loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Shahidi augusa kortini wimbo maarufu wa ‘Harambee’ wa CCM

MEYA wa Ubungo, Boniface Jacob ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa wimbo unaotumiwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) wakati wa kampeni, unalenga kuwahamasisha wananchi kuwanyima kura wapinzani.

Jacob ambaye ni shahidi wa 10 wa upande wa utetezi, alidai hayo jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba wakati kesi ya uchochezi, inayowakabili vigogo tisa wa Chadema, ilipokuja kwa ajili ya kusikilizwa.

Akiongozwa na Wakili wa Utetezi, Peter Kibatala, Jacob alidai kichinjio kama ilivyoainishwa kwenye mashitaka ni kitambulisho cha kupigia kura, ambacho hutumika kwenye uchaguzi mbalimbali.

Aliutaja wimbo huo “Harambeee, Harambeee mama harambeee wapinzani tuwalete, tuwachane chane tuwatupe, CCM tuwalete tuwakumbatie tuwabusu,”.

Alidai wimbo huo ulitungwa na marehemu Kapteni John Komba na kuimbwa na bendi ya Tanzana One Theatre (TOT) na kwamba chama hicho kinapofanya mikutano yake, huimbwa vizuri.

Baada ya kudai hayo, Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi alipinga swali kuhusu wimbo huo alilouliza Kibatala, aliyehoji maana ya wimbo huo. Lakini, baadaye Hakimu aliruhusu kuulizwa, ndipo shahidi huyo alidai wimbo huo unamaanisha kuwanyima kura wapinzani.

Katika ushahidi wake, Jacob alidai Februari 16,2018 majira ya saa 4:00 au 5:00 asubuhi Mkurugenzi wa Kinondoni, Aron Kagurumjuli alikula kiapo kuwa Wakala Mkuu wa Uchaguzi kwa Chadema na kwamba ndiye alikuwa mshehereshaji kwenye mkutano wa kufunga kampeni wa chama hicho, uliofanyika Viwanja vya Buibui Mwananyamala, Dar es Salaam.

Alidai wazungumzaji wakuu katika mkutano huo, alikuwa Mbowe aliyezungumza kwa dakika 30 kuhamasisha watu kujitokeza kupiga kura pamoja na mgombea wa ubunge kwenye uchaguzi mdogo, Salum Mwalimu ambaye alizungumza kwa dakika 20 ,akiomba kura na kueleza kwa nini ana nia ya kuongoza jimbo hilo.

TAKWIMU za udumavu ...

foto
Mwandishi: Francisca Emmanuel

Post your comments