loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Takukuru yaokoa bil. 4/-ufisadi Ushirika

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imeokoa zaidi ya Sh bilioni nne za awamu ya kwanza ya Sh bilioni 51.7, zilizochunguzwa zenye viashiria vya ubadhirifu wa fedha, mali na rushwa katika vyama vya ushirika nchini na wahusika kadhaa wamechukuliwa hatua za kisheria.

Aidha pamoja na mafanikio hayo ya mwezi mmoja na nusu wa uchunguzi, mikoa 11 kati ya 28 ya kiuchunguzi ya Takukuru, ikiwamo Kinondoni, Ilala na Dodoma, imeshindwa kurejesha fedha yoyote mpaka sasa na imepewa onyo.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, John Mbungo, aliyasema hayo jana Dar es Salaam, alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu matokeo ya uchunguzi wa Ripoti ya Ukaguzi wa Ubadhirifu wa Vyama vya Ushirika ya mwaka 2018/2019 iliyotolewa na Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga, Novemba 26 mwaka jana.

Aidha kwa mujibu wa taarifa ya ukaguzi ya Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO) na kukabidhiwa kwa Takukuru, vyama vilivyofanyiwa ukaguzi ni 4,413 vikiwamo vyama vikuu (Union) 38, vyama vya mazao (AMCOS) 2,710, vyama vya Akiba na Mikopo (Saccos) 1,488 na vyama vinginevyo 217.

“Kwa mujibu wa muhtasari wa taarifa iliyokabidhiwa Takukuru, jumla ya fedha iliyokuwa na viashiria vya ubadhilifu wa fedha na mali pamoja na rushwa ni 124,053,250,874, Uchunguzi wa awamu ya kwanza uliofanywa na Takukuru mpaka sasa umefanikiwa kuchunguza Sh 51,794,221,683.09 wakati uchunguzi wa Sh 72,259,029,190.91 unaendelea,” alisema.

Mbungo alisema katika ufuatiliaji huo, Takukuru imefanikiwa kuokoa Sh 4,066,162,092.38, fedha ambazo baadhi zimerejeshwa kwa wakulima na vyama vya ushirika ama kutunzwa katika akaunti maalumu zilizofunguliwa kwa ushauri wa warajisi wa vyama vya ushirika na wakuu wa mikoa na wilaya, kwa ajili ya kuzirejesha kwenye vyama vya ushirika au wakulima.

Hata hivyo akijibu maswali ya waandishi, Mbungo alisema matamanio ya Takukuru si kuhifadhi fedha zinazorudishwa katika akaunti, bali ni kuwafikia wakulima waliokuwa wakidai pamoja na vyama vya ushirika.

Mbungo alisema katika awamu ya kwanza iliyochunguza Sh bilioni 51.7 na kufanikiwa kuokoa Sh bilioni nne, mikoa 11 haijarejesha fedha yoyote mpaka sasa na imetakiwa kuhakikisha wadaiwa wanarejesha kabla ya hatua kali kuchukuliwa.

Mikoa hiyo na fedha zinazochunguzwa kwenye mabano ni Kinondoni (Sh 5,509,490,727), Ilala (Sh 3,752,744,920), Singida (Sh 132,599,880), Kigoma (Sh 208,803,214.99), Shinyanga (Sh 1,478,633,215), Mwanza (Sh 4,613,127,930), Geita (Sh 26,291,447), Rukwa (Sh 595,321,710), Morogoro (Sh 198,600,359) na Dodoma (Sh 1,854,301,158).

Mikoa ambayo fedha imeokolewa na bado inadaiwa ni Ruvuma, Kilimanjaro, Manyara, Katavi, Pwani, Mbeya, Iringa, Simiyu, Arusha, Lindi, Njombe, Tanga, Tabora, Mara, Temeke, Songwe na Mtwara.

Mbungo alisema baadhi ya wahusika, waliobainika katika ubadhirifu wamefikishwa mahakamani na wengine wanaendelea kuhojiwa na kuchunguzwa na taasisi hiyo ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao.

“Haijalishi unarudisha fedha au haurudishi, Takukuru inachukua hatua za kisheria kwa wahusika wote. Lakini hatuwezi kuwataja hapa kwa sababu za kiusalama. Huwezi kuuza siri kwa maadui, ila kwa kweli hatua zinachukuliwa na niwaombe wenye fedha za wakulima, iwe mfanyabaishara, chama au taasisi, arudishe mara moja,”alisisitiza.

Alisema wakati hatua za kuokoa fedha zikiendelea katika awamu ya kwanza, awamu ya pili ya uchunguzi wa Sh bilioni 72.259 kiasi ambacho ni sehemu ya Sh bilioni 124 kilichobainishwa katika taarifa ya Waziri Hasunga, unaendelea.

“Hatua kali dhidi ya wote watakaokaidi agizo la kurejesha fedha walizochukua zitachukuliwa kwa mujibu wa sheria ikiwa ni pamoja na kutaifisha mali zao kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Mashitaka,” alisema.

Mbungo alimshukuru Rais Dk John Magufuli kwa kuwapa fedha, zinazowawezesha kuendesha operesheni hiyo. Aliwaomba wananchi waendelee kushirikiana na Takukuru, kutoa taarifa ya watu wanaojihusisha na rushwa kwa namba ya simu ya dharura 113, ambayo ni bure au kutumia Takukuru Application kutuma sauti, picha na video.

Novemba 26 mwaka jana, Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga aliikabidhi Takukuru Ripoti ya Ukaguzi wa Vyama vya Ushirika ya Mwaka 2018/2019, iliyofanywa na COASCO kwa vyama vyote vya ushirika nchini ili kuchunguza ubadhirifu na rushwa katika matumizi ya fedha za ushirika nchini.

Katika ukaguzi wa COASCO, walibaini kuwa hadi kufikia Juni 30, 2019 vyama vya ushirika vilivyosajiliwa vilikuwa 11,410 na kati ya vyama hivyo, vyama hai ni 6,463, vyama sinzia ni 2,844 na vyama visivyopatikana au kujulikana vilipo ni 2,103.

MGOMBEA Urais wa Chama ...

foto
Mwandishi: Gloria Tesha

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi