loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mil 400/- zatolewa kubadili zahanati kuwa kituo cha afya

SERIKALI imetoa Sh milioni 400 ili kupanua zahanati ya Kijiji cha Masinono kilichopo katika Kata ya Bugwema, Musoma Vijijini ili kiwe kituo cha afya.

Mkuu wa Wilaya Musoma, Dk Vincent Anney, alilieleza gazeti hili kwa simu jana kuwa, iwapo zahanati hiyo itapanuliwa, wilaya hiyo itakuwa na vituo vitatu vya afya vinavyofanya kazi.

“Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), imetoa kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya upanuzi wa zahanati ya Masinono ili iwe kituo cha afya,” alisema Dk Anney.

Alisema hivi sasa Musoma Vijijini ina vituo vya afya viwili vinavyofanya kazi na kuwa vituo hivyo vipo katika kata za Murangi na Mugango, huku vingine vikiendelea kujengwa.

“Mpango wa serikali ni kujenga kituo cha afya kila kata, hivyo hatua ya kutoa kiasi hicho cha fedha ni mwendelezo kutimiza mkakati huo, ambao unalenga kusogeza huduma za afya karibu na wananchi,” alisema.

Mkuu wa wilaya huyo alisema zipo zahanati zaidi ya 20 zinazotoa huduma za afya huku nyingine zikiendelea kujengwa ili kuhakikisha kila kijiji kinakuwa na zahanati.

“Tuna vijiji 68 na kata 21, tunaendelea kuhamasisha wananchi kuunga mkono juhudi za serikali za kuwaletea maendeleo, nao wanajitolea kwa hali na mali kushiriki, katika ujenzi wa zahanati na vituo vya afya,” alisema.

Mbunge wa Musoma Vijijini, Profesa Sospeter Muhongo, aliwaomba wakazi wa Kata ya Bugwema wajitume na kushirikiana ipasavyo ili upanuzi huo ukamilike mapema.

“Ndugu zangu wa Kata ya Bugwema, fursa imepatikana, naomba tujitume na tushirikiane ipasavyo, ili ujenzi ukamilike kabla ya Mei 30 mwaka huu... hongera Kata ya Bugwema. Ushauri wangu ni kwamba, wananchi tuchangie ujenzi huo ili fedha zilizotolewa na serikali ziweze kutupatia majengo mengi muhimu likiwamo jengo la chumba cha kuhifadhia maiti,” alisema Profesa Muhongo.

Alisema wakazi wa kata hiyo wamekuwa wakihifadhi maiti, katika chumba cha Kituo cha Afya cha Nyamuswa, Ikizu wilayani Bunda na kwamba muda umewadia wa kujenga chumba hicho kijijini Masinono.

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments