loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Takukuru yaokoa Sh mil 60 za wakulima wa tumbaku

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Tabora imefanikiwa kuokoa zaidi ya Sh milioni 60 za wakulima wa tumbaku zilizokuwa zimechotwa na baadhi ya viongozi wa vyama vya msingi vya wakulima wa tumbaku (AMCOS) kwa nia ya kuwaibia.

Hayo yalibainishwa jana na Kamanda wa Taasisi hiyo mkoani Tabora, Mussa Chaulo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake. Alisema kuwa mafanikio hayo yametokana na uchunguzi wa kina uliofanywa na maofisa wa taasisi hiyo kwa kushirikiana na wananchi katika kipindi cha Oktoba hadi Desemba 2019 na jumla ya Sh milioni 69.9 za wakulima na taasisi nyinginezo ziliokolewa.

Alibainisha kuwa kutokana na jitihada hizo jumla ya Sh milioni 29.7 za wakulima zilizokuwa zimechotwa kwa ubadhirifu na viongozi watatu zilirudishwa kwenye chama cha msingi cha Ushirika cha Mitowo AMCOS kilichoko wilayani Sikonge. Chaulo alifafanua kuwa kutokana na ubadhirifu huo AMCOS ilishindwa kulipa stahiki za wakulima za mauzo ya tumbaku yao lakini baada ya taasisi hiyo kuingilia kati na kuchukua hatua fedha hizo zimerejeshwa na kuingizwa katika akaunti zao.

Aliongeza kuwa taasisi hiyo pia imefanikiwa kurejeshwa kwa kiasi cha Sh milioni 22 za chama cha msingi Mole AMCOS kilichoko wilayani Sikonge zilizokuwa zimelipwa isivyo halali kwa mtu ambaye hakuwa mwanachama kwa madai ya kuiuzia AMCOS hiyo tumbaku hali hiyo iliwezesha wakulima wote waliokuwa na madai kulipwa fedha zao.

Kamanda Chaulo alibainisha kuwa chama cha msingi Kilima AMCOS nacho kimerejesha jumla ya Sh milioni 5.8 za wakulima zilizokuwa zimekatwa kinyume na utaratibu huku chama cha msingi Igalula AMCOS kikirejesha kiasi cha Sh milioni saba zilizokuwa zikidaiwa na wakulima.

Aidha alisema kuwa chunguzi mbalimbali ambazo zimekuwa zikifanywa na taasisi hio pia zimewezesha kuokolewa kwa kiasi cha Sh milioni 5.3 na kurudishwa kwenye akaunti ya Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU.

Akizungumzia malalamiko yenye viashiria vya kuomba na kupokea rushwa na makosa mengineyo, Chaulo alisema walipokea jumla ya malalamiko 109 kati ya mwezi Oktoba na Desemba 2019 ambapo majalada 10 ya uchunguzi yamekamilika na kufungua kesi mpya 5 mahakamani. Alieleza kuwa mashauri 19 yanaendelea kusikilizwa mahakamani na kesi moja imetolewa hukumu ambapo Jamhuri imeshinda, huku akibainisha kuwa majalada yaliyokamilika yanahusisha watuhumiwa ambao ni watu binafsi na watumishi wea umma.

TAKWIMU za udumavu ...

foto
Mwandishi: Lucas Raphael, Tabora

Post your comments