loader
Picha

JPM: Kiongozi Afrika anayetamani maendeleo makubwa kuliko madaraka

PAMOJA na sifa nyingine nyingi, sifa ya kuongoza kwa misingi na utaratibu wa kikatiba ndio naweza kusema imeisaidia sana CCM kuendelea kubakia madarakani na kuongoza nchi kwa amani, umoja na mshikamano madhubuti.

Chama cha TANU kilichozaa CCM, kiliongoza katika misingi ya kuheshimu haki za binadamu, kupinga unyonyaji, rushwa na ulevi wa madaraka. Chama hicho kiliamini na kutambua kuwa cheo ni dhamana tu na si vinginevyo. Ni kwa msingi huo mwanachama wa Tanu alipaswa kuapa hatokitumia cheo chake kwa manufaa yake isipokuwa yale ya umma.

TANU ilitafsiri rushwa kuwa ni adui mkubwa sana wa haki na kila mwanachama alipaswa kuapa hivyo na kwamba ataipinga rushwa kwa nguvu zake zote. Misingi hii ilirithiwa na CCM pale chama hicho kilipozaliwa mwaka 1977 na kimeendelea kuidumisha na hivyo CCM kuimarika kwa vitendo.

Ingawa kuna wakati kilianza kwenda nje ya misingi hiyo, lakini kiligundua hilo baada ya kujitathimini na kuja na mkakati wa kujivua gamba. CCM kimekuwa kikijitathmini mara kwa mara. Ninakumbuka wakati fulani tathmini hiyo ilifanywa na aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Chama hicho, Wilson Mkama na hata Katibu wa CCM wa sasa, Dk Bashiru Ally aliwahi pia kukifanyia tathimini chama hicho wakati akihakiki mali zake.

Viongozi wengi wa CCM wamelelewa na kukua katika misingi ya kuheshimu na kuthamini vyeo kama dhamana wanayopewa kwa kuaminiwa na kuheshimiwa kwa ajili ya kuongoza wananchi kwa maslahi mapana ya taifa bila kuwa na ulevi na uroho wa madaraka. Chama hicho pia kimekuwa kikiepuka usultani kwa kuachiana kijiti cha madaraka ya uongozi tofauti na baadhi ya vyama.

Mwalimu Nyerere aliwahi kusema kwamba madaraka ni mzigo na kwamba kiongozi anapaswa kuelewa kwamba matatizo ya wananchi ni mzigo wake na hivyo ana dhima ya kuubeba. Pia akatahadharisha kwamba mtu mkweli kabisa kabisa hakimbilii Ikulu kwa sababu ni kazi tu na pia ni mahala patakatifu, hakuna biashara na wala si pango la walangizi.

Akatutaka Watanzania kumwogopa mithili ya ugonjwa wa ukoma kiongozi anayekimbiia Ikulu, na hususani kwa kuwahonga wapiga kura. Nchi nyingi za Afrika zimeendelea kukumbwa na machafuko na migogoro ya kisiasa inayosababisha vita vya wenyewe kwa wenyewe kutokana na kutotilia manani maono kama haya ya Mwalimu Nyerere.

Kama ambavyo amekuwa akisema mwanaharakati ambaye pia mwanasheria wa Kenya, Patrick Oluoch Lumumba (PLO) wanasiasa wengi wa Afrika wamekuwa wakikibilia Ikulu si kwa sababu ya kutatua mizigo ya wananchi wao bali kushibisha matumbo yao.

Mbaya zaidi, viongozi hawa ‘maslahi’ wamekuwa ving’ang’anizi wakishaingia Ikulu kutokana na kuendelea kutaka kunyonya wananchi wao au kutokana na hofu ya kushitakiwa kutokana na utawala wao mbovu, kuumiza wananchi au kuiba mali za umma. Lakini kuna tatizo pia la wapenda madaraka wengine Afrika wanaoanzisha chokochoko za kutaka tu kuingia Ikulu kwa nguvu hata kama kuna kiongozi imara, mwenye maono na mwenye kubeba vilivyo matatizo ya wananchi.

Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, CCM ilimsimamisha Dk John Magufuli, mtu ambaye hadi miezi michache ya kuchukua fomu ya kugombea urais kupitia chama hicho hakuwa anafikiriwa. Licha ya kuwa na rekodi nzuri pengine kuliko waziri yeyote katika tawala zilizokuwa zimepita tangu Tanzania iiingie kwenye uchaguzi wa vyama vingi, lakini hakuonekana kutaka sana kugombea nafasi hiyo.

Ni mgombea aliyeingia katika kinyang’anyiro cha urais bila makundi na bila ‘kumwaga’ pesa au kuchangiwa na wapambe ‘nuksi’ ili kufanikisha kampeni zake. Wakati wa kampeni zake, Dk Magufuli alinadi sera za CCM na kuahidi kuzitekeleza kwa vitendo na wengi wetu hatukuamini kutokana na mazoea kwamba sera za vyama nyingi huwa tamu kuzisikia na hutangazwa sana wakati wa kampeni lakini baada ya uchaguzi utekelezaji wake huwa wa kusuasua na nyingi kutotekelezeka kabisa.

Serikali ya awamu tano ilipoingia madarakani Novemba, 2015 ilianza kwa kasi kubwa sana utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015, 2020. Inawezekana kwamba haijatekeleza zote kwa asilimia 100 lakini mingi, tena mikubwa zikiwemo sera ya elimu bila malipo, uboreshaji wa huduma za jamii ikiwa ni pamoja na maji, afya na umeme, zimekuwa zikitekelezwa kwa mafanikio makubwa na kwa muda mfupi sana.

Miradi mikubwa ya kimkakati inayotekelezwa hapa nchini ni pamoja na ujenzi wa reli ya kisasa, bwawa la ufuaji wa umeme katika bonde la mto Rufiji, ujenzi wa barabara za lami na madaraja likiwemo daraja la Kigongo-Busisi ambalo litakuwa refu kuliko yote Afrika Mashariki.

Ufanisi huu mkubwa umesababisha wananchi wengi nikiwemo mimi kuwa na imani kubwa sana na uongozi wa Rais Magufuli. Kuimarika kwa huduma za usafiri wa reli na anga ni moja katika mafanikio na mabadiliko makubwa ambayo yamewagusa sana wananchi kwani ni mambo yanayorahisisha shughuli za biashara na usafirishaji nchini.

Lakini ikumbukwe kama kuna jambo kubwa limefanyika katika serikali hii ya awamu ya tano ni kupambana na ufisadi na hatimaye uliobaki baki sasa unaendelea kupumulia mashine. Katika awamu hii, nidhamu ya watumishi wa umma katika kuwahudumia wananchi imekuwa ya hali ya juu. Ile tabia ya kufanya kazi kwa mazoea imepungua sana ama haipo tena katika maeneo mengi.

Watanzania sasa wanakula matunda yanayotokana na uchapaji kazi ya Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Magufuli. Haya na mengine mengi yanayoendelea kufanywa na kutekelezwa na awamu hii yakiwagusa hasa wananchi wanyonge wa nchi hii yamewaibua baadhi ya watu yakiwemo makundi mbalimbali ya kijamii kutaka Rais Magufuli, ikiwezekana aongezewe muda wa kuongoza nchi yetu hata baada ya miaka yake kumi kukamilika kama ilivyoelezwa katika katiba ya nchi.

Rais mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi alishaweka hadharani msimamo wake kwamba kama Watanzania wangelimkubalia ni kumwongezea muda mchapakazi huyu hodari kuongoza nchi baada ya miaka yake 10. Lakini hivi karibuni Rais John Magufuli alirejelea kusema kwamba hana mpango wala hafakirii kutaka kutawala zaidi baada ya muda wake wa miaka 10 kumalizika.

Alianza Januari mwaka juzi pale alipomwelekeza katibu wa itikadi na uenezi wa Halmashauri Kuu ya CCM, Humphrey Polepole kuwajulisha wana CCM na Watanzania kwa ujumla kuwa hafurahishwi na mjadala uliokuwa unaendelea juu ya kuongezewa kipindi cha urais.

Hata hivyo, Aprili mwaka jana akizungumza na wananchi Wilayani Newala mkoani Mtwara, Rais Magufuli alisema muda wake wa uongozi ukiisha ataondoka na yeye si Rais wa maisha.

Desemba 13, mwaka jana katika mkutano wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi jijini Mwanza, Rais Magufuli alisema CCM ni kiwanda cha kutengeneza viongozi na kuwatoa wanachama hao hofu kwa kusema akimaliza muda wake atapatikana kiongozi mwingine atakayemrithi.

Kama hiyo haitoshi Desemba 18, akihutubia wananchi katika uzinduzi wa mradi wa visima vya maji katika shule ya msingi Chato mkoani Geita, Rais Magufuli alirudia kusema kwamba hategemei kuongeza hata siku moja baada ya kumaliza muda wake wa urais “kwa sababu muda nitakaokuwa nimepewa kwa mujibu wa katiba ndio nitakaokuwa nimepewa na Mungu kuwatamkia watanzania.”

La msingi ni kwamba Rais Magufuli amekuwa ni mzalendo wa kweli anayejali na kupigania haki na maendeleo ya watanznia wote bila ubaguzi wowote. Ni mtu ambaye angetamani Tanzania ikimbie kimaendeleo ikiwezekana kesho nchi iamke tajiri kama nchi zingine zilizoendelea.

Na inshallah tutafika. Mwandishi wa makala haya ni Mwalimu kitaaluma na mchangiaji wa gazeti hili. Mawasiliano yake ni 0755985966

WAKAZI 1,639 wa vijiji vya Matongo na Nyabichune katika eneo ...

foto
Mwandishi: Samson Sombi

Weka maoni yako

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi