loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

'Nina watoto 10, nimezaa kama panya'

“NILIANZA kuzaa nikiwa binti mdogo wa miaka 19 na mtoto wangu wa kwanza nilimzaa mwaka 2000 na sasa nina watoto 10, nikiwa na umri wa miaka 37,” anasema Theopista Shukrani, mkazi wa kijiji cha Busiri kilichoko kilomita tisa kutoka Nansio, Ukerewe.

Huku akinyonyesha mtoto wake wa 10 mwenye umri wa mwaka mmoja, Theopista anaonekana mzee kuliko umri wake huku akionekana kudhoofu.

“Kwa kweli nimezaa kama panya… Yaani unajifungua baada ya miezi mitatu, minne unashtukia mimba tena imeingia, ukiwaambia watu wazima waliokuzunguka utasikia wanasema wewe zaa tu, mbona sisi zamani tulizaa,” anasema.

Theo anakiri kwamba elimu juu ya uzazi bora sambamba na mumewe kutokuwa na uelewa pia wa uzazi wa mpangilio, umemfikisha hapo alipo sasa.

Anasema idadi watoto aliozaa anadhani, siyo tu kwamba inatosha lakini imemzidi uwezo baada ya kuanza kuona maumivu ya kuhudumia watoto 10 hasa linapokuja suala la mahitaji kama chakula, mavazi na malazi.

Pamoja na kushukuru hatua ya serikali kuja na mpango wa elimu bure unaomhakikishia kwa asilimia nyingi watoto wake kuweza kusoma lakini anasema bado mahitaji ni mengi kama vile maji safi na salama, matibabu na hata mahitaji mengine ya shule.

“Kwa kweli mzigo wa kulea hawa watoto ni mkubwa na umenilemea kiasi kwamba sina uwezo wa kuwapatia mahitaji muhimu ikiwemo chakula cha uhakika,” anasema Theo ambaye baba wa watoto wake ni mvuvi ambaye anapoondoka kwenda kwenye shughuli zake katika visiwa mbalimbali huchukua muda mrefu kurejea, wakati mwingine hata baada ya miezi miwili.

Theopista anakiri kwamba wale waliokuwa wanamshauri kuzaa wanasahau kwamba zamani vyakula vilikuwepo vingi, mtu anaingia shamba anachimba viazi au mihogo anachemsha anakula.

“Lakini sasa hivi maisha tunahemea, hebu niambie leo unaujazito hauna chochote, maandalizi ya kujifungua yanahitaji fedha na ndio maana wataalamu wanasema tunahatarisha maisha yetu,” anasema Theo ambaye anatamani kufunga uzazi lakini bado hajui aanzie wapi kwa sababu mumewe ambaye wakati wa mahojiano haya alikuwa katika safari zake za kikazi, hajui kama anaweza kuafiki.

Edina Bahati ambaye pia ni mkazi wa Ukerewe alipitia hayo ya Theopista lakini sasa amejikwamua. Ingawa tayari ana watoto saba lakinikutokana na elimu ya afya ya uzazi aliyopata suala la kuzaa bila mpangilio limekoma.

“Mume wangu alikuwa pia mbabe. Alikuwa akininyanyasa, wakati mwingine anakuingilia bila kukuandaa, utasikia tu geukia huku…ilifika kipindi nilianza kulichukia tendo la ndoa, lakini baada ya kupata elimu ya afya ya uzazi ikanijengea ujasiri.

“Siku hiyo nilimpikia chakula mume wangu, wali na Sangara, nikaunga vizuri sana kwa nazi, nikamwandaa kwa upendo toka mchana baada ya kula na kushiba nikampa na haki yake ya ndoa, ndipo nilipoanza kuongea naye kwa upendo kuhusu kutoongeza idadi ya watoto na pia asiwe anadai haki ya ndoa kibabe. Mwanzo alibadilika na kuanza kuwa mkali

“Lakini nilimsihi sana. Akaniuliza tunaipata wapi hiyo njia ya uzazi wa mpango kwenye miti shamba? Nikamwambia hapana kwenye vituo vya afya. Kwa kweli baada ya hapo hata afya yangu inaimarika na kwa sasa hanisumbui kuhusu suala la kumpa unyumba mpaka niwe tayari.”

Usipogeuka kipigo

Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa makala haya katika vijiji mbalimbali vya Ukerewe unaonesha kuwa asilimia kubwa ya wanaume hawataki kusikia habari ya uzazi wa mpangilio.

Halikadhalika, wengi wanadhani kwamba njia nyingi za uzazi wa mpango siyo salama na wapo wanaodhani kwamba zinasababisha ugumba. Pia wapo wanaoamini kwamba mwanamke akianza kutumia njia za uzazi wa mpango anaweza kuwa mtu wa kutoka nje ya ndoa.

Hii ni tofauti na wanawake wengi waliohojiwa kwani wanaonesha kwamba wanatamani kufunga uzazi bali mazingira yanakuwa magumu.

Hii wanasema ni pamoja na kutopata ushirikiano kutoka kwa waume zao, elimu duni ya masuala ya afya ya uzazi na kutamalaki kwa mfumo dume ndio unaofanya wajikute wakizaa watoto wengi bila ridhaa yao. Ingawa mimba haikai kwa mwanaume, lakini uchunguzi anaonesha kwamba katika jamii yetu anayetakiwa kufanya maamuzi kuhusu watoto ni mwanaume.

Hilo limejidhihirisha pia kwa Theopista anaposema: “Kuna shirika moja lililikuja huku kijijini na kutuelimisha kuhusu uzazi wa mpango, nikamwambia mwanaume lakini alikasirika sana.

“Ukimwambia anakwambia sitaki uzazi wa mpango kwani wewe ndio unanunua chakula… Lakini ukweli ni kwamba chakula chenyewe ni cha kuhemea, watoto kuvaa kwenyewe shida, maisha ni magumu sana.”

Anaongeza: “Huku kwetu siku zote mwanaume hataki kuwa chini. Unatakiwa tu kumtii lakini yeye hajui unanyonyesha na unahitaji vyakula bora zaidi kwa ajili yako na mtoto kama walivyotufundisha watalaamu, hajui upo kwenye hali gani, yeye akija akikwambia geuka, unageuka kumpa haki yake, usipogeuka kipigo,” anasema.

Waganga wapotoshaji Marietha Mgambo mwenye watoto wanane anasema siku za nyuma walikuwa wakikimbilia kwa waganga wa kienyeji ili kupata dawa za kufunga uzazi, lakini matokeo yake walijikuta wakilaghaiwa na kupewa dawa ambazo hazikuzaa matunda.

“Unakuta unapewa hirizi uvae kiunoni na wanakuhakikishia kwamba mimba haitaingia, unavaa lakini unajikuta mimba inaingia. Mara nyingine unaambiwa ile damu ya hedhi uikamue uweke kwenye chupa, kisha ile chupa uifunge na kuiweka kwenye chungu kisha kichimbie chini. Utafanya vyote hivyo lakini mwisho wa siku mimba hiyo!” anasema.

Anasema mwanzo wanawake waliishi kama watumwa lakini kwa sasa mashirika yameingia na kuwaelimisha wanawake kwa wanaume. Kwa upande wa Flora aliyetaja jina moja pekee akigoma kutaja la pili anasema:

“Mimi mwenyewe nilikuwa nazaa bila mpangilio, walikuwa wakinielekeza nawaambia ni wanangu kumbe najipotosha mwenyewe, ulikuwa ukivaa dawa kiunoni unashangaa miezi miwili mitatu mimba tayari.”

Flora mwenye watoto wanane anasema alikuwa akizalia nyumbani akiwa haamini hospitali lakini mimba ya sita ilikaribia kumuua na ndipo akakaimbizwa hospitali ambako aliokolewa yeye na mtoto.

Pamoja na hayo hakukoma kutumia miti shamba aliiamini na kwamba mimba ya mwisho ndio ilikuwa hatari zaidi.

“Nilikuwa nikivuja maji. Kuna jirani yangu akaniambia niende kituo cha afya Bukondo, nilienda ikashindikana, akanipa usafiri kwenda Nansio kituo cha Wilaya, nilizoea kutumia mitishamba, sasa nikawa namwambia kama mitishamba imeshindikana hospitali itawezekana? Lakini hakuchoka, akanipeleka Nansio,” anasema.

Anasema baada ya siku tatu akajifungua mtoto ambaye alishaanza kuchoka sana.

“Nilikuwa namwagika sana maji kwa siku tatu mfululizo, lakini nashukuru baada ya kwenda hospitali kubwa ya wilaya niliweza kupata huduma na kujifungua salama,” anasema.

Licha ya kuwa tayari na waoto wanane Flora anasema sasa ameanza kutumia uzazi wa mpango na kwamba kimsingi hataki tena kuzaa.

Changamoto ya mitishamba

Mratibu wa afya mkoa wa Mwanza, Cecilia Mrema anasema changamoto ya matumizi ya mitishamba wakati wa kujifungua ni kubwa bado kutokana na watu kutaka kuharakisha uchungu na kujifungua haraka.

Anafafanua kwamba mitishamba hiyo wanayokunywa bila kipimo maalumu inasababisha watumaiji kuvuja damu nyingi wakati wa kujifungua.

“Wengi wanapoteza maisha, tunachofanya tunaenda kwenye msiba na tunaomba nafasi ya kuzungumza na waombolezaji hadharani tunasema wazi huyu kafariki kutokana na kutumia mzizi fulani wa kuongeza uchungu, mfuko umepasuka amepoteza damu nyingi.

“Tunaamini kwa kufanya hivi jamii itaelewa na kuacha matumizi ya mitishamba kuharakisha uchungu,” anasema Mrema anahimiza elimu zaidi iendelee kutolewa kwa wananchi, ili kupunguza vifo vya wajawazito na watoto.

“Mfano, ukiwaelimisha wanandoa umuhimu wa kwenda kliniki kuna vidonge vya kuongeza damu watapewa, watatumia na watafanikiwa kupunguza zile asilimia za kupoteza maisha wakati wa kujifungua,” anasema.

Wanataka kuzaa kwa mpango Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) katika ripoti yake ya mwaka 2019, theluthi mbili ya wanawake wenye uwezo wa kubeba mimba na ambao wana nia ya kuchelewesha kupata ujauzito au kudhibiti idadi ya watoto lakini huacha kutumia huduma za uzazi wa mpango kwa hofu ya madhara ya huduma hizo.

Hiyo ni kwa mujibu wa matokeo ya utafiti katika nchi 36. Shirika hilo linasema ingawa mimba zisizopangwa si lazima ziwe mimba zisizohitajika, bado zinaweza kusababisha madhara ya kiafya kwa mama na mtoto kama vile utapiamlo, magonjwa, ukatili, kupuuzwa na hata kifo.

“Mimba zisizopangwa zinaweza kusababisha pia kiwango kikubwa cha kuwa na watoto wengi, kiwango kidogo cha elimu, ukosefu wa ajira na umaskini, changamoto ambazo zinaweza kukumba kizazi na kizazi,” imesema taarifa hiyo ya WHO. Sera kuhusu uzazi bora Sera ya Idadi ya Watu ya Mwaka 2006, inatambua haja ya kuwaelimisha wanawake kuhusu manufaa ya uzazi wa mpango.

Pia Sera ya Taifa ya Afya ya Mwaka 2007 inasisitiza kuhusu dhamira ya serikali kushirikiana na sekta binafsi na washirika wa maendeleo kuendelea kutoa huduma za afya bure kwa wajawazito, watumiaji wa huduma za uzazi wa mpango na watoto wenye umri chini ya miaka mitano. Nchini Tanzania kiwango cha kuzuia mimba kwa njia za kisasa miongoni mwa wanawake walioolewa wakiwa na miaka 15 hadi 49 ni asilimia 32.9 Idadi ya wanawake waliokwishaolewa wenye umri kati ya miaka 15 na 49 ambao hawajapata huduma za uzazi wa mpango, wale wanaotaka kuzaa kwa mpangilio au kusitisha uzazi lakini hawatumii njia za kuzuia mimba ni asilimia 22, ikitofautiana kati ya mkoa na mkoa.

Kiwango cha vifo vya kina mama (MMR) nchini Tanzania, kama kilivyokadiriwa katika utafiti wa karibuni sana wa DHS wa mwaka 2015/16, ni watu 556 kwa kila vizazi hai 100,000.

Hii ina maana kwamba wanawake 11,000 hufa kila mwaka wakati wa ujauzito, kujifungua au katika kipindi cha siku 42 za kuharibika kwa mimba, bila ya kuzingatia chanzo.

Uzazi wa mpango unatoa mwanya wa kupunguza mimba zisizotarajiwa zinazochangia kuwaweka wanawake hususani mabinti wadogo katika hatari ya kutoa mimba na kujiweka kwenye hatari ya vifo.

Kimsingi, njia za kisasa za kupanga uzazi ni muhimu sana na zinapaswa kuhusisha wanandoa wote wawili, mwanamke na mwanaume. Pia wanawake hawapaswi kuzitumia vichochoroni bali kuwaona wataalamu ili kuwashauri watumie njia ipi. Baadhi ya dawa hizo ni vidonge vya kumeza vya homoni, kitanzi (IUD), kondomu ya kiume na ya kike, sindano na vipandikizi.

foto
Mwandishi: Vicky Kimaro

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi