loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Samatta apongezwa kila kona

SERIKALI imempongeza na wadau mbalimbali wa soka wamempongeza mshambuliaji wa Kimataifa wa Tanzania, Mbwana Samatta baada ya kusaini mkataba wa miaka minne na nusu kuichezea klabu ya Aston Villa inayoshiriki Ligi Kuu ya England na kuwaomba Watanzania kumuombea ili afanikiwe zaidi.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Waziri wa Habai, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe akisema serikali imefurahi kama Watanzania wote walivyofurahi na kumpongeza Samatta kwa juhudi zake kwani hajabahatisha ila kwa nidhamu ya hali ya juu inawakwamisha vijana wengi wa Kitanzania.

“Hakika serikali imefurahi kama Watanzania walivyofurahi, tunampongeza Samatta kwa juhudi zake, najua hakubahatisha ila kwa nidhamu yake ya hali ya juu ndio imemfikisha hapo, kitu ambacho kinawakwamisha vijana wengi wa Kitanzania,” alisema Dk Mwakyembe.

Pia aliwataka Watanzania kumwombea Samatta ili afanye vizuri kwanza, kwani alipofikia sio kilele cha mafanikio kuliko kukimbilia na kusema ajengewe sanamu “Watu wasikimbilie masuala ya sanamu, tumuombee afanye vizuri kwanza, hata tukijenga sanamu lakini asipofanya vizuri Aston Villa haitaleta maana, alipofika Samatta sio kilele cha mafanikio tunataka awe Messi wa Dunia nyingine,” alisema Mwakyembe.

Baada ya kusaini mkataba wa miaka minne na nusu kuchezea timu hiyo yenye maskani yake Birmingham, Samatta aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kuwa ilikuwa ndoto, lakini Aston Villa imeifanya iwe kweli.

“Yote ilikuwa ndoto, asante @avfcofficial kuifanya iwe kweli, Sasa ni wakati wa kutoa 100% kwa timu yangu,”.

Aliandika Samatta anayetumia @Samagoal77_. Mbali na pongezi za serikali pia Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilimtakia kila la heri nahodha huyo wa Taifa Stars katika timu yake mpya ya Aston Villa na kusema wana imani ataendelea kufungua milango kwa wachezaji wengine wa kitanzania katika mpira wa miguu.

“Hatua hiyo sio kuwa itamsaidia yeye tu bali itasaidia pia katika timu ya Taifa pale atakaporudi kuitumikia pia tunaamini kauli mbiu yake ya haina kufeli ataendelea kuipigania na kufikia lengo,” alisema Ndimbo.

Pia alisema wanamtakia heri katika majukumu yake mapya Aston Villa na kuendelea kuipeperusha vema bendera ya Taifa la Tanzania. Katika upande mwingine watu mbalimbali na taasisi zimempongeza kwa hatua aliyofikia na kutoa maoni kwa serikali.

Mohammed Samatta ambaye ni kaka Samatta, amesema kutokana na hatua aliyopiga mdogo wake kwenye soka, kama atapewa heshima ya kujengewa sanamu au mtaa kupewa jina lake, atakuwa amestahili.

Victor Wanyama wa Kenya anayecheza Tottenham Spurs ya England aliandika katika ukurasa wake wa Twitter:”

Hongera sasa kaka Samatta na karibu kwenye premier league nakutakia kila lenye heri unapoanza maisha mapya.

Klabu ya Simba nayo ilimpongeza ”Hongera sana Mbwana Samatta kwa hatua kubwa, ambayo umepiga kwenye maisha yako ya soka. Wanasimba tunakutakia kila la heri kwenye timu yako mpya ya Aston Villa. NguvuMoja,”

Nayo klabu ya Yanga imempongeza Samatta kwa kuwa balozi mzuri wa soka la Tanzania na kumtakia heri katika majukumu yake hayo mapya katika klabu hiyo. Pia mshambuliaji Emanuel Okwi alimpongeza Samatta pamoja na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimempongeza kwa kufanikiwa kuwa mchezaji wa kwanza kutoka Tanzania kucheza Ligi Kuu England kwa mkataba wa miaka minne na nusu.

“Chadema inamtakia kila la heri Samatta ili mafanikio yake ya kucheza kwenye mojawapo ya Ligi kubwa duniani yawe chachu na hamasa kubwa ya kuongeza mori na bidii ya kusonga mbele zaidi, kwake yeye na wachezaji wa Kitanzania, wanaocheza ndani na nje ya nchi yetu.”

“Tunatoa wito kwa serikali kuitumia milango ambayo itakuwa imefunguka au fursa zilizotengenezwa kupitia Samatta kusajiliwa na Aston Villa,” ilisema Chadema.

Samatta amesajiliwa na Aston Villa kwa mkataba wa miaka minne na nusu na ataitumikia klabu hiyo hadi Juni, 2024 kwa ada ya Pauni milioni 8.5 na baada ya kutambulishwa alisema kwake ina maana kubwa kwani Tanzania wanapenda kuangalia ligi kuu ya England.

“Kwangu mimi ina maana kubwa sana, nchini Tanzania watu wanapenda soka na wanapenda kuangalia Premier League. Itakuwa ni kipindi ambacho Watanzania wanakwenda kumuangalia mchezaji wao akiichezea Aston Villa”, alisema Samatta katika mahojiano yake ya kwanza na mtandao wa klabu hiyo. Samatta akiwa KRC Genk ya Ubelgiji, alicheza mechi 191 akifunga mabao 76 na kutoa ‘assist’ 20.

Watanzania watarajie kumwona Samatta kuanzia wikiendi hii katika michezo ifuatayo ya Ligi Kuu ya England, Aston Villa dhidi ya Watford, Leicester City, Bournemouth, Tottenham Hotspurs , Southampton, Sheffield United, Chelsea, Newcastle United, Wolverhampton na Liverpool.

Aston Villa inashika nafasi ya 18 katika msimamo wa Ligi Kuu ya England ikiwa imeshinda mechi sita, imefungwa mechi 13 na sare nne, na inapigania kutoshuka daraja.

MWIGIZAJI maarufu wa tamthilia ya Karma, Wema Sepetu amewaomba radhi ...

foto
Mwandishi: Waandishi Wetu

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi