loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

JPM na msisitizo wa Nyerere kuhusu kodi

“KUTOKUKUSANYA kodi ni sifa mojawapo ya serikali corrupt. (serikali inayokumbatia rushwa). Serikali corrupt popote duniani haikusanyi kodi, serikali corrupt inatumwa na wenye mali, inawafanyia kazi wenye mali, serikali corrupt haiwezi kumwambia kitu chochote mtu mwenye mali... Itabaki kufukuzana na vijitu vidogo vidogo mabarabarani.”

Mwalimu pia alihimiza sana suala la uadilifu, vita dhidi ya wala rushwa na umuhimu wa viongozi kuwa na miiko katika utendaji kazi wao. Alisema hata wakati wa utawala wake kulikuwa na rushwa, lakini walikuwa wakali sana dhidi ya rushwa ambayo alisema ni adui wa haki. Tukirudi kwenye kodi, Mwalimu katika hotuba yake aliyoangalia nyufa tano zilizokuwa zinainyemelea Tanzania alisema hakuna nchi duniani inayoweza kuendelea bila kukusanya kodi.

Mwalimu alilisisitiza sana suala la kodi kwa sababu nchi haiwezi kutekeleza miradi mbalimbali yenye umuhimu mkubwa kwa maendeleo ya jamii kaama ujenzi wa mabarabara na madaraja, reli, bandari, hospitali, shule mabwawa ya kuzalisha umeme, viwanja vya ndege na kadhalika bila kodi. Tatizo la kutokukusanya kodi ipasavyo, mbali na mengine kama yale ya rushwa na ufisadi, ni mambo ambayo Rais wa awamu ya tano, John Magufuli, amekuwa akipambana nayo sana tangu siku ya kwanza alipoingia madarakani na mafanikio lukuki tunayaona.

Utawala wa Rais wa Magufuli umekuwa imara katika kukusanya kodi, kwa kuziba myanya ya wakwepa kodi na maeneo ambako kulikuwa kodi haikusanywi kama vile kwa chimbaji wadogo wa madini sasa kodi inakusanywa.

Katika historia ya Tanzania, mwaka jana Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilikusanya kiasi kikubwa cha fedha kutokana na msisitizo na msimamo wa Rais Magufuli ambaye kwa dhati anaonyesha kulipa kipaumbele suala la ukusanyaji kodi. Kama ilivyokuwa kwa mwezi Septemba 2019, TRA ilifanikiwa kuvunja rekodi nyingine kwa mwezi Desemba, 2019 kwa kukusanya kiasi cha Sh trilioni 1.987 ikiwa ni sawa na ufanisi wa asilimia 100.20 wa lengo la kukusanya Sh trilioni 1.983.

Kumbuka kabla ya Rais Magufuli kuingia madarakani kiasi kilichokuwa kinakusanywa ni wastani wa Sh bilioni 850 kwa mwezi. Serikali ya awamu ya tano imekuwa ikihimiza umuhimu wa kukusanya kodi kwa sababu ndio njia pekee ya kuiletea nchi maendeleo ambayo wananchi wanayataka. Aina za kodi ambazo serikali imekuwa ikizitumia kujipatia mapato yake ni pamoja na tozo mbali mbali zilizowekwa kisheria kama vile kodi za moja kwa moja (direct tax) na kodi zisizo za moja kwa moja (indirect tax).

Mfano wa kodi zisizo za moja kwa moja ni zile ambazo mtu hulipa kupitia katika mfumo wa biadhaa na mfano ni pale mtu anaponunua bidhaa na kulipa kodi ya ongezeko la thamani (VAT. Serikali huwa zinaweka kodi au tozo kwa raia wake na kwenye biashara kama njia ya kukuza mapato ambayo yatasaidia kutimiza sehemu ya matakwa ya bajeti ya nchi kwa mwaka.

Fedha hizi za bajeti ni kwa ajili ya kuendesha serikali, miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na kutengeneza mazingira mazuri ya kufanya biashara. Ipo miundo mbalimbali ya ulipaji kodi, mfano unapokuwa unafanya kazi unahitajika kulipa kodi kulingana na mshahara wako, kodi inayoitwa PAYE (pay as you earn). Mbali na kutekeleza miradi mbalimbali, kutokana na ukusanyaji kodi makini, serikali ya awamu ya tano, imetekeleza mambo mengi ya maendeleo kwa raia wake kama vile suala la usalama, tafiti za kisayansi na ulinzi wa mazingira.

Fedha nyingine imepelekwa kwenye malipo ya wastaafu (pensions), elimu bure na huduma za watoto. Kupitia kodi, serikali imeweza kufanya upanuzi wa viwanja vya ndege nchini lengo likiwa ni kuongezea idadi ya ndege zinazotakiwa kutua na idadi ya watalii na wageni kutoka nchi mbalimbali.

Kukamulika kwa ujenzi wa jengo la tatu la abiria la Kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere ni matokeo ya ukusanyaji mzuri kodi katika kipindi cha mwaka 2017/2018. Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli imeweza kuliimarisha ipasavyo Shirika la Ndege Tanzania, ili kuboresha huduma za usafiri wa anga ndani na nje ya nchi.

Katika mwaka 2017/2018, ndege moja aina ya Bombardier Q400 yenye uwezo wa kubeba abiria 76 na nyingine ni aina ya Dreamliner–Boeing 787–8 yenye uwezo wa kubeba abiria 262 zilinunuliwa na kutokana na kodi za Watanzania. Ndege hizi zimeweza kuongeza ufanisi katika uendeshaji wa ATCL na kuwezesha upatikanaji wa huduma za uhakika na nafuu za usafiri wa anga nchini.

Vile vile, safari za moja kwa moja za kimataifa zimepunguza gharama za usafiri na hivyo kuongeza idadi ya watalii wanaokuja nchini na kuongeza mchango wa sekta ya utalii katika ukuaji wa uchumi.

Ndege hizo zinatoa fursa za ajira kwa Watanzania kama vile wahudumu wa ndege, marubani, wabeba mizigo, waongoza ndege, wakata tiketi na mafundi, hivyo kupitia ndege, tatizo la ajira nchini linapungua kwa kuimarisha mapato binafsi ya watu na kusaidia kuendesha familia zao.

Takwimu za mwaka jana zilikuwa zinaonesha kwamba kodi ambazo zimetumika kununua ndege, zimeongeza ajira 102 kwa wasichana na marubani 60. Kufufuliwa kwa shirika la ndege la ATCL ni miongoni mwa matunda ya ukusanyaji kodi yanaofanywa na Serikali ya awamu tano.

Shirika hilo lilikuwa kwenye hali mbaya hivyo ununuaji wa ndege mpya unaleta uhai na ufufuo wa ATCL linaloleta ushindani na uboreshwaji wa huduma za ndege nchini. Wakati wa mapokezi ya ndege hizo za Dreamliner, Bombadier na Airbus, Rais Magufuli amekuwa akisisitiza kwamba ndege hizo ni mali ya Watanzania na kwamba kampuni ya ATCL imewakodisha kama koti, wakifanya vibaya wananyang’anywa na kumwazima mtu mwingine.

“Nafurahi kuzaliwa Tanzania kwa kuwa ni nchi tajiri, ununuzi wa ndege ni kodi za Watanzania maskini, ndege sio ya Magufuli ni ya Watanzania, nikifa nitaiacha hapa ikiwatumikia wananchi, inawasafirisha wagonjwa kuwahi kwenye matibabu na wanapona.

“Inawaleta watalii, pesa inaingia, nchi yetu ni ‘donor country’, (nchi mfadhili) hakuna hata senti tano iliyotoka kwa mfadhili, mfadhili ni Watanzania wenyewe, mkiangalia historia ya mashirika mengine ya ndenge “yanapasenteji” kubwa ya watu wengine ingawa yameandikwa majina ya nchi zao,” anasema Rais Magufuli.

Akisisitiza umuhimu wa kulipa kodi Rais Magufuli anasema: “Air Tanzania ni shirika linalomilikiwa na Watanzania kwa asilimia 100 na hii ni faida ya kulipa kodi, jukumu la sisi viongozi tunaongoza taifa hili ni kuhakikisha kodi inayokusanywa inatumika ipasavyo isipotee, kama ni pesa imepangwa kununua ndege ikanunue ndege.”

Akizindua barabara yenye urefu wa kilometa 360 iliyogharimu shilingi bilioni 140.025, itokayo Mpanda kwenda Katavi hadi Tabora inayotarajiwa kukamilika 2021, Rais Magufuli alisema Serikali inatarajia kuongeza ndege nyingine zifike 11.

“Tumenunua ndege nane, tunaongeza nyingine tatu, Airbus mbili na Bombardier moja, tumeshaanza kuruka Bara la Afrika, sasa tunaenda Bara la Asia na baada ya muda tutaenda Ulaya na tunatumia fedha zetu wenyewe, kwa hiyo ndugu zangu chapeni kazi na mlipe kodi,” alihimiza.

Aidha ununuzi wa ndege unarahisisha shughuli za kibiashara kusafirisha watu na mizigo kwa wafanyabiashara kutoka eneo moja kwenda eneo lingine kwa haraka zaidi. Shughuli za kibiashara zinaporahisihwa zinasaidia mapato na uchumi wa nchi kuongezeka na kuimarika zaidi.

Kupitia makusanyo ya kodi yanayopatikana, Serikali inapata uwezo wa kuwahudumia wananchi wake mpaka waliopo vijijini kwa kuwapelekea huduma za afya, nishati ya umeme, maji, pembejeo za kilimo, ujenzi wa barabara, madaraja na vivuko.

Ni kwa mantiki hiyo, ni vyema kusema serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Magufuli imefanyia kazi ipasavyo kauli ya Mwalimu Nyerere ya kuhimiza nchi kukusanya kodi kwa maedeleo yake. Na hii imedhihirisha kwamba hii siyo serikali corrupt abadani.

Kifo cha Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamini Mkapa ...

foto
Mwandishi: Vicky Kimaro

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi