loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mashabiki Genk wamuaga Samatta

MASHABIKI wa klabu ya KRC Genk ya Ubelgiji wamemuaga Mshambuliaji wa Kimataifa wa Tanzania, Mbwana Samatta wakimshukuru na kusema watamkumbuka kwa heshima na mchango wake alioutoa kwa klabu yao.

Kupitia ukurasa wao wa mtandao wa kijamii wa Istagram uitwao KRC Genk Forever walichapisha picha ya Samatta, ambaye anatarajiwa kujiunga na klabu ya Aston Villa inayocheza Ligi Kuu ya England.

“Ulikuja kama kijana wa kawaida, lakini sasa unaondoka kwa heshima kupitia lango kuu ukiwa kama gwiji. Tunalia kwa kuwa unatuacha, lakini tunajivunia na kuona fahari kwa kuwa tumekushuhudia ukiwa umevaa jezi yetu kwa kipindi cha miaka minne,” waliandika.

“Wewe Samatta ni mmoja kati ya watu wakubwa na wa maana sana katika historia ya Genk. ASANTE ALLY MBWANA SAMATTA” walimalizia kuandika kwa maandishi makubwa.

Samatta mwenye umri wa miaka 27 amecheza mechi 191 akiwa KRC Genk akifunga mabao 76 na kutoa pasi ya mwisho 20, Jana Samatta alitarajiwa kufanyiwa vipimo tayari kujiunga na Aston Villa kwa dau la Pauni Milioni 10 kuimarisha safu ya washambuliaji katika klabu hiyo ambayo ipo katika nafasi ya 18 baada ya kucheza mechi 22.

Samatta ambaye ana kauli mbiu yake isemayo “Haina kufeli” mara nyingi amekuwa akiwaasa wachezaji hasa vijana kupambana maana hakuna kisichowezekana. Ukiangalia machapisho yangu ya Instagram nataka kuwashauri vijana kuhusu maisha na namna ya kufanikiwa.

Najaribu kutuma ujumbe kwamba kwenye maisha unaweza kuvuka changamoto nyingi lakini mwisho wa siku utafanikiwa tu kama una malengo na kuyafanyia kazi.- Mbwana Samatta.

Mchezaji huyo jana alifanyiwa vipimo vya afya kabla ya kusaini mkataba rasmi wa kuichezea timu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu ya England.

foto
Mwandishi: Rahel Pallangyo

Post your comments