loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Tabibu ampasua mgonjwa, aacha utumbo nje

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Rukwa inamshikilia tabibu msaidizi, Eliud Humbo aliyemfanyia upasuaji mgonjwa kinyume na taratibu ili apewe rushwa ya Sh 100,000.

Upasuaji huo usio wa kawaida ulifanyika katika Kituo cha Afya Matai wilayani Kalambo huku ikielezwa kwamba tabibu huyo msaidizi hana utaalamu wa upasuaji wa aina yoyote ile kwa bindamu.

Humbo alimpasua tumbo mgonjwa huyo na kuuacha utumbo wake nje na kumsababishia maumivu makali.

Mgonjwa huyo alikuwa na rufaa ya kwenda Hospitali ya Mkoa iliyopo katika Mji wa Sumbawanga.

Hayo yalibainishwa na Mkuu wa Takukuru, Mkoa wa Rukwa, Hamza Mwenda kwa wanahabari mjini hapa wakati akitoa taarifa ya utendaji wa kazi wa Oktoba hadi Desemba 2019/20.

"Awali mgonjwa huyo alibainika kusumbuliwa na ugonjwa wa ngiri na madaktari walimpatia rufaa kwenda kutibwa katika Hospitali ya Mkoa wa Rukwa iliyopo katika Mji wa Sumbawanga,’’ alisema.

Wakati akijiandaa kutoka katika Kituo cha Afya Matai ili akatibiwe mjini Sumbawanga alikutana na Humbo ambaye alimhakikishia kuwa ana uwezo wa kumfanyia upasuaji na atapona.

Baada ya mtuhumiwa kupokea fedha hizo kutoka kwa mgonjwa huyo, alikwenda kwa Msimamizi wa Kitengo cha Tohara kwa wanaume akidai ana mgonjwa aliyekuwa akihitaji kutahiriwa.

"Mtuhumiwa huyo alikabidhiwa vifaa vilivyohitajika kwa kumfanyia tohara mgonjwa wake, lakini alimfanyia upasuaji wa ngiri kwa kumpasua tumbo lake,’’ alisema.

Baada ya kufanyiwa upasuaji huo alilazwa wodini ambapo siku iliyofuata kidonda kilianza kuoza huku utumbo wake ukiwa nje na hali yake ilibadilika ghafla na kuwa tete. Ilidaiwa kuwa daktari wa zamu alipomhoji juu ya ugonjwa wake unaoendelea kumsumbua ndipo siri ilipofichuka na taarifa tukafikishiwa Takukuru.

“Tumemkamata mtuhumiwa huyo na tayari tumemfikisha mahakamani, amefunguliwa kesi kwa kuomba na kupokea rushwa,"alisisitiza. Alisema mgonjwa huyo alikimbizwa katika Hospitali ya Mkoa wa Rukwa mjini kwa matibabu zaidi na hali yake inaendelea kuimarika.

MGOMBEA ubunge kwa tiketi ...

foto
Mwandishi: Peti Siyame, Sumbawanga

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi