loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Hakimu- Msipomleta Lissu tutatoa amri ngumu

WADHAMINI wa aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu wameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kuwa wamemwandikia barua Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ya kumuomba awasaidie kumleta mshitakiwa Lissu hapa nchini.

Hata hivyo, mahakama hiyo imesisitiza kuwa inamhitaji Lissu mahakamani hapo ili shauri linalomkabili yeye na wenzake wanne, liweze kuendelea katika hatua nyingine.

Mdhamini Robert Katula alidai jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba kuwa wamefanya juhudi za kuwasiliana na mshitakiwa na mara ya mwisho aliwaeleza kuwa anawasiliana na wakili wa chama chake.

Alidai kuwa baada ya kuwaeleza hayo, mpaka sasa hawajafanikiwa kupata jibu lolote, ndipo walipoamua kumuandika barua Mbowe ili awasaidie kumleta mshitakiwa huyo nchini ili waweze kumfikisha mahakamani.

Alidai wakati walipomdhamini Lissu, hawakujua kama atapigwa risasi na kuondoka nchini, hivyo waliomba muda zaidi wa kufuatilia majibu ya barua hiyo.

Wakili wa Serikali, Sylvia Mitanto alidai kuwa jukumu la kuhakikisha mshitakiwa huyo, anafika mahakamani ni la wadhamini wenyewe na si la mtu mwingine. Alidai wadhamini hao, walikubali kumuwekea dhamana mshitakiwa huyo, hata kabla ya kuugua na waliridhia asafiri.

Aliongeza kuwa walikuwa wana jukumu la kujitoa katika nafasi hiyo kabla Lissu hajasafiri. Baada ya kueleza hayo, Hakimu Simba alisema suala bado linabaki palepale kuwa mshitakiwa huyo aletwe mahakamani, kwani kupigwa kwake risasi hakumzuii kufika.

“Tunaomba mtuletee mshitakiwa hapa, tena (mdhamini) usije ukafikiri tutakusamehe, tunakupa muda mwingine tuletee mtu huyo kabla hatujatoa amri nyingine itakayokuwa ngumu zaidi dhidi yenu wadhamini na mshitakiwa mwenyewe,” alisema Hakimu Simba.

Hakimu Simba aliahirisha kesi hiyo hadi Februari 20, 2020. Alisisitiza kuwa Lissu afikishwe mahakamani na kwamba dhamana kwa washitakiwa wengine inaendelea.

Mbali na Lissu, washitakiwa wengine ni Mkina, Mhariri wa gazeti la Mawio, Jabir Idrisa na Mchapishaji wa Kampuni ya Jamana, Ismail Mehboob. Lissu na wenzake wanakabiliwa na mashitaka matano, ikiwemo la kuandika habari za uchochezi kinyume na Sheria ya Magazeti ya Mwaka 2002.

Inadaiwa kuwa Januari 12 hadi 14, 2016 katika jiji la Dar es Salaam, washitakiwa watatu, Jabir, Mkina na Lissu, kwa pamoja waliandika na kuchapisha taarifa za uchochezi zenye kichwa cha habari kisemacho, ‘Machafuko yaja Zanzibar’.

Katika mashitaka ya pili, wanadaiwa kuwa Januari 14, 2016 katika jiji la Dar es Salaam, walichapisha habari hizo ili kuleta chuki kwa wananchi wa Zanzibar.

Mshitakiwa Mehboob anadaiwa kuwa Januari 13,2016 katika jengo la Jamana lililopo Manispaa ya Ilala, Dar es Salaam, alichapisha gazeti la Mawio lililokuwa na taarifa za uchochezi.

Inadaiwa mshitakiwa huyo pia alichapisha gazeti hilo bila ya kuwasilisha hati ya sheria ya kiapo kwa Msajili wa Magazeti.

Mbali na mashitaka hayo, washitakiwa hao kwa pamoja wanadaiwa kuwa Januari 14, 2016, Dar es Salaam, bila ya kuwa na mamlaka yoyote, waliwatisha na kuwatia hofu wananchi wa Zanzibar wasiweze kuingia kwenye marudio ya Uchaguzi Mkuu.

foto
Mwandishi: Francisca Emmanuel

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi