwenye masoko.

Halikadhalika, wafanyabiashara na wenye viwanda hutegemea kuimarika kwa sekta ya uchukuzi kusafirisha bidhaa zao kwenda kwa walaji. Wakati akisoma hotuba ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2019/20 Juni 13 mwaka jana, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alisema pato la taifa lilikua kwa kiwango cha asilimia 7.0 mwaka 2018 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 6.8 mwaka 2017.

Kisha akasema: “Ukuaji huu ulichochewa zaidi na kuongezeka kwa uwekezaji hususani katika miundombinu kama vile ujenzi wa barabara, reli, uboreshaji wa bandari na viwanja vya ndege.”

Vingine vilivyochangia ukuaji huo alivitaja kuwa ni kutengemaa kwa upatikanaji wa nishati ya umeme na kuimarika kwa huduma za usafirishaji. Kisha akasema kwamba sekta ya uchukuzi na uhifadhi mizigo ilikuwa miongoni mwa zilizokua kwa kasi ikiwa na asilimia 11. 8 nyuma ya sekta za sanaa na burudani (asilimia 13.7) na sekta ya ujenzi (asilimia 12.9).

Katika kuimarisha sekta ya uchukuzi nchini, Serikali ya awamu ya tano chini ya uongozi wa Rais John Magufuli, hivi karibuni aliweka jiwe la msingi katika daraja la Kigongo- Busisi lenye urefu wa kilomita 2.3 ambalo ujenzi wake unatarajia kugharimu shilingi bilioni 699.2.

Daraja linatajwa kwamba ndilo refu kuliko yote Afrika Mashariki na ni la sita kwa urefu katika bara la Afrika. Akiweka jiwe hilo la msingi katika eneo la Kigongo wilayani Misungwi, Rais Magufuli alisema ujenzi wa daraja hilo unaofanywa kwa fedha za ndani ni kielelezo kingine kwamba Tanzania ina uwezo wa kutekeleza miradi yake yenyewe kwa kutumia fedha zake za ndani bila kutegemea wafadhili kutoka nje.

Aligusia kwamba manufaa ya kiuchumi ya utekelezaji wa mradi huo makubwa hayatanufaisha Watanzania pekee hususuani wakazi wa mikoa ya kanda ya ziwa bali pia nchi jirani za Rwanda, Uganda, Kongo- DRC na Burundi.

Alisema kukamilika kwa mradi huo utakaotoa jumla ya ajira 1600 kwa wakazi wa maeneo ya jirani utapunguza sana changamoto ya usafirishaji waliyokuwa wanaipata wananchi hasa wakati ambapo vivuko vinavyosafirisha wananchi kwenye maeneo hayo vinapopata changamoto.

Rais alisema kutokana na changamoto alizopitia hasa baada ya kuhudumu katika sekta ya ujenzi kwa takribani miaka 17, anasema mradi huo utakuwa mkombozi kwa wakazi wa mikoa ya Kanda ya Ziwa na nchi za maziwa makuu.

Alimtaka Mkandarasi anayejenga daraja hilo, Kampuni ya China Civil Engineering Group Limited kutoka China kwa kushirikiana na Railway 15 kuhakikisha kuwa anafanya kazi usiku na mchana ili ujenzi wa daraja hilo la kihistoria linakamilika kabla ya muda uliopangwa.

Licha ya kuwashukuru watendaji wa Wizara ya Ujenzi kwa kutangaza zabuni ya ujenzi wa mradi huo mapema, Rais Magufuli alimshukuru pia Spika wa Bunge, Job Ndugai na wabunge kwa ujumla kwa kupitisha mapema fedha za ujenzi wa mradi huo.

WANANCHI KULIPWA FIDIA

Tayari serikali imetoa fidia ya kiasi cha Sh bilioni 3.145 ambacho kimepokelewa hivi karibuni na Wakala wa Barabara Mkoa wa Mwanza ili kuwalipa fidia wananchi watakaolazimika kupisha ujenzi wa daraja hilo linalounganisha wilaya za Misungwi na Sengerema –mkoani Mwanza. Kaimu Meneja wa Tanroad Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Pius anasema kutolewa kwa fidia hiyo kwa wakati ni utekeezaji wa ahadi ya Rais John Magufuli aliyoitoa Desemba 7 mwaka jana wakati wa ziara yake ya kikazi.

Anasema Rais Magufuli aliahidi Serikali kutoa fedha kwa ajili ya kuwalipa wananchi wanaostahili kulipwa fidia hiyo kwa mujibu wa sheria. Anasema jumla ya kaya 165 ndizo zinaotarajiwa kulipwa fidia na kwamba kaya 132 ni za eneo la Kigongo wilayani Misunwgi na kaya 33 ni za Busisi, Sengerema.

Anafafanua kuwa wenye makaburi 75 katika eneo la Kigongo na makaburi matatu yaliyoko Busisi watafidiwa kupitia kiasi hicho cha fedha kilichotolewa na Serikali.

“Tunamshukuru sana Rais kwa kutoa fedha hizi kwa wakati ambazo naamini zitarahisisha shughuli za ujenzi huu,” anasema na kuongeza kuwa wananchi wote wanaostahili kulipwa fidia zao watalipwa kwa mujibu wa sheria.

Mwandishi wa makala haya aliwashuhudia baadhi ya wananchi wa Busisi na Kigongo wamaoguswa na hatuia ya kupisha ujenzi wakiwa na nyuso za furaha huku baadhi yao wakimpongeza Rais Magufuli kwa jinsi alivyotoa pesa hizo kwa wakati.

Rais akizungumza na wananchi wa maeneo ya Kigongo- Busisi Desemba mwaka jana, aliwatoa hofu wale wanaoishi katika eneo la mradi kwamba watalipwa fidia zao mara moja.

“Asitokee mtu ambaye hastahili akaja kudai hapa fidia,” alisisitiza huku akiwataka wakazi wa wilaya ya Misungwi na wananchi watakaopata ajira kwenye mradi huo waonyesheuadiolifu kwa kutoiba vifaa vya ujenzi.

Akawahimiza watanzania kuendelea kulipa kodi kwani kupitia kodi miradi kama hiyo ya maendleo inawezekana na kwamba inaimariasha pia uhuru wa Watanzania na kuifanya nchi iheshimike kimataifa na duniani kwa ujumla.

KAULI ZA VIONGOZI

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Isaac Kamwele alisema daraja hilo litawaondolea adha ya usafiri waliyokuwa wanakumbana nayo wananchi wa mikoa ya Kanda ya Ziwa na nchi jirani.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara (TANROAD), Patrick Mfugale alisema baada ya daraja hilo kukamilika watu watatumia muda wa dakika nne tu kuvuka ziwa Victoria katika ya Kigongo na Busisi badala ya muda wa takribani saa mbili na nusu unaotumika sasa kwa kutegemea kuvuka kwa feri.

Spika Ndugai alisema yeye na timu yake ya Kamati ya Miundombinu ya Bunge walikuwa wanashuhudia historia nyingine ya kutukuka ikiwekwa na Rais John Magufuli.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza, Dk Anthony Diallo alimtaka Rais Magufuli kuendelea kuchapa kazi kwa kujenga miradi mikubwa bila kuangalia makunyanzi ya wale wanaoikejeli.

Mbunge wa Jimbo la Misungwi, Chalres Kitwanga alisema anaamini kwa dhati kwamba maono ya mbali aliyonayo Rais Magufuli juu ya kuwaletea wananchi maendeleo endelevu yataifikisha Tanzania mbali kimaendeleo.

“Rais sisi wananchi wa Misungwi tutaendelea kumuunga mkono Rais wetu kwa kazi kubwa anazofanya kwa utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo,” alisema Kitwanga.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongela alitumia nafasi hiyo kumshukuru Rais Magufuli kwa heshima kubwa aliyoupatia mkoa wake kwa kuridhia sherehe za miaka 58 ya uhuru na miaka 57 ya Jamhuri kufanyika mkoani Mwanza sanjari na uwekaji wa jiwe la msingi kwenye daraja hilo kubwa na la kihistoria.

MGOMBEA urais wa ...

foto
Mwandishi: Na Nashon Kennedy

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi

Magufuli: Nataka kumalizia kazi

masaa 14 yaliyopita Magnus Mahenge, Dodoma

MGOMBEA urais wa ...

Wanawake waihakikishia CCM ushindi

masaa 14 yaliyopita Magnus Mahenge, Dodoma

 

Waziri aagiza mifumo ya fedha ipunguze rushwa

masaa 16 yaliyopita Mwandishi Maalumu, Simiyu

WAZIRI ...