loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

TCRA endeleeni kuzima laini za simu kwa utalaamu

MAENDELEO ya sekta ya mawasiliano, yamesababisha watu wengi kuwa watumiaji wa laini za simu za mkononi. Jambo hili ni zuri, lakini pia lina changamoto zake na hizo ni matatizo ya kiusalama, udanganyifu na wizi.

Kutokana na changamoto hizo na nyinginezo, ndiyo maana serikali iliamua mwaka jana laini zote zisajaliwe upya kwa kutumia Kitambulisho cha Taifa na alama za vidole, ili kumjua kila mtumiaji wa laini ya simu.

Hivyo, tunaipongeza Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa kuanza kuzima laini za simu, ambazo hazijasajiliwa kwa alama za vidole.

Pia, tunashukuru maelezo mazuri yaliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, James Kilaba katika taarifa yake juzi, kuwa watatekeleza jukumu hilo kwa awamu na kwamba watatumia ustaarabu na utalaamu, ili kuwafanya wamiliki wa laini hizo, kurudi kuhuisha laini zao.

Kwamba wanafanya hivyo ili kuiwezesha mifumo ya Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) isizidiwe, endapo laini nyingi zitafungwa kwa wakati mmoja.

Kilaba anaeleza kuwa laini ambazo hazijakamilisha usajili, zitazimwa pole pole kwa sababu kitaalamu hawawezi kuzima laini milioni tano au milioni kumi kwa mara moja, kwa kuwa mifumo ya NIDA haitaweza kuhimili kuhudumia idadi kubwa ya watu kwa wakati mmoja.

Tayari watu 975,000 ambao tayari wana Vitambulisho vya Taifa na hawajasajili laini zao kwa alama za vidole, walizimiwa laini zao juzi saa 6:00 usiku.

Kundi lingine ni wale ambao walisajili laini zao mwanzoni, kwa kutumia Kitambulisho cha Taifa lakini siyo kwa alama za vidole, ambao idadi yao ni 318,950.

Watu hao walitakiwa kurudi kuhuisha usajili wao kwa alama za vidole, lakini hawakufanya hivyo. Hao nao laini zao zimezimwa. Kilaba anasema lengo la TCRA, siyo kumnyang’anya mtu laini yake, ambayo ameizoea na kuipenda.

Bali, inachofanya ni kuisitisha laini kutoa na kupokea huduma ili mmiliki aihuishe. Pia, kwa namna ya kipekee tunalipongeza Jeshi la Polisi kwa taarifa yake juzi kwa wananchi kuhusu usajili wa simu.

Taarifa hiyo ya Polisi ilisema kwamba usikubali kumsajilia mtu laini yake kwa jina lako, hata kama mtu huyo ni wa karibu sana, kama baba, mama, dada na kaka.

Kwamba kumbuka namba yako imesajiliwa kwa jina lako, hivyo kama tukio lolote kihalifu litatokea na namba yako ya simu kuonekana, moja kwa moja unakuwa mtuhumiwa namba moja.

Watu wengi wamepewa kesi za mauaji au wizi bila kujua. Hivyo, Polisi wapo kazini na wanapoona vidhibiti, wanachukua na hawatajua kama umehusika au hujahusika. Usinunue simu kwa mtu usiyemjua.

Hiyo ni hatari, kwani hujui hiyo simu imetolewa wapi? Inawezekana ukapewa kesi ya wizi au mauaji endapo simu hiyo ilikuwa imeibiwa kwa mtu aliyeuawa. Hivyo, chukua tahadhari unaponunua simu.

SHIRIKISHO la soka Tanzania (TFF), Jumanne ya wiki hii lilizindua ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi