loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Mnada Msalato wamchefua Waziri, agoma kuufungua

WAZIRI wa Nchi, Ofi si ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, George Simbachawene amekataa kufungua machinjio ya mnada wa Msalato ambayo yalifungwa mwaka jana kutokana na kuwa katika hali mbaya.

Akizungumza mara baada ya kufika kwenye machinjio hayo ambayo yalifungwa kutokana na kutokuwa na mazingira ya kuridhisha ya usafi Oktoba 31 mwaka jana, Simbachawene alisema hawezi kufungua machinjio hayo kutokana na ukarabati wake ukiwa hauna viwango.

“Hili sio jengo la serikali, la mtu mmoja tu mlalahoi anaweza kujengajenga tu, lakini sio viwango vya majengo ya serikali, Hapa nikiuliza fedha zilizotumika ni shilingi ngapi, mtataja kiwango cha ajabu, mmetumia kiasi gani kufanya ukarabati,”alisema.

Mchumi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Shaban Juma alisema ukarabati huo umegharimu Sh milioni 22.

Simbachwene alipoomba maofisa wa Jiji wampatie ripoti ya ukarabati na kujibiwa kuwa kuna ofisa anakuja nayo, kauli hiyo ilimfanya waziri huyo kusema: “Ninyi hamjajiandaa, jengo lenyewe la hovyo, ripoti haipo, mnanileta mimi hapa waziri niangalie niwaruhusu muendelee na shughuli, lakini nikiangalia hapa ni kitu cha hovyo.

“Kwa hiyo sifungui hii machinjio mpaka mmalizie viporo vyote vilivyobakia kwa sababu unaponisomea taarifa za mradi lazima unisomee mpaka gharama zilizotumika, unioneshe pungufu uliopo na kazi zilizofanyika na waliosimamia niwe nawaona, “Hiyo tarazo ni uchafu mtupu, umaliziaji sio mzuri, pale kwa kuoshea pachafu, huwezi kuweka tiles imevunjia, kila kitu ni cha ovyo ovyo tu.

Hili tangi liko chini hapa, mnataka nifungue tangi halina maji na mmesema yatakuwa mawili naona moja tu.” “Ofisa mifugo yupo, ofisa mazingira yupo, mchumi yupo, lakini mnapitisha kitu cha ovyo kama hiki, mimi siwezi kufungua, nikifanya hivyo ni kuhalalisha wananchi kula uchafu.” Kutokana na hali hiyo, Simbachawene alitoa wiki moja kwa uongozi wa Halmashauri ya Jiji kumalizia kazi zilizobaki.

Baada ya waziri kuondoka, maofisa wa jiji walionekana wakilaumiana. Ofisa wa Mifugo mjini Dodoma, Gration Mwesiga alisema kwa kifupi: “ Tumepokea maelekezo ya Waziri.”

Diwani wa kata ya Msalato, Ally Mohamed alisema amepokea uamuzi wa waziri kwa uchungu kwani wananchi wake wataendelea kuteseka. Naye mmoja wa wachinjaji katika machinjio hiyo, Emmanuel Danny alisema hatua ya kutofunguliwa kwa machinjio hayo kunawarudisha nyuma vijana waliokuwa wakipata kipato.

Oktoba 31 mwaka jana, Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira Tanzania (Nemc) lilifunga machinjio ya Msalato na kuitoza Halmashauri ya Jiji la Dodoma faini ya Sh milioni tano. Hatua hiyo imechukuliwa baada ya kamati ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira kufanya ziara katika machinjio hiyo.

foto
Mwandishi: Anastazia Anyimike

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi