loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Ufaulu wa kijana Yohana wamuibua baba mafichoni

MATOKEO ya kufaulu kwa Yohana Lugedenga wa Shule ya Sekondari Igaganulwa mkoani hapa yaliyoacha gumzo nchini hasa kutokana na hali ya familia yake, yamemuibua baba yake mzazi, Lameck Lugedenga, aliyeondoka nyumbani hapo zaidi ya miaka sita kwa madai ya kwenda kutafuta maisha.

Itakumbukwa kwamba gazeti hili ndilo la kwanza kuandika habari ya Yohana wa Simiyu zilizochapishwa Januari 10 mwaka huu na kuzua gumzo kila kona ikiwemo mitandaoni. Mara baada ya habari hiyo HabariLEO ilifika mkoani hapa na kwenda nyumbani kwao walikopanga chumba kimoja cha nyumba ya udongo katika Kitongoji cha Madukani C, Kata ya Dutwa kuzungumza nao hali halisi ya maisha yao na changamoto wanazopitia.

Akizungumza na kwa njia ya simu akiwa Ifakara mkoani Morogoro, baba mzazi wa Yohana, Lameck Lugedenga alisema: “Nimefurahi sana, siwezi kuja nitapata presha, acha kwanza nitulie, Yohana kanifurahisha ingawa siko nao muda mrefu niko huku nahangaika kutafuta maisha,”alisema Lameck kwa njia ya simu.

Licha ya kutoa kauli hiyo, mkewe Masalu Lulyalya ambaye aliachiwa watoto watatu awalee na mumewe huyo aliyeondoka nyumbani hapo mwaka 2013, alizungumza na mumewe kwa simu ya mkononi kuhusu matokeo hayo na kumwambia arudi aje kumuona mwanae kafaulu lakini akamsii akisema, “siwezi kuja kwa sasa nitaanguka presha, subiri kwanza”.

Mama huyo akizungumza na HabariLEO nyumbani hapo alisema; “nami nilimsihi baba yake Yohana arudi ila amedai hawezi kuja sasa, nashangaa yeye anasema atapata presha,mimi je nimehangaika na huyu mtoto acha tu ni Mungu anajua tulikotoka,namshukuru kwa kufaulu nataka aendelee kusoma,”alisema Masalu. Mbali na ufaulu huo wa kupata daraja la kwanza kwa alama A kwenye masomo yote tisa yakiwemo ya sayansi, Yohana ametaja shule nne za serikali za vipaji maalum anazotamani kwenda kusoma kidato cha tano na sita.

Aidha pia alitaja shule moja binafsi. Shule hizo ni Ilboru Sekondari, Kibaha Sekondari, Tabora Boys Sekondari, na Mzumbe Sekondari ambazo ni za serikali vipaji maalumu huku pia akisema iwapo atajitokeza mfadhili na kumtaka akasome shule binafsi, angependa kusoma Feza Boys Sekondari. Lakini pia, Yohana sio kijana mwenye maneno mengi ni mpole na anazungumza kidogo tena mpaka umuulize tabia ambayo inalandana na mama yake ni mpole ila mwenye bidii ya kutaka mwanae asome afanikiwe na aje kuikomboa familia yake.

Akifurahia matokeo ya Yohana Mkuu wa Shule ya Msingi Igaganulwa Buzinza Taburo aliyosoma kijana huyo na kufaulu kwa alama A darasa la saba, alisema matokeo ya Yohana yanafurahisha na jamii nzima ya shule kwa sababu alikuwa mwanafunzi mwenye bidii licha ya changamoto za ufukara wa familia yake uliosababisha asaidiwe mahitaji yake na walimu.

“Matokeo ya Yohana tulianza kuyaona tangu alipokuwa shule ya msingi hapa,alikuwa mwanafunzi wetu mkimya hana maneno hadi umuulize jambo na ndiye pia aliyesaidia wenzake, kwa sababu wakati mwingine tulimwambia awafundishe wenzake na alifanya hivyo,”alisema Mwalimu Taburo.

Aliongeza Yohana ni kweli ametoka familia duni ni zaidi ya maskini kwa sababu kuna wakati alishindwa kwenda shule na tabia yake ya upole ilimfanya asiseme anayopitia hadi pale walimu walipochunguza na kugundua anakabiliwa na changamoto za uchumi kifamilia na kuamua kumsaidia akarudi shuleni hadi akahitimu.

“Kila darasa alikuwa anaongoza akiwa msingi alishika namba moja kila muhula na kila muhula alikuwa akifaulu kuliko muhula uliopita,”alisema Taburo.

Mwalimu wa Kiswahili Sekondari afunguka. Akishangilia na kumkumbatia Yohana kwa kumtoa kimasomaso kwenye somo la Kiswahili, Mwalimu wa somo hilo, Baraka Musa wa Shule ya Sekondari Igaganulwa alisema amefurahishwa zaidi na matokeo ya Yohana kwa sababu alianza kumfundisha akiwa kidato cha kwanza.

“Nilitoa jaribio darasani na nilipokuwa nasahihisha karatasi za wanafunzi nilishangaa mbona nasahihisha making scheme yangu mwenyewe? kumbe ni mtihani wa Yohana kwa sababu alipata alama 96 ya 100, ndio nikajua uwezo wake.

Aidha alimzungumzia zaidi Yohana mwalimu huyo alisema kuna wakati mwanafunzi huyo alianza kushuka ufaulu wa somo hilo hadi kupata alama 56lakini allimsihi asichague masomo bali asome yote ushauri aliozingatia na kupata matokeo hayo bora. Naye Mwenyekiti wa Kitongoji cha Madukani C, Mpemba Kengele ambaye familia hiyo iko chini ya uongozi wa kitongoji hicho alisema kufaulu kwa Yohana kumewashangaza wengi kwa sababu hawakujua kama anasoma.

“Hatukujua kama ni mwanafunzi, hata mimi sikujua kwani yeye na mama yake walikuwa wanafanya kazi ya vibarua shambani kwangu ,eka moja kupalilia nawapa Sh 25,000, niliposikia Yohana kafaulu wa Madukani C tukawa tunaulizana nia nani ndio nikaoneshwa ni huyo,” alisema Kengele. Kwa habari zaidi za Yohana endelea kusoma HabariLEO matoleo yajayo.

foto
Mwandishi: Ikunda Erick, Simiyu

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi