loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mbunge aliyefariki alikuwa akiishi na mashine

ALIYEKUWA Mbunge wa Newala Vjijini, Rashid Ajali Akbar (CCM) amezikwa katika kijiji cha Chihangu kilichopo Newala Vijijini, huku mazishi yake yakihudhuriwa viongozi wakiwemo mawaziri.

Akbar alifariki dunia juzi katika nyumba yake ya wageni ya Mingoyo Mnazi mmoja Mkoani Lindi baada ya kusumbuliwa na ugonjwa wa moyo kwa muda mrefu.

Kwa mujibu wa Mganga Mfawidhi Hospitali ya Sokoine mkoani Lindi, Nicolas Mmuni marehemu alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa moyo kwa muda mrefu na wiki iliyopita alikuwa akipata matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Muhimbili, Dar es Salaam na kuruhusiwa.

“Lakini pia kwa shida yake ya moyo marehemu aliwekewa mashine ya kuuwezesha moyo kufanya kazi vizuri ambayo alikuwa anatembea nayo ndani ya mwili wake,” alisema.

Dk Mmuni alisema katika eneo alilofia Mnazi Mmoja, zilikutwa dawa alizokuwa akitumia kwa ajili ya matibabu zinazohusiana na matatizo ya moyo.

Viongozi kadhaa waliohudhuria mazishi hayo walimuelezea mbunge huyo kama mchapakazi kazi na aliyekuwa na uzoefu mkubwa katika utumishi.

Baadhi ya wabunge wakiwemo Mbunge wa Newala Mjini, George Mkuchika na Mbunge wa Nanyamba, Abdallah Chikota kwa nyakati tofauti walimuelezea mbunge huyo kuwa alikuwa ni mtu ambaye wakati wote yuko karibuni na jamii na kufanyakazi kwa karibu na wabunge wenzake.

“Tutamkumbuka kwa mazuri yake mengi aliyoyafanya enzi za uhai wake ikiwemo shughuli mbalimbali za ujasiriamali alizokuwa akizifanya mfano hapa Newala aliwekeza hoteli ambayo ilikuwa ikitoa huduma kwa jamii kutoka maeneo tofauti ndani na nje ya Mtwara,” alisema Mkuchika.

Naye, Chikota alisema Akbar pia aliwekeza kwenye mambo mengi ikiwemo kujishughulisha na ujasiriamali.

“Tutamuiga katika mambo mengi tu katika suala la ujasiriamali, masuala ya uongozi na ukaribu wake na jamii. Pia alikuwa yuko vizuri na sisi kama wabunge tulikuwa tukifanya kazi kwa ushirikiano kwa maslahi ya wananchi wetu na taifa kwa ujumla,” alisema Mbunge huyo.

Kwa upande wake, Rais Dk John Magufuli alimtumia salamu za rambirambi Spika wa Bunge Job Ndugai kutokana na kifo cha ghafla cha mbunge huyo.

Dk Magufuli alielezea kuhuzunishwa kwake na kifo cha Akbar ambaye wakati wa uhai wake aliwatumikia wananchi wa Newala Vijijini kwa dhati na alifanyakazi kwa ushirikiano mzuri na viongozi wake katika Bunge, chama na serikali.

“Spika naomba unifikishie salamu zangu za pole kwa familia ya Akbar, wabunge, wananchi wa Newala Vijijini na wote walioguswa na msiba huu, nawaombea moyo wa uvumilivu na ustahimilivu katika kipindi hiki cha majonzi,” alisisitiza Rais Magufuli.

Aidha, Chama cha Mapinduzi (CCM) taifa kupitia Mwenyekiti wake, Rais Dk Magufuli kimetoa salamu za rambirambi kutokana na msiba huo.

Kwa mujibu wa Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole, mbunge huyo alikuwa na mchango mkubwa katika kamati ya wabunge wa CCM.

“Amekisaidia chama kutambua changamoto za wilaya ya Newala hasa jimbo la Newala vijijini na kuziwasilisha bungeni ikiwemo kuzifuatilia utekelezaji wake,” alisema Polepole.

Akisoma wasifu wa marehemu Katibu wa Bunge, Steven Kigaigai alisema kuwa, marehemu alikuwa na uzoefu mkubwa wa kazi na utumishi hasa katika eneo la uhasibu kwani kuanzia mwaka 1987 alifanyakazi ya uhasibu katika Benki ya Taifa ya Biashara (NBC), Mamlaka ya bandari, kampuni ya Tanzania Limited na shirika linalomikiwa na Chama cha Mapinduzi (SUKITA).

Akielezea shughuli zake za kisiasa, alisema mwaka 2000 mpaka 2005 alikuwa diwani wa Kinondoni Jijini Dar es salaam na alitumikia shughuli za ubunge kwa kipindi cha miaka mitano ikiwemo mwaka 2015 hadi mwaka huu 2020 alipopatwa na umauti. Mbunge huyo ameaacha mjane na watoto wanne wakiwemo wakike wawili na wakiume wawili .

Baadhi ya viongozi waliohudhuria msiba huo ni pamoja na Waziri wa Maji Profesa Makame Mbarawa ambaye yuko katika ziara ya kikazi wilayani Newala, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Jenista Muhagama na mkuu Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa.

foto
Mwandishi: Sijawa Omary, Mtwara

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi