loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Tanesco yaokoa bilioni 24/- kuacha mitambo ya mafuta

SHIRIKA la Umeme nchini (Tanesco) limesema limefanikiwa kuokoa Sh bilioni 23.5 ambazo zilikuwa zikitumika kila mwaka kwa ajili ya kuendeshea mitambo ya umeme kwa kutumia mafuta baada ya kuachana na mitambo hiyo.

Pia shirika hilo limeongeza ukusanyaji wa mapato hadi kufikia Sh trilioni 1.53.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Dk Tito Mwinuka alisema fedha hizo zilikuwa zinatumika katika uendeshaji wa mitambo ya kufua umeme katika vituo mbalimbali hapa nchini ambavyo vimezimwa baada ya maeneo hayo kufikiwa na gridi.

Dk Mwinuka alivitaja vituo ambavyo vimezimwa mitambo yake ni pamoja na Tunduru, Mtwara, Namtumbo, Songea, Madaba, Ruvuma,na Liwale.

“Tunashukuru sasa hivi tumefanikiwa kuokoa kiasi hicho cha fedha tokea mwaka 2018, na tunaamini tutazidi kupiga hatua kwa hii miradi tunayoifanya,”alisema Dk Mwinuka.

Alisema kupitia miradi mbalimbali hali ya fedha ya shirika hilo imeboreka na wanaendesha shirika bila kupata ruzuku na wanamudu kuwalipa watoa huduma wengi.

Aidha alisema mchango wa wazalishaji binafsi wa umeme nao umekuwa ukithaminiwa ambapo asilimia ya serikali ni asilimia 86.5 huku asilimia 13.5 ni mchango wa sekta binafsi kwenye gridi ya taifa.

Alisema mafanikio mengine makubwa yamepatikana katika ufuaji wa umeme, ununuzi, usafirishaji pamoja na eneo la uwekezaji ambalo nalo limechangia kwa kiasi kikubwa katika mafanikio ambayo yamepatikana ndani ya miaka hiyo minne.

Alisema kupungua kwa vituo vya kufua umeme kwa kutumia mafuta,kumetokana na uwekezaji ambao wameufanya kwenye sekta ya umeme.

Akizungumzia changamoto za umeme jijini Dar es Salaam amesema shirika lake limefanikiwa kuboresha kituo cha ubungo cha kupooza umeme kwa kufunga transfoma mpya ambayo ina uwezo wa kufanya kazi katika maeneo mbalimbali tofauti na ilivyokuwa awali.

Aidha alisema Mwaka 2015 mita zilizofungwa nchini zilifikia 1,648 386 na hadi kufikia mwaka 2019 mita zilizofungwa ni 2,700,682 sawa na ongezeko la asilimia 63.4 ikiwa ni ongezeko la mita milioni 1.05.

Alisema uboreshwaji wa kituo cha Ubungo kumetokana na mahitaji ya jiji hilo muhimu kwa biashara na viwanda. Alisema wataalamu wa ndani wamesaidia kuliimarisha shirika hilo kwa kusaidia kuwezesha kupatikana kwa umeme wa 132,kv.

“Hivi karibuni tumeboresha kituo cha Ubungo,kutokana na mahitaji ya Jijini kuwa makubwa na kusababisha kituo kuzidiwa na megawati 240,hii imesaidia kutatua tatizo la umeme,”alisema Dk Mwinuka.

Alitaja mafanikio mengine ni kushuka kwa gharama za umeme mwaka 2016 ambapo serikali ilishusha gharama za umeme.

BEKI  wa zamani wa ...

foto
Mwandishi: Sifa Lubasi

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi