loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Simba waondoka kibabe Mwanza

Wachezaji wa Simba SC wamewasili jijini Dar es Salaam baada ya kuondoka kanda ya Ziwa wakiwa na pointi sita kwa kushinda mechi mbili.

Simba jana iliifunga Alliance FC kwa mabao 4-1 katika mchezo uliochezwa Uwanja wa CCM, Kirumba Mwanza na kuzidi kujiimarisha kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Katika mchezo uliopita Simba iliifunga Mbao FC kwa mabao 2-1 mchezo uliochezwa katika uwanja huo Alhamisi iliyopita.

Katika mchezo huo, Alliance FC walianza kupata bao dakika ya 28 likifungwa na Israel Patrick kwa mpira wa moja kwa moja, nje ya eneo la penalti akipiga kwa ufundi baada ya kuangalia kipa wa Simba aliposimama.

Baada ya bao hilo, Simba walicharuka na kuanza kuliandama lango la Alliance FC na dakika ya 45 kiungo Jonas Mkude alisawazisha kwa shuti la nje ya eneo la penalti likiwa ni bao lake la pili katika ligi kuu kwa msimu huu.

Baada ya kutoka mapumziko, Simba ilizidi kuliandama lango la Alliance FC na dakika ya 58, Medie Kagere anafunga bao la pili kwa kichwa, likiwa ni bao la 11 katika msimu huu. Dakika ya 63, Clatous Chama alifunga bao la tatu, likiwa ni bao lake la pili kwa msimu huu na karamu ya mabao katika mchezo huo, ilihitimishwa na Hassan Dilunga baada ya kufunga bao la nne dakika ya 72 likiwa bao lake la nne kwa msimu huu.

Kwa matokeo hayo, Simba inazidi kuwa kileleni mwa ligi ikiwa na pointi 41 baada ya kucheza michezo 16, ikishinda michezo 13, kupata sare mbili na kufungwa mmoja wakati Alliance FC imecheza michezo 17, imeshinda mitano, sare tano na kufungwa michezo saba ikiwa inashika nafasi ya 13 ikiwa na pointi 20.

foto
Mwandishi: Rahel Pallangyo

Post your comments