loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Kasi uboreshaji daftari la kudumu Wapiga Kura inazidi kupendeza

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) imeanzishwa kwa mujibu wa Ibara ya 74 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 na kupewa majukumu mbalimbali ya msingi ikiwa ni pamoja na kusimamia na kuratibu uandikishaji wa wapigakura katika uchaguzi wa rais na wabunge katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na uchaguzi wa madiwani kwa Tanzania Bara.

Uboreshaji huo wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, kisheria hutakiwa kufanyika mara mbili ndani ya miaka mitano, yaani baada ya Uchaguzi mmoja kumalizika na kabla ya unaofuata kufanyika.

Uchaguzi Mkuu wa Rais na Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Madiwani wa Tanzania Bara wa mwaka 2015, umeshamalizika ndiyo maana Julai 18, mwaka 2019, Waziri Mkuu, Kassimu Majaliwa Majaliwa alialikwa na Tume kuzindua Uboresha wa Daftari la kudumu la Wapiga Kura wa mikoa 31 ya Tanzania kwa awamu ya kwanza katika Mkoa wa Kilimanjaro. Baada ya uzinduzi huo, uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ulishika Kasi katika mikoa mingine.

Hadi sasa mikoa 18 tayari imeshaboresha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura. Mikoa ambayo mpaka sasa imekamilisha uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ni Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Simiyu, Mara, Mwanza, Shinyanga, Geita, Kagera, Kigoma, Tabora, Katavi, Rukwa, Songwe, Singida, Dodoma, Mbeya na Iringa.

Mikoa 13 iliyobaki katika uboreshaji huu ingawa mchakato unaendelea katika mikoa hiyo ni Njombe, Ruvuma, Mjini Magharibi, Kaskazini Unguja, Kusini Unguja, Kaskazini Pemba, Kusini Pemba, Lindi, Mtwara, Tanga, Morogoro, Pwani na Dar es Salaam.

Ukiangalia takwimu za awali, utaona kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeenda kwa kasi sana kuboresha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika mikoa mingi zaidi ukilinganisha na iliyobaki pamoja na changamoto za kusimamisha zoezi la uboreshaji kupisha masuala mengine ya kitaifa kama; Uchaguzi wa Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mitihani ya Darasa la Saba, Kidato cha Pili na Kidato cha nne.

Kutokana na kasi iliyonayo Tume, Zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumi la Wapiga Kura kwa mikoa 13 iliyobaki linatazamiwa kumalizika mwezi Februari, 2020. Awamu ya kwanza itaisha pale tu, daftari la awali la litakapowekwa wazi katika Ofisi za Kata Mwezi Machi, 2020 ili wapigakura walioandikishwa upya na walioboresha taarifa zao waangalie majina yao kama hayajakosewa na taarifa zao kama ziko sahihi na kuwawekea pingamizi wale ambao wameandikishwa kwenye daftari hilo, lakini hawana sifa za kuwemo kwenye daftari hilo.

Watu ambao hawana sifa za kuandikishwa kuwa wapigakura wapya kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga kura ni wale ambao ni raia wa nchi nyingine, wana utii wa nchi nyingine, wamethibitishwa na daktari kuwa hawana akili timamu na wamehukumiwa adhabu ya kifo na mahakama.

Sababu nyingine ambazo zinazweza kuwakosesha watu wasiandikishwe kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga kura ni kwamba wanatumikia kifungo cha zaidi ya miezi sita gerezani, wamezuiliwa kujiandikisha kuwa wapigakura na sheria za uchaguzi ama sheria nyingine kwa makosa yanayohusiana na uchaguzi na hawatakuwa wametimiza umri wa kupiga kura ifikapo siku ya uchaguzi.

Watu ambao wana sifa za kuandikishwa kuwa wapigakura wapya katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ni wale ambao ni raia wa Tanzania, wametimiza umri wa miaka 18 na kuendelea au watatimiza umri wa miaka 18 ifikapo siku ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020. Wengine ni wale ambao hawajapoteza sifa kwa mujibu wa sheria za uchaguzi au sheria nyingine yoyote iliyotungwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Zoezi hili la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga kura kwa jumla litawahusu wananchi wote waliotimiza umri wa miaka 18 na kuendelea ambao hawakuandikishwa mwaka 2015, watakaotimiza umri wa miaka 18 Oktoba, 2020, waliojiandikisha 2015 na sasa wamehama kata na jimbo moja kwenda lingine.

Wananchi wengine watakaohusika katika kazi hii ni wale ambao walikosa sifa za kupiga kura mfano kuondoa wale waliofariki dunia au wamepata uraia wa nchi nyingine, wale ambao jinsia zao, tarehe za kuzaliwa na majina yao yalikosewa wakati wa uandikishaji wa mwaka 2015, waliopoteza kadi zao na wale ambao kadi zao za kupigia kura zimeharibika.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) inatumia njia mbalimbali kuwahimiza na kuwahamasisha wananchi wote wanaohusika na zoezi hili la uboreshaji waende vituoni kujiandikisha na kuboresha taarifa zao ili waweze kushiri Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020.

Njia ambazo Tume inatumia kuwahimiza na kuwahamasisha wananchi waende vituoni ni matangazo kupitia vyombo vya habari kama magazeti, redio na televisheni vikiwamo vipindi mubashara vya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.

Njia nyingine ni kupitia matumizi ya gari la matangazo la Tume na gari la matangazo la halmashauri, asasi za kiraia, kushiriki maonesho mbalimbali ya kitaifa kama Sabasaba, Nanenane, mikusanyiko ya kijamii kama vile masoko, matamasha na kupitia mitandao ya kijamii.

Tume inatoa rai kwa namna ya pekee kwa kila mwananchi mwenye sifa ya kuandikishwa kuwa mpigakura aende kituoni akajiandikishe na mwenye kuhitaji kuboresha taarifa zake, naye aende kituoni akaziboreshe ili apate kadi yake kama kaulimbiu inavyosema: “Kadi Yako Kura Yako, Nenda Kajiandikishe.” Mwandishi ni Ofisa Habari wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec).

HUDUMA bora za afya ya msingi zinapunguza uhitaji, gharama na ...

foto
Mwandishi: Bathromeo Wandwi

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi