loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Kanyasu aagiza mifugo iliyokamatwa Mkungunero kurejeshwa

NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu ameiagiza Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania ( TAWA) kuiachia na kuirudisha mifugo ikiwemo ng’ombe 179 zilizokuwa zimekamatwa ndani ya Pori la Akiba la Mkungunero, mali ya Mathayo Marao, Mwananchi wa Kijiji cha Kimotorok kilichopo ndani ya pori hilo katika wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara kwa makubaliano ya kutoingiza tena mifugo hiyo.

Uamuzi huo umekuja kufuatia utata uliopo eneo ilipokamatiwa mifugo hiyo kwa vile kijiji hicho cha Kimotorok ni miongoni mwa vijiji na vitongoji 366 vilivyo ndani Hifadhi na vinavyosubiria maamuzi ya Rais John Magufuli na ni moja kati ya maagizo aliyoyatoa kwamba wananchi wa vijiji hivyo wasibuguziwe hadi pale maamuzi ya mwisho yatakapotolewa.

Kwa mujibu wa wahifadhi, mifugo hiyo iliyokamatwa mwishoni mwa mwaka jana inadaiwa kukutwa mita 450 ndani ya pori hilo huku wananchi wakidai kuwa mifugo hiyo ilikutwa nje ya mita 450 kutoka kwenye mpaka mahali ambako wamekuwa wakiishi huku wakisubiri kauli ya mwisho ya Rais.

Naibu waziri Kanyasu kutumia busara na kufikia uamuzi huo kwa kuzingatia kuwa kijiji hicho kipo ndani ya Hifadhi. Akizungumza jana katika mkutano huo uliofanyika kwenye Kijiji cha Kimotorok, Kanyasu alisema uamuzi huo umefanyika kwa busara kwa vile mifugo hiyo ilibidi ipelekwe mahakamani.

Alisema kitendo cha kuacha kupeleka kesi hiyo mahakamani kinasaidia kupunguza idadi kubwa ya mifugo kufa kwani hadi sasa zaidi ya ndama kumi wameshakufa na aliwataka wananchi hao kuacha kutumia vibaya kauli ya Rais Magufuli kwa kuvamia maeneo mapya ya Hifadhi kwa kisingizio cha kauli hivyo ilhali wanatakiwa kubaki na mifugo yao mahali walipo.

Katika hatua nyingine, Kanyasu alisema serikali haipendi kutaifisha mifugo inayokamatwa hifadhini kama sheria inavyoelekeza kwa vile wananchi wengi wamejikuta kwenye umasikini wa hali ya juu, hivyo aliwataka waache tabia ya kuingiza mifugo hifadhini kwa vile watafilisiwa.

Kanyasu pia alitoa onyo kwa wananchi wanaovamia wahifadhi wakiwa wanatekeleza majukumu yao na kuahidi kuwa serikali haitamvumilia mwananchi yeyote atakayethubutu kutumia mabavu dhidi ya wahifadhi.

Mbunge wa Simanjiro, James Millya aliwataka wananchi waache tabia ya kuingiza mifugo ndani ya Hifadhi na kulaani vitendo vya baadhi ya wananchi wanaohamasisha ghasia dhidi ya wahifadhi na kuahidi kuwa yeye hatakuwa tayari kumsaidia mwananchi yeyote atakayekamatwa kwa kutenda kosa hilo kwa vile wahifadhi hao wanafanya kazi za kulinda Hifadhi hizo kwa niaba ya watanzanua wote.

TAKWIMU za udumavu ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Maalumu

Post your comments