loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Matakwa ya mila yapaisha utapiamlo Singida

MILA potofu juu ya lishe katika baadhi ya makabila mkoani Singida, zimetajwa kuwa ni moja ya sababu ya watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano kukumbwa na utapiamlo kutokana na wazazi wao kutopata mlo kamili wakati wakiwa wajawazito na hata baada ya kujifungua.

Uchunguzi uliofanywa na Mwandishi wa habari hizi kwa jamii ya kabila la Wanyaturu, ambalo ndilo kabila kuu mkoani Singida, unaonesha kuwa licha ya elimu juu ya umuhimu wa lishe bora kwa wanawake wajawazito na anayenyonyesha kutolewa mara kwa mara, baadhi ya vyakula bado haviliwi na kundi hilo ili kutii matakwa ya kimila.

Patrick Mdachi ambaye ni Ofisa Maendeleo ya Jamii mstaafu alisema kuwa hadi hivi sasa ni mwiko kwa mwanamke mjamzito wa kabila la Kinyaturu kula mayai kwa imani kuwa mtoto atakayezaliwa hataota nywele kichwani na anaweza kufa ghafla.

Alisema vyakula vingine zinavyozuiwa na wazee wa mila ni pamoja na utumbo mwembamba kwa madai kuwa ndoa itayumba na maini kwa madai kuwa mtoto tumboni anatakuwa mnene na kuwa na uzito mkubwa, hivyo kusababisha upasuaji wakati wa kujifungua ambapo utumbo wa ‘daftari’ wa mbuzi au ng’ombe unaaminika kuleta mabaka kichwani kwa mtoto.

“Mimi ni mtafiti wa masuala ya kimila na nimeandika kitabu maalum cha Wanyaturu wenzangu na mila zao, kwa hiyo najua vyema na orodha ni ndefu ya vyakula vinavyozuiwa kuliwa na wajazito lakini itoshe tu kusema kuwa bado tuna safari ndefu kupinga mila potofu za lishe bora,” alisema Mdachi.

Baadhi ya wanawake wazee ambao hawakupenda kutajwa majina yao gazetini wanadai kuwa kuzuiwa kula baadhi ya vyakula ndiko kulikosababisha wanawake wengi kujifungulia nyumbani bila matatizo yoyote enzi hizo tofauti na hivi sasa kwani wengi wanaenda hospitalini na baadhi yao hujifungua kwa upasuaji huku matatizo yatokanayo na uzazi yakiwa lukuki..

Hata hivyo, Ofisa lishe wa Mkoa wa Singida Teda Sinde alisema hoja za wanawake hao zinadhihirisha wazi kuwa bado kuna changamoto kubwa ya mila potofu juu ya masuala ya lishe katika baadhi ya makabila na kuchangia kuwepo kwa tatizo la utapiamlo kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano kutokana na mlo duni kwa baadhi ya wanawake wajawazito na waliojifungua.

Alisema kuwa Ofisi yake imeona changamoto hiyo na kuanza kutoa elimu kwa jamii juu ya uandaaji wa lishe bora na kupiga vita mila potofu zinazozuia baadhi ya vyakula muhimu kiafya kwa sababu za kimila.

Takwimu za utafiti wa kitaifa juu ya hali ya lishe mkoani Singida kwa mwaka juzi (TNNS 2018 ) zinaonesha kuwa asilimia 29.8 ya watoto chini ya miaka mitano wana tatizo la udumavu, asilimia tano ukondefu na asilimia 15 wana uzito mdogo wakati asilimia 27.9 tu ya watoto hao ndio walionyonyeshwa maziwa ya mama kwa kipindi cha miaka miwili.

TAKWIMU za udumavu ...

foto
Mwandishi: Abby Nkungu, Singida

Post your comments