loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mwamba wa Malameni ulivyotumika kuangamiza watoto wenye ulemavu

KWA mujibu wa Kamusi Kuu ya Kiswahili, utamaduni (tamaduni) ni mwenendo wa maisha ya jamii unaohusisha asili, mila, desturi, jadi au itikadi na mtazamo katika jamii fulani; mtindo wa jumla wa maisha wa jamii fulani.

Utamaduni ndio unaitofautisha jamii moja na nyingine. Kitaifa, utamaduni ndicho kitambulisho kikuu cha taifa na ni kielelezo cha utashi na uhai wa watu wake. Nguzo za utamaduni ni pamoja na mila na desturi, lugha, michezo na historia. Kwa mfano, katika baadhi ya mila na desturi za makabila, mtoto akizaliwa hakuna mtu anayeruhusiwa kumwona zaidi ya mama mpaka baada ya sherehe ya kumpa jina.

SAME, KILIMANJARO

Wilaya ya Same ni kati ya wilaya sita zinazounda mkoa wa Kilimanjaro ikiwa umbali wa kilometa 105 kutoka Moshi mjini. Same ilioanzishwa mwaka 1962 inakadiriwa kuwa na wakazi wapatao 296,287 na idadi ya kaya zipatazo 65,842. Hali ya hewa ya wilaya ni ya kiwango kati ya nyuzi joto 15 hadi 30 na kiwango cha mvua cha wastani wa kati ya lita za ujazo 500 hadi 2,000 kwa mwaka.

Kiikolojia, Wilaya imegawanyika katika Kanda tatu; Ukanda wa juu ambao ni milimani, eneo linalofaa kwa kilimo cha tangawizi, kahawa, ndizi, maharage, miwa, miti (kwa ajili ya mbao/ boriti/kuni) na matunda mbalimbali kama mapapai, na maparachichi. Ukanda wa kati na ukanda wa chini ambao ni tambarare.

Ukanda wa tambarare katika wilaya ya Same una hali ya kijangwa na makazi mtawanyiko na wakazi wa maeneo hao wanaojishughulisha na ufugaji. Katika wilaya hiyo kuna Hifadhi ya Mkomazi ambayo ilianzishwa mwaka 1951 kama pori la akiba la Mkomazi –Umba, kutoka katika pori Tengefu la Ruvu na lina ukubwa wa kilometa za mraba 3600. Hifadhi ya Mkomazi yenye ukubwa wa kilometa za mraba 3245 iko Same kwa asilimia 61 na Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga kwa asilimia 39.

KABILA LA WAPARE

Wapare ni kabila kutoka milima ya Pare, Mkoa wa Kilimanjaro, Kaskazini mwa nchi ya Tanzania. Kabla ya kuingia huko, inasemekana watu wa kabila hilo walikuwa wanaishi Taveta nchini Kenya, kwa zaidi ya karne moja iliyopita na wakati huo walikuwa wakijulikana kwa jina la Waasu.

Masimulizi yanaonesha kuwa, Waasu walipoingia Tanganyika, walitamani kufanya makao yao kwenye miteremko ya Mlima Kilimanjaro, lakini wakavurumishwa na wenzao waliokuwepo kabla yao, yaani Wachaga.

Wachagga hao hawakuwa radhi kuwaruhusu Wapare kuwa na makazi eneo hilo, hivyo waliwafukuza kwa kupigana kama ilivyokuwa tabia ya makabila mengi hapo zamani. Wakati wa kupambana walikuwa wakiambiana, “Mpare… Mpare” wakimaanisha kwamba ‘Mpige… Mpige!’ Waasu hawa wakatimka mbio na kuparamia milima ambayo sasa inaitwa milima ya Upare.

Waasu wakaanza kuitwa Wapare kwa maana ya “Wapige”. Hizi ni hadithi zinazosimuliwa na baadhi ya Wachagga ambao ndio watani pekee wa Wapare, utani uliozaliwa baada ya purukushani hizo za kuingia Tanganyika. Hata hivyo, hakuna hata Mpare mmoja anayeafiki maelezo hayo, isipokuwa wanakiri kuwa walitokea Taveta, ndiyo maana hata baadhi ya maneno na lafudhi yao haiko mbali sana na watu wa Taveta.

Zamani Wapare walikuwa na sala tofauti kwa kila ukoo na eneo lao la tambiko. Katika karne ya 19 hadi 20 Wamisionari waliingia maeneo mengi ya Upare. Imani za Wapare kwa sasa zinatofautiana kutokana na maeneo, walio kusini mwa wilaya ya Same katika maeneo ya Ndungu, Kihurio, Bendera, Hedaru, Makanya, Suji, Chome, Tae, Gonja, Mamba hadi Vunta kuna waumini wa Kanisa la Wasabato ambao ni wengi sana. Maeneo Kama Chome, Mbaga, Gonja, Vudee yana waumini wengi wa Kanisa la Kilutheri, katika Wilaya ya Mwanga kuna idadi kubwa ya Walutheri na Waislamu. Wakatoliki, japo ni wachache, wanapatikana zaidi katika maeneo ya Kisangara Juu, Vumari na Mbaga.

MWAMBA WA MALAMENI

Hadi kufikia mwaka 1930, mila na desturi za Wapare katika kuwatoa watoto wenye ulemavu wakidai kuwa ni kuondoa mapepo ambayo yangeweza kuwasababishia laana na mikosi katika familia hizo zilikuwa zikiendelea kufanya, hii ikiwa ni kabla ya Wamishionari wa Kikristo kuanza kueneza neno la Mungu katika milima hiyo ya Upareni. Inaelezwa kwamba hata mapacha walichukuliwa pia kama mkosi na kuuawa. Miaka ya mwishoni mwa 1800 Ukristo ulianza kupenya katika milima hiyo.

Mchungaji mmoja kutoka Leipzig aliyefahamika kwa jina Jacob Jenson Dannholz, alijenga kanisa katika kijiji cha Mbaga ambako Malameni Rock inapatikana kati ya mwaka 1908 hadi 1917. Hadi sasa unapofika katika Vilima vya Mbaga ili uweze kwenda kujionea namna mwamba huo ulivyo, itakulazimu utembee muda wa saa moja na nusu hadi kufika kwenye jiwe hilo la Malameni ambalo lilikuwa likitumika kuwatoa watoto wenye ulemavu. Na ukifika hapo ni sharti upewe maelekezo na wazee wa eneo hilo kuhusu historia ya jiwe hilo.

USHUHUDA WA MCHUNGAJI

Ushuhuda huu ni wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri unatolewa na Mchungaji, Martin Kosmalla, ambao aliuhifadhi kwa njia ya maandishi tangu mwaka 1932. “Jana nilikuwa nikiitwa na mwanamke mara mbilimbili, niliambiwa kuwa mwanamke huyo alikuwa na maumivu makali na kwamba asingeweza kuzaa mtoto,” anaanza Mchungaji Kosmalla katika ushuhuda wake.

“Nilikwenda katika nyumba yake kumwona na kwamba kama naweza kumsaidia. Nilipofika nilimkuta na kumchunguza mtoto aliye tumboni ambaye mapigo ya moyo yalikuwa yakidunda vizuri na nilikuwa na matumaini ya kumwambia mwanamke yule habari njema”

“Mtoto wako ni mzima, anaishi, yu hai hajafa. Ndipo nilipoliona tabasamu likionekana kwa mwanamke yule aliyekuwa amejawa na huzuni na maumivu makali na alikubaliana na maneno yangu.”

Mchungaji Kosmalla, anasimulia zaidi kuwa, baada ya tukio lile kupita siku ile, usiku wake akiwa nyumbani kwake amelala, aligongewa mlango na alipotoka nje alikutana na baba wa familia ya yule mwanamke, aliambiwa kwamba mkewe amejifungua mtoto wa kiume na kinachovutia zaidi hali yake ya afya ilikuwa nzuri na mkewe anaendelea vizuri.

Mwanaume wa kabila la Wapare anaweza akawa tajiri wa mifugo na mali nyingi lakini pasipokuwa na watoto basi huonekana kama mtu maskini. Hali hiyo huwekwa msisitizo na methali mbalimbali, kwamba mwanaume tajiri bila watoto sifa zake ni bure na utajiri wake ni nani atakayeulinda. Mchungaji Kosmalla anasema licha ya kuzaliwa kwa watoto lakini kwa kabila la Wapare kitu kingine cha ziada kinachoangaliwa baada ya mtoto kuzaliwa ni hali na afya yake.

“Endapo kutakuwa na hitilafu katika mwili wa mtoto, hofu huikumba familia yote na kifo itakuwa ndio zawadi pekee kwa mtoto huyo,” anasema Mchungaji Kosmalla.

Katika mwamba wa Malameni uliopo katika kijiji cha Mbaga-Manka ndio mahali ambapo watoto wasio na hatia walikuwa wakiuawa kwa kuweka juu nyakati za usiku na mama zao, ambao huwapeleka katika jiwe hilo na pindi wanapofika katika jiwe hilo, huwanyonyesha na kuwabembeleza hadi usingizi utakapowashika, kisha kuwalaza hapo ili watakapozinduka wataviringika kutoka juu hadi chini na ndio hadithi yao huishi palepale.

Jiwe hilo pia wengine waliliitwa ‘Mkumba vana’ Mama zao baada ya kuwabembeleza kuondoka hapo kwa machozi makubwa wakilia, kwani hawatakuja kuwaona tena watoto wao, lakini yote hayo ni kwa sababu ya ulemavu waliozaliwa nao au kuzaliwa wakiwa mapacha. Mchungaji huyo anasimulia siku moja wakati akiendelea na huduma yake katika milima ya Pare aliamua kuondoka na waamini wake kwenda katika mwamba ambao ulikuwa ukiangamiza watoto hao waliozaliwa wakiwa na ulemavu.

Mchungaji Kosmalla anasema wakati wa kupanda kwenda katika mwamba huo, walikuwa wakipanda taratibu na kwa uangalifu mkubwa kutokana na mwinuko wake kuwa mkali ili waweze kufika katika kilele cha mwamba huo na baada ya kufika hadi kilele cha mwamba huo alisimama huko na kuwaambiwa waumini wake.

“Hapa ndipo mahali ambapo watoto wenye ulemavu, wasio na hatia walihukumiwa na mama mwenye mtoto alikuwa akimbusu mtoto wake kwa mara ya mwisho na kumwacha hapa asimwone tena kwani atakapozinduka katika usingizi ataviringika kutoka juu hadi chini na kupoteza maisha.”

DHANA YA ULEMAVU ILIVYOJENGEKA

Kwa mujibu wa kamusi ya mtandaoni Wikipedia; Ulemavu ni hali ya kuwa na hitilafu ya kudumu mwilini au akilini inayomzuia mtu kutekeleza shughuli zilizo kawaida katika maisha ya jamii.

Unamwekea mtu mipaka asiweze kutekeleza shughuli fulani katika maisha yake, tofauti na watu wengine. Kuna nchi nyingi walemavu wana klabu za michezo au kuendesha michezo katika vitengo vya pekee vya klabu za kawaida. Kwa kawaida wanatekeleza michezo ya kawaida lakini kufuatana na kanuni zinazolingana na hitilafu zao. Lakini cha kushuruku ni kwamba mila hii potiofu haipo tena na Mwamba wa Malameni au Mkumba Vana umebaki sasa kuwa eneo la utalii.

foto
Mwandishi: Cheji Bakari

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi