loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

STAMICO kuanzisha mradi wa kusafisha dhahabu Mwanza

SHIRIKA la Madini la Taifa (STAMICO) lipo katika hatua za awali za uanzishwaji wa Mradi wa Kusafisha Dhahabu (Gold Refinery) na tayari kampuni ya ubia ijulikanayo kama Mwanza Precious Metals Refinery Company Limited imeanzishwa, Imeelezwa.

Hayo yamebainishwa jana na Kaimu Mtendaji Mkuu wa Stamico, Dk Venance Mwase wakati  akiwasilisha kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini taarifa  kuhusu utekelezaji na hali ya upatikanaji wa fedha za maendeleo ya shirika hilo kwa kipindi cha nusu mwaka wa 2019/20.

Dk Mwase alieleza kamati hiyo kuwa mradi huo utaendeshwa kwa ubia ambapo Stamico itakuwa  na hisa asilimia 25 na mwekezaji asilimia 75, huku ikilelezwa kwamba, mradi huo  utakaojengwa jijini Mwanza utahusisha ujenzi wa mtambo wenye uwezo wa kusafisha wastani wa kilogramu 200 hadi 500 kwa siku.

Aliongeza kuwa, makadirio ya fedha zinazohitajika ni dola la kimarekani milioni 58.204 ambazo zimepangwa kwa ajili ya ununuzi wa mtambo wa kusafishia dhahabu, gharama za awali za mradi, kununua dhahabu kutoka katika masoko pamoja na gharama za uendeshaji na kuongeza.

Aidha, Dk Mwase alisema kwamba katika kipindi cha Julai hadi Desemba, 2019, tayari mradi umetekeleza majukumu kadhaa ikiwemo kupata leseni ya kujenga na kuendesha mtambo huo, kusainiwa mkataba wa ubia pamoja na kuanza taratibu za uanzishwaji wa kampuni ya ubia na kupata eneo la ujenzi wa mtambo chini Mamlaka ya Ukanda Maalum ya Uwekezani nchini.

Pia alisema majukumu mengine yaliyotekelezwa ni pamoja na kufanyika kwa Athari kwa Mazingira (EIA) kwenye eneo la mradi upembuzi yakinifu pamoja na kukusanya taarifa za upatikanaji wa dhahabu katika maeneo mbalimbali yanayokusudiwa.

Kuhusu Mgodi wa Stamigold ambao ni Kampuni Tanzu ya Shirika hilo ameieleza kamati hiyo kuwa, kuanzia Julai hadi Desemba, 2019, mgodi huo umezalisha na kuuza wakia 7,133.00 za madini ya dhahabu na wakia 879.19 za madini ya fedha, vyote vikiwa na thamani ya Sh bilioni 24.17.

"Mhehimiwa Mwenyekiti, katika kipindi hicho, mgodi umelipa jumla ya shilingi bilioni 1.7 kwa ajili ya malipo ya mrabaha, ada ya ukaguzi na kibali cha kusafirisha madini nje ya nchi,’’ alieleza Dk  Venance.

Kuhusu mradi wa makaa ya mawe katika Mradi wa Kabulo na Kiwira, alisema jumla ya tani 4,359.10 ziliuzwa na kulipatia Shirika Sh milioni 17.55 na kuongeza kuwa, ‘’Shirika lilifanikiwa kulipa mrabaha, ada ya ukaguzi na tozo ya Halmashauri ya jumla ya shilingi milioni 23.64.”

Kwa upande wake, Waziri wa Madini Doto Biteko wakati akitoa ufafanuzi wa hoja zilizoibuliwa na kamati, aliwatoa hofu wajumbe wa kamati hiyo kuhusu maendeleo ya Stamico ambapo alieleza pamoja na changamoto zinazolikabili, linakua na linafanya vizuri.

Waziri Biteko aliiomba kamati hiyo kuendelea kuilea na kuishauri Stamico kwa kuwa mwelekeo wake ni mzuri na kwamba hivi sasa lina uwezo wa kuzalisha hadi Sh bilioni 20 tofauti na ilivyokuwa awali.

‘’Mheshimiwa Mwenyekiti, itakuwa bahati mbaya sana kulifuta shirika hili. Linakua, wanaendelea vizuri na wana bodi nzuri, watendaji wanasikiliza ushauri na kuufanyia kazi na mapungufu yanafanyiwa kazi, naomba muendelee kuilea na kuishauri Stamico,’’ alisisitiza Waziri Biteko.

MGOMBEA Urais wa Chama ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi