loader
Dstv Habarileo  Mobile
Picha

Nala kuwa eneo rasmi la wajasiriamali wa viwanda

MKURUGENZI wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Godwini Kunambi amesema halmashauri yake imetenga eneo la Nala, kama eneo litakalotumika na wajasiriamali ambao wanafanya shughuli zinazoendana na viwanda.

Kunambi aliyasema hayo wakati wa kujibu hoja za wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) walipotembelea kikundi cha Youth Entrepreneur cha Nzuguni kinachojishughulisha na utengenezaji wa majiko.

Alisema uongozi wa Halmashauri ya jiji la Dodoma umetenga eneo la Nala kuwa la viwanda na kuwa wajasiriamali ambalo wanafanya shughuli zinazoendana na viwanda watapelekwa huko.

“Kwenye soko kuu la Ndugai tumetenga eneo la wajasiriamali wanaofanya shughuli zingine ambazo haziendani na viwanda, lakini kama hawa ambao shughuli zao ziko kiviwanda tunawapeleka Nala ambako tumetengea eneo hilo.

“Tuko katika mipango ya kuweka mazingira mazuri kwa ajili ya wafanyabiashara na tukishakamilisha kupeleka miundombinu ikiwa ni pamoja na maji na umeme basi tutawahamishia huko,”alisema.

Alisema halmashauri yake imetenga Sh bilioni 3.7 kutokana na mapato yake ya ndani kwa ajili ya kutoa mikopo isiyokuwa na riba kwa vikundi va vijana, wanawake na wenye ulamavu.

Kunambi alitumia fursa hiyo kuliomba Bunge kuangalia namna ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma likatumia sehemu ya asilimia 10 ya fedha zinazotengwa kwa vijana, wanawake na wenye ulemavu kuzitumia kwa ajili ya kujenga miundombinu hiyo.

“Sheria inataka tutoe fedha hizo kwa vikundi, lakini ingekuwa sio sheria tungeweza kutumia sehemu ya fedha hizo ili kuharakisha ujenzi wa miundombinu kwa ajili ya wajasiriamali,”alisema.

Kutokana na ombi hilo, Mwenyekiti wa Kamati ya LAAC, Vedasto Mwiru alisema kama fedha hizo zinatumika kwenye jambo la maendeleo hakuna shida na kuwa Bunge litapitia utekelezaji huo ili kuhakikisha fedha zisitumike ndivyo sivyo.

Kutokana na kazi nzuri iliyofanywa na kikundi cha Youth Entrepreneur, ingawa walionekana kukosa elimu ya utunzaji fedha, Mbunge wa viti, Tauhida Galoss Nyimbo (CCM) aliwapongeza vijana hao na kutoa fursa kwa mwenyekiti wa kikundi hicho ya kupata mafunzo ya utunzaji wa fedha yatakayoendeshwa na wataalamu kutoka Nigeria na Afrika Kusini yatakayofanyika Zanzibar.

Wakiwa kwenye kikundi cha KAWADO, Mbunge wa Buyungu, Christopher Chiza (CCM) alikipongeza kikundi hiko na kuwataka kuweka hesabu zao vizuri ili wanapokaguliwa zisiwaletee tatizo lolote.

TAKWIMU za udumavu ...

foto
Mwandishi: Anastazia Anyimike

Post your comments